Pages

Thursday, April 10, 2014

MSAADA WAKO UNAHITAJIKA KUWEZA KUOKOA MAISHA YA WAKINA DADA HAWA

Dada Zuhura Juma (27) mkazi wa Temeke jijini Dar.
HAWAKUJUA kama wangekuwa hivi, lakini imetokea tu! Zuhura Juma (27) mkazi wa Temeke jijini Dar na Disnia Rajab, mwenye makazi yake Gezaulole jijini Tanga, wapo katika mateso makali kwa muda wa miaka kumi sasa baada ya miguu yao kuvimba kwa namna ya kusikitisha. 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa gazeti hili, wanawake hao walisema walipatwa na ugonjwa huo bila kutarajia. Awali walianza kuhisi maumivu ya kawaida na kuamini wangepona, lakini miguu yao iliendelea kuvimba siku baada ya siku.
Dada Disnia Rajab mkazi wa Gezaulole jijini Tanga.
Akisimulia mkasa wake, Zuhura alisema ugonjwa huo ulimpata mwaka 2004 alipopata ujauzito wa mtoto wake wa kwanza.
Dada Disnia Rajab kabla ya kupata ugonjwa.
“Kwanza nilipata tatizo la presha ambayo ilisababisha miguu kuvimba lakini sikuwa na shaka kwani nilijua ni hali ya kawaida kwa mama mjamzito  kuvimba miguu kisha hurejea katika hali ya kawaida.
“Baada tu ya kujifungua, mguu mmoja ulirudi kama kawaida lakini huu (wa kushoto) ukawa bado, nilipokwenda hospitali waliniambia nisijali utarudi wenyewe kama zamani.
“Wakaniambia niendelee kunywa vidonge vya Laxis walivyonipa kwa ajili ya kupunguza maji.
“Lakini cha ajabu, siku moja hali yangu ilizidi kuwa mbaya, nikaenda Hospitali ya Temeke. Wao walishindwa kunitibu na kunihamishia Muhimbili ambako nililazwa kwa muda wa siku tano,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani, alianzishiwa kliniki ya ugonjwa wa matende iliyopo Muhimbili lakini katika hali ya kusikitisha madaktari walimwambia hawezi kutibiwa nchini.
“Kwa kweli nililia kwa uchungu maana nilijua uwezo wa kwenda huko nje ya nchi sina, nikaona nakufa na urembo wangu.”

 
Kwa upande wake, Disnia alisema yeye pia aliupata ugonjwa huo mwaka 2004. Kwanza alihisi maumivu ya kichwa ghafla usiku huku mwili ukitoka jasho. Asubuhi kulipokucha, alikuta mwili umevimba.
“Nilichukuliwa hadi Hospitali ya Bombo. Pale nililazwa kwa siku saba, presha ilikuwa juu, nikawekewa dripu, nilichomwa sindano presha ikashuka. Uvimbe wa mwili ukapungua isipokuwa mguu huu wa kushoto, madaktari waliniruhusu kurudi nyumbani ili nianze kliniki,” alisema.
Alisema pamoja na kuanza kliniki, hali ikazidi kuwa mbaya. Amezunguka hospitali nyingi na kutibiwa, lakini kote huko imeshindikana hadi alipoambiwa asingeweza kutibiwa nchini na anatakiwa kuwa na fedha kiasi kisichopungua shilingi milioni 20.
Licha ya matatizo ya maumivu yanayomfanya asiwe na uwezo wa kujitafutia riziki, pia watoto wake watatu aliozaa na mumewe aliyemkimbia baada ya kupatwa na ugonjwa huo, wamekuwa wakimtegemea yeye.
WANACHOOMBA KWA WATANZANIA

Kama kuna Mtanzania yeyote aliyeguswa na matatizo ya wanawake hawa, anaombwa kutoa aina yoyote ya msaada anaoona unafaa huku ikizingatiwa kuwa, kutoa ni moyo  na si utajiri.
Kwa Zuhura Juma, tumia simu namba 0754 021301 au 0717 319555 na kwa Disnia Rajab, wasiliana naye kwa simu namba 0755 033718, 0685 836159 au 0719 546505.

No comments:

Post a Comment