John Mnyika. |
Rufaa ya Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, John Mnyika, anayepinga uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Bunge Maalumu, imepelekwa kwa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge hilo.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, alisema hayo jana alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Mnyika kuhusu rufaa yake.
Sitta alisema rufaa hiyo ya Mnyika, ipo mezani mwa Kamati hiyo ya Kanuni, na ikimaliza kazi yake, itatoa taarifa kwake na yeye atatoa taarifa kwa Bunge Maalumu.
Mnyika alisema alipeleka hoja ya kukata rufaa kupinga uteuzi wa wajumbe watano wa Kamati ya Uongozi, wanaoteuliwa na Mwenyekiti na wajumbe wengine.
Alisema amekata rufaa kupinga Kamati ya Uongozi kwa kuwa ina sura ya upande mmoja, kwa maana kuwa imetawaliwa na wajumbe kutoka CCM na wajumbe wengi wanatoka Tanzania Bara.
Wajumbe watano walioteuliwa na Mwenyekiti ni Fakharia Khamisi Shomari, Mary Chatanda, Profesa Ibrahim Lipumba, Amon Mpanju na Hamoud Abuu Juma. Hata hivyo Profesa Lipumba alijitoa katika nafasi hiyo.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo, ni viongozi waliochaguliwa kuongoza kamati 12 zitakazojadili ibara na sura za rasimu ya Katiba pamoja na Kamati ya Uandishi na Kamati ya Kanuni.
No comments:
Post a Comment