Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete ameridhia hati hiyo ioneshwe na
waandishi wa habari walikuwa wa kwanza kuiona hati halisi jana.
Hati hiyo ambayo mwandishi aliiona, imepigwa chapa na taipureta na ina kurasa tatu na jalada lake lina rangi ya damu ya mzee.
Aidha,
ili kuondoa upotoshwaji wa makusudi uliofanywa na wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba hasa kutoka Ukawa, Balozi Sefue alisema Rais Kikwete
ameridhia nakala zilizothibitishwa, ziwekwe kwenye Makumbusho ya Taifa
ili kila mwananchi aione na kuepuka upotoshaji huo.
Alipoulizwa kama
Hati hiyo pia ipo Umoja wa Mataifa, Balozi Sefue alisema: "UN
wasingeweza kuondoa kiti cha Tanganyika na Zanzibar kama kusingekuwapo
hati ya makubaliano ya kuwa nchi mbili zimeungana na kuwa Tanzania."
Alipoulizwa
ni kwanini Serikali ilichelewa kutoa hati hiyo na ni wapi inahifadhiwa,
Balozi Sefue alisema; "inatosha kuwahakikishia wananchi kuwa hati zote
tatu zipo salama, na kutokana na teknolojia zilizotumika, hati hizo
hazitolewi ovyo."
Alisema kuchelewa kuitoa kunaweza kuwa kosa kwa
kuwa hawakutarajia upotoshwaji kufikia ulipofikia, lakini akasisitiza
kuwa hawezi kusema inapohifadhiwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda aliliambia Bunge jana kuwa tayari ametumiwa na Ikulu,
nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyosainiwa na Mwalimu
Nyerere na Abeid Karume.
Alisema kutokana na hatua hiyo, alimkabidhi
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu Samuel Sitta nakala hiyo, wakati Bunge hilo
likisubiri hati iliyothibitishwa kisheria itakayowasilishwa katika
Bunge hilo ndani ya siku mbili kati ya leo na kesho.
Akizungumzia
hatua hiyo, Sitta alisema itakapowasili hati iliyothibitishwa kisheria,
ataitoa nakala na kusambaza kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba
ili waisome na kuwasaidia katika kujenga hoja za majadiliano bungeni.
Akizungumzia
ilipokuwa hati hiyo, Balozi Sefue alisema hati hiyo ipo, ilikuwepo siku
zote na kufafanua kuwa ni lazima baadhi ya hati muhimu zihifadhiwe kama
mboni ya jicho.
"Lazima tukubaliane kuwa zipo hati fulani ambazo ni
kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru,
ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho.
"Hati hizo ni pamoja na
Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa
Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya
mwaka 1964. Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalumu ambayo ni
salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi,
tunazifungua ili kuzihifadhi kwa namna yoyote ile," alisema Balozi
Sefue.
Kwa kuwa upotoshwaji huo usiotarajiwa umefanyika kwa nguvu
katika Bunge Maalumu la Katiba, Balozi Sefue alisema kama Bunge Maalumu
likiomba nakala halisi, kama hawataridhika na nakala zilizothibitishwa,
ombi hilo litafikishwa kwa Rais Kikwete na akiridhia, itapelekwa
wakaione.
"Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum,
nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama
Hati ipo au la.
"Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye
Makumbusho ya Taifa, ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50
ijayo na kuzidi, aione," alisema Balozi Sefue.
"Sasa maneno yamekua
mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha
wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.
"Hivyo,
kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dk Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amaan Karume.
Aliendelea kusema lengo ni; "Ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli.
Hati hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi."
Balozi
Sefue aliendelea kueleza masikitiko ya Serikali, kwamba leo, miaka 50
baada ya Mungano, kumeibuka dhana potofu inayojengwa kuwa Muungano huu
si halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano.
Alisisitiza kuwa kwa
upande wa Serikali wamesikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito
kwamba labda waasisi hawakuwa makini au walifanya kiini macho na
kusema hawakutarajia wawepo Watanzania wenzao wafikie hapo.
"Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi walichosaini waasisi wetu.
"Waasisi
wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia saini
Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya
kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho hicho kwa
miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.
"Mambo yote mawili
yametusononesha sana sisi serikalini, na bila shaka yamewasononesha
wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda waasisi wa Taifa letu na
kuuenzi Muungano wao," alisema Balozi Sefue.
