Pages

Monday, May 19, 2014

Tazara sasa ‘mahututi’ yaomba kusaidiwa




 
Abiria waliokuwa wasafiri na treni ya TAZARA, kwenda katika mikoa ya Mrogoro, Iringa na Mbeya, wakiwa kwenye foleni Stesheni ya Dar es Salaam, juzi, ili kurejeshewa fedha zao, baada ya wafanyakazi wa shirika hilo kugoma wakidai mishahara yao ya miezi minne. Picha na Rafael LubavaDar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Ronald Phiri amesema shirika hilo linaweza kufa iwapo wabia wake (Tanzania na Zambia), hawatachukua hatua za dharura ikiwamo kuongeza mitaji ya kuchochea kasi na ufanisi katika uzalishaji.
Kauli hiyo imekuja baada ya siku nne mfululizo za mgomo wa wafanyakazi zaidi ya 3000 wakidai mishahara ya Februari hadi Mei.
Akizungumza jana na gazeti hili, Phiri alisema kwa sasa shirika hilo lina vichwa 16 tu vya treni ambavyo siyo vizima.

 
Aliongeza kutokana na mazingira hayo, shirika limekuwa likizalisha tani 280,000 zinazoingiza Sh3.2 bilioni, huku matumizi yake yakiwa juu kwa Sh4.8 bilioni ikiwa ni sawa na hasara ya Sh1.6 bilioni kila mwezi.
“Mishahara pekee ni mzigo mkubwa kwa shirika, nadhani ipo sababu ya nchi mbili hizi kuongeza mtaji,” alisema Phiri.
“Wateja wamepungua sana na sababu kubwa ni kuchelewa kufika mizigo yao kutokana na treni kuharibika njiani mara kwa mara,” alisema.
Alisema jambo lingine ambalo kwa kiasi kikubwa limesababisha utendaji kuzorota ni upatikanaji wa tabu wa mafuta ya treni.
Phiri alisema hatua ya mgomo unaoendelea kwa sasa ndiyo unazidi kuongeza majeraha mara mbili ndani ya shirika hilo ukilinganisha na hasara iliyojitokeza mwaka jana kutokana na mvua.
Alisema pamoja na misaada inayopatikana kutoka China, shirika hilo bado linajiendesha kwenye wakati mgumu.
“Shirika lilianza kujiendesha kwa hasara tangu miaka ya 1990 hadika 2000 kwa sababu za uchakavu wa miundombinu na vichwa vya treni. Mfano mwaka jana tulipata hasara kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu kuanzishwa ,” alisema Phiri.CHANZO MWANAINCHI

No comments:

Post a Comment