Pages

Thursday, March 27, 2014

POLISI WATANO naWAFANYABIASHARA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI


Gari ya magereza itumikayo kubeba wafungwa na mahabusu.
Askari Polisi watano na wafanyabiashara saba wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni Jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na kesi tatu tofauti ikiwamo unyang’anyi wa kutumia bastola na panga na kufanikisha uporaji wa mali zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 100.

Katika kesi ya kwanza, Meneja wa Kituo cha Mafuta cha GBP, Germano Chaba (30), mfanyabiashara Salum Musa (22), Koplo Rajabu Ugolo (39), Konstebo Albanus Kosa (32), mfanyabiashara Bahati Ahmed (35), Konstebo Salimon (30) na Kostebo Seleman (36) wanadaiwa kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia bastola na panga.
Washtakiwa hao walisomewa mashtakiwa yao mbele ya Hakimu Mkazi Athuman Nyamlani.
Wakili wa Serikali, Mmassy Bondo alidai kuwa, Februari 17, mwaka huu eneo la Boko Basihaya, katika kituo cha mafuta cha GBP, jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliiba Sh. 77,379,240 mali ya kampuni hiyo.
Ilidaiwa kuwa mara na kabla ya wizi huo washtakiwa walimtishia Joyce Warioba, Diana Sostenez, Ebeneza Kisanga na Peter Lawrence kwa bastola na panga ili kufanikisha unyang’anyi huo wa fedha.
Washtakiwa walikana mashitaka hayo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na washtakiwa watasomewa maelezo ya awali Machi 28, mwaka huu.
Katika kesi ya pili, Rajabu Mkendwa, Juma Ngwele, Konstebo Albanus, Musa, Omary Juma, Charles Mbelwa, Adamu Mkombozi, Ally Salum na Gerad Matutu walisomewa shitaka la unyang’anyi wa vitu mbalimbali vya ndani vyenye thamani ya Sh. milioni 4.5, mali ya Hong Tang.Ilidaiwa kuwa mara na kabla ya tukio hilo washtakiwa walimtishia kwa bastola na panga Suzan Juan na Nelson William.
Washtakiwa walikana mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Benedicta Beda na Wakili wa Serikali Hilda Kato alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.Hakimu Beda alisema kesi hiyo itatajwa Aprili 3, mwaka huu.
Katika kesi ya tatu, washtakiwa Musa, Omary Hamis, Mkombozi na Mbelwa walisomewa shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha mbele ya Hakimu Mkazi Selemani Mzava.
Wakili wa Serikali Tumaini Mfikwa alidai kuwa, Machi 6, mwaka huu maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliiba vitu mbalimbali vikiwa na thamani ya Sh. milioni 49 mali ya Deogratius Ngonyani. 
Ilidaiwa kuwa mara na kabla ya unyang’anyi huo, washtakiwa walimtishia kwa bastola Melisa Deogratias ili kufanikisha uporaji huo.Kesi hiyo itatajwa Aprili 3, mwaka huu na washtakiwa wote wamerudishwa mahabusu kwa kuwa mashtaka yanayowakabili hayana dhamana

No comments:

Post a Comment