James Chotamasogo akitembelea magongo baada ya kukatwa mguu
wa kushoto katika Hospitali ya Ocean Road, kutokana na ugonjwa wa kansa.
MWANAFUNZI James Chotamasogo (20) aliyemaliza kidato cha nne
mwaka jana katika Shule ya Sekondari ya Road Baden Powel inayomilikiwa na
Kanali Mstaafu, Idd Omar Kipingu, iliyopo jijini Dar amekatwa mguu wa kushoto
katika Hospitali ya Ocean Road, kutokana na ugonjwa wa kansa.Kufuatia tukio
hilo, kijana huyo ambaye ni yatima amekosa pakwenda hali iliyomfanya Kanali
Kipingu kuchukua jukumu la kumlea.
Mwandishi wetu alimtembelea katika Hospitali ya Magonjwa ya
Kansa ya Ocean Road, jijini Dar wiki iliyopita ambapo alikuwa na haya ya
kusema:
“Mimi ni mtoto wa pili kati ya watatu katika familia yetu,
nikiwa mdogo baba aliugua akafariki dunia, tulibaki na mama ambaye muda wote
alizidiwa na majukumu, hata hivyo naye hakuchukua muda kwani baada ya miezi
miwili tangu baba afariki naye akaaga dunia, tulibaki peke yetu tukiwa hatuna
uwezo wa kujihudumia.
“Tulikuwa tukiishi kwa kutegemea kilimo na uvuvi wa samaki
katika Kijiji cha Ndewele, Kilolo mkoani Iringa.
Maisha yalizidi kuwa magumu lakini nilipofanya mtihani wa
kuhitimu darasa la saba, nilifaulu kwenda kidato cha kwanza tatizo hapakuwa na
mtu wa kuninunulia vifaa vya shule.
James Chotamasogo akiwa ameketi na magongo yake.
Kufuatia hali hiyo, nikaja Dar kutafuta kazi ambapo nilipata
kibarua cha kutunza bustani na mifugo.
“Nilimweleza bosi wangu huyo kuwa bado nilihitaji kuendelea
na masomo, alikubali kunisomesha kwa kunilipia ada kutokana na mshahara wangu.
Nilisoma kwa bidii nikijua nitabadili maisha ya familia yetu.
“Siku moja nikiwa naendesha baiskeli nikiwa nimebeba majani
ya ng’ombe, niligongwa na gari eneo la Kimara, nikaangukia mtaroni.
“Niliumia lakini nilijikokota hadi nyumbani kwa bosi wangu,
wakati huo hakuwepo, alikuwepo mke wake ambaye hakunijali wala kunipeleka
hospitali, damu ilivilia katika mguu wa kushoto, nilitumia barafu kuukanda ili
kupunguza maumivu, nilikuwa naenda shule huku naumwa, baadaye nilishindwa
kufanya shughuli za nyumbani, wakanifukuza nikiwa kidato cha tatu.
“Mzee mmoja alinionea huruma alinichukuwa nikawa naishi
kwake, ada ya shule nikawa silipiwi bali chakula na pa kulala nilipewa, baada
ya siku chache nikafukuzwa shule kwa kukosa karo.
“Nilienda kwa msaidizi wa mkuu wa shule nikamweleza matatizo
yangu ili nisilipe ada, alifikisha kilio changu kwa mmiliki wa shule ambaye ni
Kanali Kipingu, alikubali nisome bure na niishi pale shuleni bwenini.
“Mguu wangu ulizidi kuuma nikawa nashindwa kwenda shule,
Kanali Kipingu alinipeleka Hospitali ya Bagamoyo,Lugalo,
IMTU na Nasana nako ikashindikana kupona ndipo akanipeleka Kibaha kwa Dk. Bake
aligundua nina ugonjwa wa kansa ambayo ilitokana na kucheleweshwa kutibiwa
majeraha niliyopata, nilihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, madaktari
walinieleza kwa hali iliyofikia, mguu ulitakiwa kukatwa wakashauri nifanye
kwanza mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.
“Ilinibidi nifanye mtihani, lakini kwa mawazo kwani
nilifikiria maisha yangu yatakavyokuwa huko mbeleni, kwa sasa nipo hapa
Hospitali ya Ocean Road nimekatwa mguu na naendelea na matibabu, natakiwa
kununua mguu wa bandia kwa shilingi milioni moja na laki mbili.
“Nawashukuru madaktari walionihudumia kwani wakati wowote
naweza kuruhusiwa, sina mahala pa kwenda lakini namshukuru Kanali Kipingu kwa
kuniruhusu nirudi kwenye bweni nikaendelee kukaa na wanafunzi wenzangu. Naomba
msaada kwa Watanzania wote.”
Aliyeguswa na habari ya James anaweza kumsaidia kupitia
namba zake ambazo ni 0716 101980 au 0753
358172.
No comments:
Post a Comment