Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, June 12, 2014

BAJETI KUU KUSOMWA LEO BUNGENI DODOMA

Watanzania leo wanaelekeza macho na masikio yao mjini Dodoma, kusikiliza Hotuba ya Bajeti ya Serikali, inayotarajiwa kusomwa saa 10 kamili bungeni na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Tayari Waziri Saada alishaeleza kuwa makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, unaoanza Julai mwaka huu, yatakuwa Sh trilioni 19.6 kutoka makadirio ya Sh trilioni 18.2 ya Bajeti inayoisha muda wake.
Vipaumbele vya Bajeti hiyo, kwa maana ya miradi itakayozingatiwa zaidi, ni iliyo katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaohusisha sekta sita za Kilimo, Elimu, Maji, Utafutaji rasilimali fedha, Nishati, Uchukuzi na Uboreshaji wa Mazingira ya kufanyia biashara na Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano.
Akisoma mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, alisema mapendekezo ya mpango huo, yana vipaumbele vitano.
Cha kwanza ni miundombinu, kikifuatiwa na 

 
kilimo, viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kuongeza thamani, maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi na uendelezaji wa shughuli za utalii, biashara na fedha.
Katika hotuba hiyo, Watanzania wengi watakuwa makini kusikiliza bidhaa na huduma zitakazoongezwa kodi, jambo linalotarajiwa kuongeza bei ya bidhaa za huduma husika katika soko.
Katika bajeti inayoishia,  Serikali iliongeza kodi kwenye magari makuukuu, bia, vinywaji vikali na baridi ambavyo kodi imekuwa ikiongezwa kila mwaka na kuwaathiri watumiaji.
Kutokana na hali hiyo wanywaji pombe na sigara baada ya bajeti ya mwaka juzi ya 2012/2013, walilazimika kutumia fedha nyingi ili kupata huduma hizo kwa kiwango kile kile katika mwaka huu wa bajeti unaoisha.
Bidhaa zisizokuwa za mafuta ambazo zilifanyiwa marekebisho na kuongezwa kodi ni mvinyo, pombe, vinywaji vikali, na sigara.
Ushuru pia uliongezwa kwenye magari yasiyokuwa ya uzalishaji na yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20 mpaka asilimia 25.
Lengo la Serikali katika hilo, lilikuwa kupunguza uagizaji wa magari chakavu ili kulinda mazingira na kupunguza ajali za mara kwa mara.
Katika bajeti hiyo, vijana wa bodaboda walicheka baada ya Serikali kusamehe ushuru wa barabara kwa pikipiki hizo za biashara.
Moja ya kivutio kikubwa cha Bajeti inayowasilishwa leo, ni matarajio ya wafanyakazi kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu, ya kuongeza mshahara wa kima cha chini na kupunguza kodi ya mshahara (PAYE).
Rais Kikwete alisema Serikali itaendelea kuongeza mshahara wa kima cha chini na kubainisha kuwa mwaka 2005 alipoingia madarakani, alikuta mshahara wa kima cha chini ni Sh 65,000 na kukipandisha taratibu hadi kufikia Sh 240,000 cha sasa.
Kuhusu kupunguza PAYE, Rais Kikwete alisema kusudi la Serikali ni kupunguza kodi hiyo ya mshahara kutoka asilimia 13 inayotozwa sasa, ifikie katika kiwango cha tarakimu moja.
Kuhusu misamaha ya kodi ambayo mwaka huu imekuwa gumzo bungeni, huku wabunge wengi wakitaka ipunguzwe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alinukuliwa akisema wafanyabiashara na vigogo wanaokwepa kodi kwa kujificha kwenye mwavuli wa misahama, hawako salama.
“Tutafuatilia kikamilifu kwa kuwa wapo watu wanaingiza bidhaa wanapewa msamaha, lakini ukija kwenye huduma za jamii unakuta bidhaa hizo zinauzwa kibiashara,” alisema.


Mwigulu pia alizungumzia ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kufafanua kuwa, yatadhibitiwa.


“Bahati nzuri niliyonayo, sikuzaliwa na chembe ya woga, kwa hiyo kwenye hili hakuna mkubwa wala mdogo, hakuna mtu atagusa fedha ya umma kwa kukwepa au kwa kutumia vibaya kodi ambayo ilishakusanywa halafu akapona asiguswe,” alisema.

Mwigulu alisema katika Bajeti ya Serikali ya 2014/2015, yapo mambo ya msingi matano, ambayo yatasimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa tofauti na zilizopita.

Mbali na kuondoa misamaha ya kodi, pia makusanyo ya ndani yatatiliwa mkazo zaidi ili kujenga uwezo wa kujitegemea wenyewe badala ya kutegemea wahisani.

Jambo la tatu alisema ni kuhakikisha Serikali inapeleka fedha kwenye mahitaji muhimu na kwa wakati, ili fedha za maendeleo zitumike kama ilivyokusudiwa.

Jambo la nne litakalozingatiwa kwa mujibu wa Mwigulu, ni usimamizi wa fedha zinazopatikana kwani pamoja na makusanyo kidogo, lakini pia kuna uvujaji.

“Tunataka fedha inayopatikana na kupangiwa kazi fulani itumike kwa shughuli iliyokusudiwa. Tutahakikisha tunasimamia na kudhibiti matumizi yake,” alisema.

Naibu Waziri huyo wa Fedha alisema eneo la tano ambalo litaangaliwa ni fedha ambazo hazitokani na kodi, bali zinachangwa na wananchi na wadau wengine katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema eneo hilo ni muhimu mbalo Serikali inaona kuna haja ya kulisimamia vizuri, ili kuhakikisha fedha za  wananchi zinatumika vizuri.

Kwa upande wa Kenya, hotuba  ya Bajeti ya Serikali ya Kenya, itasomwa na Waziri wa Fedha, Henry Rotich. Katika taarifa yake kwa wabunge wa Kenya mwezi Machi mwaka huu, Rotich alieleza kuwa Bajeti ya Kenya kwa mwaka wa Fedha wa 2014/15,  itakuwa Shilingi za Kenya Trilioni 1.8.

Nchini Uganda, Waziri wa Fedha wa Uganda, Maria Kiwanuka ndiye atakayesoma hotuba ya Bajeti ya Serikali ya Uganda kwa mwaka wa fedha 2014/15.

Kiwanuka ataeleza hatua mbalimbali za kuinua uchumi, kupunguza kodi mbalimbali na kudhibiti mfumko wa bei.

Hivi karibuni, Kiwanuka alikaririwa akisema kuwa uchumi wa Uganda unaendelea kukua kwa kasi, lakini siyo katika viwango vya miaka 1990 na 2000, ambapo ulikua kwa asilimia 7.

Kwa upande wa Rwanda, hotuba ya Bajeti ya Serikali itasomwa na Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi wa Rwanda, Claver Gatete.

Bajeti yote ya  Rwanda kwa mwaka 2014/15 inatarajia kuwa Faranga za Rwanda bilioni 1,753. Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), uchumi  wa Rwanda unatarajia kukua kwa asilimia 6 katika mwaka wa fedha 2014/15, ukilinganisha na asilimia 4.6 mwaka 2013.

Burundi, Waziri wa Fedha, Mipango ya Uchumi na Maendeleo wa Burundi, Tabu Abdallah Manirakiza, ndiye atasoma bajeti ya Serikali ya Burundi kwa mwaka wa fedha 2014/15.

Tayari Shirika la Fedha Duniani (IMF) limekadiria kuwa uchumi wa Burundi, utakua kwa asilimia 7 katika mwaka 2014/15, ukilinganisha na asilimia 4.5 mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment