Waziri Mkuu Mstaafu Mh Edward Lowassa.
Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa amesema vijana 10,500 waliojitokeza hivi karibuni kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufanya usaili wa nafasi 70 za kazi katika Idara
ya Uhamiaji, ni ishara kuwa bomu la ajira litalipuka muda wowote.Akizungumza na
waandishi wa habari jana nje ya Viwanja vya Bunge, Lowassa alisema Serikali ni
lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000
wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini.Wasomi hao wa fani mbalimbali
walijitokeza katika uwanja huo Ijumaa iliyopita, kuanzia saa 12 asubuhi
wakisubiri kufanyiwa usaili huo.Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri
Mkuu mwaka 2008, amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua
kukabiliana na tatizo la ajira na akisema ni bomu linalosubiri kulipuka.Mbunge
huyo wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia
kwenye malumbano makali na Waziri
wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kuhusiana na suala la ajira kwa
vijana.Kabaka akiwa bungeni, Machi 21, 2012 alitoa takwimu za namna Serikali ilivyokuwa
inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa ameeleza tatizo
la ajira linavyowaathiri vijana.
Jana, Lowassa kuongezeka kwa makundi ya vijana wanaopora
watu katika maeneo mbalimbali nchini ni ishara ya ukosefu wa ajira. “Watanzania
sasa tupo milioni 48 na kila mwaka vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu vyuo vikuu
na kazi hakuna, pamoja na hilo hatuambiwi ni vijana wangapi ambao hawana kazi,”
alisema Lowassa.
Alisema lazima Serikali itengeneze ajira kwa wananchi wake,
huku akimtolea mfano Rais wa Marekani, Barack Obama kwamba alishinda awamu ya
pili kwa sababu ya kutengeneza ajira.
“Mfano mzuri ni katika uanzishwaji wa viwanda. Tunapofikiria
kuanzisha kiwanda cha pamba kwanza lazima tuangalie tutatengeneza ajira ngapi,”
alisema.
Katika kuonyesha kuwa ajira sasa ni tatizo nchini, juzi
jioni wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu, Naibu Spika Job Ndugai alisema Mtanzania
mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015 ili aweze kuelekewa kwa wananchi ni
lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana
hawaendi shule lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha
nne, cha sita na vyuo vikuu. Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za
mwisho za Serikali ya awamu ya nne, wale wanaojipanga kwa awamu ya tano kama
hawataongelea ajira basi waandike wameumia.”
Ndugai alisema vijana wasio na kazi ndiyo wapigakura wakubwa
na kusisitiza kuwa mgombea yeyote makini ni lazima afikirie suala la ajira kwa
vijana.
No comments:
Post a Comment