ASILIMIA
44 ya wapenzi wanaokwenda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupima
vinasaba (DNA), kwa ajili ya kujua uhalali wa watoto kwa baba,
wamethibitishiwa kuwa watoto hao si wa kwao.
Takwimu
za mwaka 2012 kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, zimeainisha kuwa
kati ya watu 90 waliokwenda kupima DNA, 40 ambao ni sawa na asilimia 44,
wameonekana kubambikiziwa watoto.
Takwimu
hizo za kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, zilionyesha kuwa katika
kesi 50 za waliokwenda kupima, matokeo yalionyesha kuwa ni wazazi halisi
wa watoto wao.
Hata
hivyo, idadi hiyo inayoonyesha kuwa kinababa siyo wazazi halisi wa
watoto, imeshuka ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2008/2009 ambazo
zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya watu waliochukua vipimo hivyo
wamebainika kuwa si wazazi halisi wa watoto hao.
Mkemia na
Mtambuzi wa Vinasaba vya Makosa ya Jinai, Gloria Machuve alisema jana
kuwa ni vyema ikitambulika kwamba takwimu hizo zinatokana na watu
waliokwenda kupima baada ya kutokea migogoro ya kimapenzi na siyo
takwimu iliyochukuliwa kutoka kwa Watanzania wote.
“Hatusemi
kuwa sasa wanaume wote Tanzania wanalea watoto ambao si wa kwao. Hizi
ni takwimu za waliokuja kupima; yaani wale wenye matatizo,” alisema.
Machuve
alisema katika maabara hiyo, kesi nyingi zinazoonyesha kuwa watoto hao
si halali, zimetokana na uhusiano wa ziada au usio rasmi baina ya wenza.
“Kwa
mfano, mwanamume ana mwanamke wa nje ya ndoa au mwenye uhusiano usio
rasmi, halafu mwanamke huyo anadai mtoto ni wa huyo mwanamume, mara
nyingi matokeo huwa si mazuri,” alisema Machuve.
Aidha,
Machuve alisema takwimu za kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 zinaonyesha kuwa
tabia ya upimaji imeongezeka miongoni mwa Watanzania.
Alisema
mwaka 2005/2006, kesi za upimaji wa vinasaba zilikuwa 96 na mwaka
2008/2009 kesi hizo zilikuwa 113 wakati mwaka 2009/2010, kesi za
waliokwenda kupima zilifikia 125.
Alisema
watu wengi wanaojitokeza kupima katika miaka ya karibuni wanataka
kufahamu uhalali wa watoto wao ili wawajibike kuwalea kihalali.
“Lakini pia kuongezeka kwa kesi za utambuzi wa vinasaba kunatokana na kukua kwa uelewa na uwezo wa kiuchumi,” alisema Machuve.
Alisema kuwa idadi ya upimaji wa DNA imeongezeka pia kwa watu wanaotaka kugawana mirathi na masuala ya uhamiaji.
“Wale
wanaoishi Ulaya wanapotaka kuchukua watoto au ndugu zao, ni lazima
wapimwe ili kuhakikisha, hivyo wanatuma vielelezo vyao kisha
tunavifananisha na vielelezo vya walio hapa,” alisema.
Machuve
alisisitiza kuwa katika kesi nyingi, wanawake hukimbia katika hatua za
upimaji na ni mara chache wanaume wakaukwepa mchakato huo.
Aidha,
Machuve alisema upimaji wa vinasaba vya makosa ya jinai umefanikiwa kwa
asilimia kubwa na asilimia 80 ya kesi zilitoa majibu chanya, yaani
vielelezo vilivyoletwa viliwanasa watuhumiwa wa makosa ya jinai.
“Kuna
kesi kama za ubakaji na mauaji ambazo tunaletewa vielelezo kama mbegu za
kiume au silaha na tulipofanya utambuzi wa vinasaba tuliupata ukweli
kwa kuwanasa watuhumiwa katika asilimia 80 ya kesi,” Machuve.
Upimaji wa jinsia tawala
Aidha, mkemia huyo alisema maabara hiyo inapima jinsia tawala kwa wale wanaozaliwa na utata wa jinsia.
Alisema
wapo watoto wanaozaliwa wakiwa na utata katika jinsia, kwa mfano ana
sura ya kiume na sauti lakini ana sehemu ya siri ya kike.
“Watu
kama hao wakifika hapa, tunaweza kuwapima ni jinsia ipi inatawala ili
wapatiwe matibabu na kisha waitumie jinsia inayotawala. Wanaweza
kufanyiwa upasuaji au kupewa vichocheo vya jinsia inayotawala,” alisema.
“Upimaji
wa DNA una gharama nyingi ambazo zinahitaji fedha, kuna gharama za
kuendesha mtambo, kuna dawa ambazo punje ndogo tu inagharimu Sh200,000,
hatuwezi kutoa bure huduma hii labda Serikali ilipie gharama hizo,”
alisema.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment