Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amestushwa
na kuhuzunishwa na ajali kubwa iliyotokea usiku wa Jumamosi, Machi 29,
2014, katika Mkoa wa Pwani ikihusisha magari matano na kusababisha vifo vya
watu 21 na majeruhi 11.
Rais
Kikwete amevielezea vifo hivyo kuwa siyo vya lazima na ni upotevu wa bure wa
maisha ya Watanzania.
Katika
salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa
Mwantumu Bakari Mahiza, Rais Kikwete amesema: “Nimeshtushwa na kusikitishwa
na taarifa ya ajali iliyohusisha magari matano na iliyotokea jana usiku katika
Kijiji cha Kibupa, kilichoko kati ya Ikwiriri na Kibiti, Wilaya ya Rufiji, Mkoa
wa Pwani, ambako maisha ya Watanzania wenzetu 19 yamepotea na wengine 11
kujeruhiwa.”
“Kufuatia
ajali hiyo, nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Mwamtumu Bakari
Mahiza salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vifo vya
Watanzania wenzetu hao. Nimefadhaishwa mno na ajali hiyo ambako pia wenzetu
wengine 11wameumia.”
“Aidha,
kupitia kwako, nawatumia ndugu, jamaa na marafiki ambao wamepoteza wapendwa wao
katika ajali hiyo. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki na niko nao katika
kuomboleza upotevu huu mkubwa wa maisha ya wenzetu. Msiba wao ni msiba wangu na
machungu yao ni machungu yangu. Nawaombea subira na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu na naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aziweke
peponi roho za marehemu.”
Rais
pia amewapa pole wote walioumia katika ajali hiyo mbaya akisema: “Mkuu wa Mkoa
nakuomba pia uwafikishie pole zangu nyingi wote ambao wameumia katika ajali hiyo.
Nawaombea Baraka za Mwenyezi Mungu ili wapone
haraka na wapate tena nafasi ya kuendelea na shughuli za kuboresha maisha yao.”
Imetolewa
na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
30
Machi,2014
No comments:
Post a Comment