Alifafanua kuwa madai ya
kuoneshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi, lakini Serikali
haikuamini kwamba hali ingefikiwa ilipofikia, ambapo watu wamethubutu
kudai na kuapa kuwa hati hiyo haipo.
"Matumaini yetu ni kuwa baada ya
leo (jana) tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na
uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna
msingi imara wa kisheria," alisema.
Sehemu kubwa ya upotoshaji
ulisambazwa kwamba hakuna Hati za Muungano, ulilenga kubatilisha
Muungano uliodumu kwa miaka hamsini sasa, ili hoja ya kubadilisha muundo
wa Muungano kutoka kuwa serikali mbili kwenda serikali tatu ipate
nguvu.
Waliokuwa wakidai kuwa hati hizo hazipo, hasa kutoka kundi la Ukawa, walitumia namna mbalimbali za kufuta uhalali wa Muungano.
Wakati
kamati za Bunge Maalumu la Katiba zilipoanza kukaa na kujadili Rasimu
ya Katiba, hoja ya kwanza ya wajumbe hasa kutoka Ukawa, ilikuwa Hati ya
Muungano iliyotiwa saini na waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na
Shekhe Karume iwasilishwe waione.
Wajumbe hao walipewa nakala ya
Sheria ya Kuridhia Muungano iliyotiwa saini na Mwalimu Nyerere na
aliyekuwa Katibu wa Bunge wakati huo, Pius Msekwa.
Hata hivyo, baadhi
ya wajumbe hasa kutoka Ukawa unaoundwa na vyama vya upinzani ukiongozwa
na CUF na Chadema, walidai sahihi zilizoko katika hati hizo,
zimeghushiwa.
Kutokana na utata huo, Kamati namba 2 ya Bunge Maalumu
la Katiba, ilimuita Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, na
akasisitiza kuwa sahihi hizo ni halali.
Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kwamba walilazimika kumuita Msekwa
ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa.
Katibu wa Bunge la Katiba,
Yahya Hamis Hamad naye alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja
tu, hivyo siyo rahisi kupelekwa bungeni Dodoma.
"Ile hati ya Muungano
ipo Dar es Salaam, lakini tunahofia kuileta maana inaweza kupotea kwani
ipo moja tu, sasa ambacho tutakifanya inaweza kutolewa nakala na
kuthibitishwa na mawakili na ikaja nakala hapa Dodoma iwapo wajumbe
wanahitaji," alisema Hamad.
Baada ya majibu hayo, wajumbe hao
waliendelea kutafuna namna ya kubatilisha Muungano, ambapo walisema
Sheria Namba 22 ya 1964 ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuridhia
Muungano nayo haijulikani ilipo.
Wajumbe hao walikiri kuwa Bunge la
Tanganyika ushahidi wameletewa kuwa waliridhia Muungano Aprili 25, 1964
na waliosaini ni Julius Nyerere, Katibu wa Bunge hilo, Pius Msekwa na
aliyekuwa Spika Adam Sapi Mkwawa, lakini kwa Zanzibar haupo.
Walidai
wa kuwa kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman
kusema hajawahi kuiona sheria hiyo, kinadhihirisha kuwa haipo.
Pamoja
na Msekwa kukiri kwenye kamati hiyo kuwa saini iliyopo kwenye hati ya
makubaliano ya Muungano ni yake, lakini wajumbe hao waliendelea kudai si
yake na imechezewa.
Wajumbe walihoji tofauti baina saini iliyopo kwenye sheria hiyo na saini yake katika nyaraka nyingine rasmi.
Wajumbe
walioibua hoja hiyo wakiongozwa na Godbless Lema, pia walitilia shaka
matumizi ya kompyuta katika sheria hizo zilizoandikwa mwaka 1964.
"Mwaka
1964 hakukuwa na kompyuta lakini hapa tunaona sheria zimeandikwa kwa
kompyuta na hata sehemu ya saini ya Msekwa na Nyerere kuna herufi
zimeandikwa kwa kompyuta," alinukuliwa Lema.
Katika maelezo yake
Msekwa licha ya kukiri upungufu, aliwakumbusha wajumbe kuwa siku ya
kusainiwa hati hizo, picha zilipigwa na zipo hadi sasa.
Hata
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Sitta alisema anahisi sahihi zimechezewa
baada ya kufutika, lakini sheria hiyo ni halisi na iliwekwa sahihi na
Mwalimu Nyerere, Spika Mkwawa na Msekwa.
No comments:
Post a Comment