Pages

Thursday, April 10, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA CCM SHINYANGA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAREHE 07.04.2014
CCM MKOA WA SHINYANGA YA LAANI KAULI YA
MBUNGE WA JIMBO LA KAHAMA JAMES LEMBELI
KUWA “CCM SIYO MAMA YANGU”
Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga KIMELAANI vikali kauli ya Mbunge James Lembeli Mbunge wa Jimbo la Kahama aliyoitoa kwenye vyombo ya habari hivi karibuni iliyosema “CCM SIYO MAMA YANGU”.
Kwa hiyo Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga na wana CCM wote kwa ujumla wamestushwa na kauli ya Mbunge Lembeli anayetokana na CCM kwani kauli hii hatukutegemea sote kama ingeweza kutolewa na Mwanachama ambaye tena ni Kiongozi ndani ya Chama.
Tunaomba ieleweke na tunautaarifu Umma na wana CCM wote kuwa CCM haina tatizo kabisa na msimamo wa Mbunge James Lembeli kuhusu msimamo wake wa serikali moja, mbili, tatu au nne na hata serikali ya Tanganyika kwani huo ni uhuru wake binafsi. Tatizo letu kubwa kwake ni kauli aliyoitoa kuwa “CCM SIYO MAMA YANGU” kwani kauli hiyo ameitoa sio mahali pake na haihusiki na utashi wake binafsi katika msimamo alionao katika BUNGE LA KATIBA. Kauli hii inaukakasi na ni sawa na kukinajisi Chama.
Lakini jambo la ajabu na la kushangaza ni kuhusu kulitumia jina la Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere vibaya, amekuwa akijifananisha na kauli ya Baba wa Taifa tungependa atambue kuwa Lembeli hana hadhi na sifa ya kujifananisha na Baba wa Taifa; kwani kujifafanisha kwake na Baba wa Taifa huko ni matumizi mabaya ya kujitwisha sifa asizostahiki kwani Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere alikuwa na karama, hekima na busara kubwa za pekee na aliheshimika Dunia kote pia alikuwa anatoa kauli zake kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati huo.
Kwani Baba wa Taifa kila jambo lililokuwa linahusu swala la Chama na Mstakabali wa Taifa alitumia vikao kulizungumza sio anavyofanya Lembeli kuropoka ovyo, kutumia ubabe na kukosa staha kwa Chama.
Tabia ya Mbunge Lembeli ya kukidhihaki Chama imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, lakini tunapenda atambue na kumkumbusha kuwa Lembeli hapo alipofika na jeuri yote na umaarufu alionao unatokana na CCM, kabla ya mwaka 2005 hakuna Mtanzania aliyemfahamu popote nchini.

Lakini baada ya kupewa ridhaa na CCM na hatimaye kuchaguliwa Ubunge ndipo akajenga umaarufu uliotokana na CCM. Lakini jingine tunapenda kumkumbusha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Lembeli alikuwa na wakati mgumu sana ndani ya Chama na nje ya Chama lakini Chama na Wanachama wakampigania kwa hali ya juu sana na kwa mazingira magumu na hatimaye ushindi ukapatikana.
Leo shukrani anazotoa kwa Chama ni kukiambia CCM SIO MAMA YAKE.
Basi na kama Lembeli anaona CCM SIO MAMA YAKE ni vyema akatueleza MAMA YAKE NI NANI – KISIASA na kama ana MAMA MWINGINE KISIASA ni VYEMA AKAMFUATA HUYO MAMA HUKO ALIKO anayeona atamfaa kumpa umaarufu zaidi ya CCM.
Mwisho CCM Mkoa wa Shinyanga hakitakuwa tayari na hakitawavumilia wanachama na viongozi wake wenye tabia kama ya Lembeli ya kuendelea kukidhalilisha Chama hadharani. 
Lakini pia Chama kitaendelea kuheshimu Demokrasia ndani ya Chama na Uhuru wa mawazo unaofuata maadili, miiko na taratibu za Chama ndani ya vikao.
Asanteni kwa kunisikiliza.

Taarifa hii imeandaliwa na Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga na imesomwa na:-

Ndugu Emmanuel S. Mlimandago
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM
Mkoa wa Shinyanga

No comments:

Post a Comment