Pages

Thursday, March 27, 2014

BUNGE MAALUMU LA KATIBA KUSITISHWA HADI MWAKANI, IKIWA..

Kikao cha Bunge Maalum la Katiba.

Kama mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba utaendelea kama linavyokwenda, uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, unaweza kusogezwa mbele hadi mwakani.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Pinda alisema muda uliopangwa kwa ajili ya Bunge Maalumu ni siku 70, lakini mpaka sasa kazi iliyofanyika ni moja, ya kutengeneza kanuni, na tayari siku 38 mpaka jana zimeisha, bado kazi rasmi ya kujadili rasimu haijaanza.
"Hatari ya kusogeza mbele uchaguzi wa serikali za mitaa ninaiona dhahiri, nadhani itabidi tu tumuombe Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, tusogeze mbele uchaguzi huu, ili kutoa nafasi kwa kazi zingine kuendelea hususan ya kutengeneza Katiba," alisema Pinda.
Mbali na uchaguzi huo, Pinda pia anapanga kupendekeza bunge hilo lisitishwe, ili kupisha muda wa Bunge la Bajeti kuanza kisha la Katiba liitishwe tena.
Alisema kama kazi ya bunge hilo itakuwa haijamalizika ifikapo mwishoni mwa Aprili mwaka huu, hatakuwa na namna isipokuwa kumuomba Rais Kikwete aliahirishe ili lipishe Bunge la Bajeti liendelee na kazi zake.
"Hatuwezi kuacha kazi zingine za serikali zikasimama, lazima ziendelee, na zitaendelea kama bajeti za wizara zitapitishwa, nadhani kama hatutakwenda sawa, tutamuomba tu Rais aahirishe bunge hili la Katiba, tufanye kazi hii nyingine iliyo mbele yetu.
"Tulijipangia siku 70, lakini tukasema kama hatutakuwa tumeikamilisha, basi tuongeze zingine 20, lakini kwa mwendo huu uliopo, sidhani kama tutaimaliza, nadhani inahitaji muda zaidi," alisema Pinda.
Wakati huohuoWaziri Mkuu Pinda alionya wajumbe wa bunge hilo kuacha kuwapotosha wananchi kuhusu hotuba zilizotolewa bungeni na Rais Kikwete na Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Alisema baadhi wanataka kuuaminisha umma kuwa rasimu iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba ikishajadiliwa na wajumbe ndiyo mwisho inapaswa kupitishwa.
"Umma ningependa ufahamu kuwa rasimu ile si mwisho wa kila kitu, bado inapaswa kujadiliwa na kuboreshwa na watu wa makundi mbalimbali," alisema Pinda.
Alisema hata Rais mambo aliyoyazungumza katika hotuba yake, yanalenga kuboresha na pia ni hoja zake ambazo wajumbe na Watanzania wanapaswa kuzijadili, kwa kuwa yeye pia ni miongoni mwa wananchi mwenye uhuru wa kutoa maoni.
"Na ndiyo maana katika kila alipokuwa akishauri jambo ama kutoa maoni yake kuhusu vifungu vilivyomo ndani ya rasimu, mwisho alisema haya ni maoni yangu, mnaweza kuyajadili ama kuyaacha," alisema Pinda.
Alisema kitendo cha baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa siasa ndani ya bunge hilo kutaka kuuaminisha umma kuwa Rais Kikwete aliwasilisha maoni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanalenga kupotosha ukweli.
"Ni kweli Rais ni Mwenyekiti wa CCM, ni dhahiri anaweza kubeba hisia za kichama, hilo lipo wazi, hata kama leo Profesa Lipumba ama Mbowe wangekuwa ni marais, na wenyeviti wa vyama vyao, hawataweza kuacha kubeba hisia za vyama vyao, huo ndiyo ukweli," alisema Pinda.
Alisema Rais alifanya kazi yake kama kiongozi wa nchi mwenye kupongeza pale palipo na mafanikio na kukosoa penye upungufu na kushauri kipi kifanyike. 
"Binafsi sioni kama kuna mahali Rais Kikwete alikosea, bali maneno haya yanayoendelea dhidi ya hotuba ile yana lengo la kupindisha ukweli," alisema Pinda.
Akizungumzia kero tatu za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi, alisema ni vyema wajumbe wakazijadili kwa kina ili katiba itakayoundwa ije na majibu.
Kero hizo ni pamoja na ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri, ardhi na utambulisho wa kitaifa.
Aliasa wajumbe wasikubali kupoteza utambulisho wa watu wa Zanzibar kwa makusudi.

No comments:

Post a Comment