Chuo kikuu cha Dodoma
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) umelipa madeni ya
zaidi ya Sh. milioni 63 ikiwa ni malipo ya kusimamia mitihani ya muhula
uliopita ya wahadhiri wa Shule ya Sanaa na Sayansi za Jamii waliogoma na
kukwamisha mitihani ya muhula huu iliyotakiwa kuanza mapema wiki hii.
Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Dk. Frowing Nyoni, alisema kuwa
awali, hawakuwa na fedha za kulipa deni hilo, lakini wamehakikisha wanapambana
mpaka fedha hizo zikapatikana.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanataaluma wa Chuo hicho (Udomasa),
Mhadhiri Msaidizi Paulo Loisulie, na Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule
hiyo, Masatu Kyabwene, walithibitisha pande hizo mbili kufikia suluhu na kwamba, mitihani iliendelea
kama kawaida.
Hata hivyo, hivi karibuni kulielezwa kuwapo kuvurugwa mitihani
mitatu, ambayo ilifanywa chini ya usimamizi wa wahadhiri, ambao siyo
waliotakiwa kufanya kazi hiyo kufuatia waliostahili kuwa katika mgomo ambambo
iliyotakiwa kufanywa na wanachuo wa mwaka wa tatu iligawiwa kwa wale wa mwaka
wa kwanza, huku mtihani mmoja wa lugha (Literature) uliotakiwa kufanywa kwa
kutumia vitabu wanachuo wakizuiliwa kutumia na hivyo kusababisha malalamiko.
Mhadhiri Msaidizi anayefundisha na aliyestahili kusimamia
somo hilo, Honoratha Thomas, akizungumzia tatizo hilo amesema wameafikiana mitihani yote mitatu
iliyofanywa bila usimamizi wa wahusika isitambuliwe.
Hata hivyo, Dk. Nyoni alikataa kuzungumzia suala hilo
akisema kwa kuwa bado wanalifanyia uchunguzi na kwamba ikibainika kulitokea
matatizo, kuna hatua zinazotakiwa kufuatwa ili kuweka mambo sawa na kutaja
hatua hizo kuwa ni pamoja na mitihani kurudiwa kutungwa upya au wanachuo
kufanya katika muhula ujao kama mitihani maalumu.
No comments:
Post a Comment