Watuhumiwa wawili wa
ujambazi wameuawa jijini Dar es Dalaam na wananchi katika jaribio la kufanya
tukio la uporaji katika eneo la benki ya NMB Wilaya ya Ilala.
Watuhumiwa hao wanadaiwa
kuwa walikuwa wakijaribu kumpora mteja aliyekuwa ndani ya benki hiyo akichukua
fedha kwa kutumia silaha mara baada ya kutoka ndani ya benki hiyo.
Kamishna wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao ambao idadi yao
haijafahamika walifika katika eneo la benki hiyo tawi la Uwanja wa Ndege wakiwa
na pikipiki tayari kufanya tukio hilo.
“Hawa walikamatwa
kufuatia taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna watu wenye pikipiki ambao wanahisi
wanataka kufanya uhalifu. Polisi waliweka mtego nje ya benki lakini
waliwashtukia polisi na kuanza kukimbia kila mmoja kwa njia yake,” alisema.
Alisema wakati wahalifu
hao wakikimbia, mmoja alifyatua risasi kwa lengo la kupambana na askari, lakini
askari hao walifyatua risasi juu kwa lengo la kumuamuru asimame.
“Walifanikiwa kumkamata
na alipopekuliwa alikutwa na bastola aina ya Browing yenye namba 230787
iliyotengenezwa nchini Chekoslovakia ikiwa na risasi tatu. Hata hivyo wananchi
waliokuwa wengi waliwazidi nguvu polisi wakamshambulia.
“Walimshambulia kwa mawe
lakini polisi walifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza hospitali lakini alifariki
akiwa njiani,” alisema Kova.
Alisema jambazi mwingine
ambaye alikimbilia katika eneo la Karakata, wananchi na askari walimkimbiza,
lakini hakusimama hata askari walipopiga risasi juu kumtaka asimame.
Alisema baada ya polisi
kuona mtuhumiwa huyo anakaidi agizo la kusimama, walimpiga riasasi miguuni na
alianguka na kuishiwa nguvu kabla ya kufariki akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Kova alisema baadaye
jioni jana, watuhumiwa wengine watatu walikamatwa. Aliwataja kuwa ni Salum
Seleman (28), Samwel Clips (32) na Said Salehe ambaye ni mganga wa kienyeji.
Alisema Seleman na Clips
walikamatwa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari baada ya kugundulika kuwa ni
watuhumiwa wa ujambazi katika tukio hilo, ambalo wenzao waliuawa.
“Hawa walifika kituoni
pale wakiwa wamebadili nguo na kujifanya ni wateja wa kawaida, lakini lengo lao
ni kuangalia hatma ya wenzao, lakini waligundulika kuwa nao walishiriki na
baada ya kuwakamata na kuwahoji wamekiri kuhusika na wao ndiyo walikimbia,”
alisema.
No comments:
Post a Comment