Meneja huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na
jukumu la kupanga bei za mafuta za kila mwezi, alihudhuria kikao hicho
mjini Dodoma kwa siku mbili; Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu mambo
mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa
fedha unaotolewa na Ewura kwenda kuhudumia umeme vijijini (Rea) na fedha
za mfuko wa barabara.
Jeshi la Polisi, Mkoa wa Temeke limethibitisha
tukio hilo na kueleza kuwa meneja huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia
tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo Vituka wilayani Temeke.
Nyumbani kwa meneja huyo wa Ewura, kulikuwa na
waombolezaji waliokuwa kwenye vikundi na kikao cha maandalizi ya mazishi
kilifanyika ndani ya nyumba ya marehemu iliyopo Yombo Vituka na baadaye
kuhamia nyumba ya jirani.
Kamati ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge
wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ilikutana na maofisa wa Ewura,
akiwamo Gashaza na wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kugundua
kuwapo kwa tofauti katika takwimu za kiwango cha mafuta kilichostahili
kutozwa kodi.
Gashaza alikwenda Dodoma kutoa ripoti ya Ewura
kwenye kamati hiyo ya Bunge akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura,
Felix Ngamlagosi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo,
takwimu za Ewura ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi
ya zile zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe
takwimu za mamlaka ya mapato.
Habari hizo, zinasema baada ya kurejea Dar es
Salaam juzi majira ya saa tatu usiku, Gashaza hakwenda nyumbani kwake na
badala yake alikwenda kwenye hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako
mkewe na ndugu yake mmoja walimfuata na akawaeleza kuwa anahisi
kutishiwa maisha yake.
Baadaye walifanya maombi maalumu kabla ya kuachana naye.
Inadaiwa kuwa marehemu aliomba akalale hotelini
kwa sababu hakuona kama ana amani kulala nyumbani kwake na ilipofika
asubuhi alikutwa ‘amejinyonga’ ndani ya chumba alicholala hotelini humo.
Nyumbani kwa marehemu waombolezaji walikusanyika
katika makundi, lakini baada ya kukaa katika kikao cha familia walitoka
na kauli moja kuwa hawatasema chochote na kwamba jukumu hilo libaki
mikononi kwa polisi.CHANZO MWANAINCHI
Polisi wathibitisha
No comments:
Post a Comment