Pages

Monday, July 21, 2014

MJUE KIUNDANI KHAMIS MCHA ALIYEITUNGUA `BLACK MAMBAS` MABAO MAWILI

Khamis Mcha `Vialli` akiwa katika harakati za kufunga katika mechi ya jana dhidi ya Msumbiji
KUTOKANA na kambi iliyowekwa mjini Gaborone nchini Botswana kwa wiki mbili na baadaye mjini Tukuyu mkoani Mbeya, Watanzania wengi walikuwa na matumaini ya kuibuka na ushindi dhidi ya Msumbiji.
Matumaini haya hayakuwa kwa mashabiki tu, hata kwa  benchi la ufundi, viongozi wa soka na wachezaji wote.
Taifa stars jana ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Msumbiji katika mechi ya kuwania kupangwa hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataia ya Afrika, AFCON, mwakani nchini Morocco.
Mechi hii ilipigwa ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam. Wakati mashabiki wakisubiri kuona Stars iliyosheheni wachezaji wote wanaocheza ligi ya ndani na nje ya nchi inafunga mabao, dakika 45 za kipindi cha ziliisha kwa suluhu pacha.
Dakika ya 47 kama sinema vile, Kevin Yondani alimfanyia madhambi mchezaji wa Msumbiji na mwamuzi kutoa penati iliyofungwa na Elias Gasper Pelembe.


Pelembe alifunga bao lake la 10 katika mechi 49 alizoichezea Msumbiji tangu aitwe kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Ni mchezaji anayecheza ligi ya Afria kusini tangu mwaka 2007 alipojiunga na timu ya Supersport United akitokea klabu ya Despotive Maputo.
 Msimu wa 2007/2008 alitwaa ubingwa na klabu ya Supersport United na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu huo. Alikaa klabuni hapo kwa misimu mitatu na baadaye akasajiliwa na matajiri wa Mamelod Sundowns.
1 (1)
Samir Hajji Nuhu na Khamis Mcha ‘Vialli’ wakimpongeza Gaudence Mwaikimba (katikati) baada kufunga moja ya bao  katika mchezo wa ligi kuu msimu ulipoita ndani ya Uwanja wa Azam Complex 
Baada ya bao hilo, kwa dakika kadhaa, kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij akatafakari na kumuita kijana mmoja wa Kizanzibar na kumueleza jambo la kufanya. Kijana huyu ni Khamis Mcha `Vialli`.
Nooij alimpumzisha Mrisho Ngassa na kumuingiza Mcha aliyeisawazishia Taifa stars bao katika dakika ya 65.
Pia Mcha alifunga bao la pili na la kuongoza kwa mkwaju wa penati baada ya Mbwana Samatta kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Mtandao huu ukaona kufurahia kiwango cha Mcha pekee haitoshi, bali kuna haja ya kujua baadhi ya mambo kuhusu mchezaji huyu mwenye kipaji kikubwa cha soka.

HIVI UNAJUA KWANINI KHAMIS MCHA `VIALLI` ALIENDA KUPIGA PENATI?

Katika mahojiano maalumu na mtandao huu, Mcha alieleza kuwa yeye ni mpigaji mzuri wa penati na amekuwa akifanya vizuri tangu utotoni.
Mcha anasema katika mazoezi ya timu ya Taifa, anapiga sana penati na wenzake wote wanamuamini sana. Ilipotokea penati, hakuona shida kuuchukua mpira na kwenda kupiga.
Mcha anasema baada ya kushika mpira, nahodha wa Taifa Stars,  Nadir Haroub `Cannavaro` akamuonesha ishara ya kumuuliza unapiga?. Anasema alimjibu kwa ishara pia kuwa, ndiyo kamanda!.
Kijana huyu anaendelea kueleza kuwa Thomas Ulimwengu akamtazama na kumwambia, usiogope mwana! . Anasema hakuwa na wasiwasi hata kidogo kwasababu anajua namna ya kupiga na wenzake wanamuamini kwa umahiri wake. Kweli bila kufanya makosa akauzamisha mpira nyavuni.
IMG_3409
SASA SWALI LIKAJE, KWANI MCHA KAANZA KUPIGA PENATI LINI?
Mchezaji huyu mwenye kipaji anasema kuwa alianza kupiga penati zamani sana. Tangu aanze kucheza mpira wa mashindano, ameshapiga penati zaidi ya ishirini na ametia kambani zote na kukosa mbili tu.
Alikosa penati kwenye mechi baina ya Zanzibar Heroes na Kenya kwenye mashindano ya CECAFA nchini Uganda na akakosa penati ya pili kwenye mechi moja ya Azam fc.
Mcha ni mahiri kupiga penati, lakini kijana huyu ni muislam. Waumini wote wa dini ya kiislam wapo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

KWANI KHAMIS MCHA `VIALLI` YUPO KATIKA MFUNGO?,

 Mchezaji huyu anasema yupo katika mfungo na anasema siku moja kabla ya mechi ya jana mwalimu aliwataja wachezaji watakaoanza katika kikosi cha kwanza na wachezaji wa akiba. Anasema wakati Nooij anataja kikosi cha kwanza, hakusikia jina lake, lakini likasikika katika majina ya wachezaji wa akiba.
Anasema mchezaji anapokuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba,a naweza kucheza au asicheze katika mechi. Sasa yeye alishika mawili. Cha ajabu, Mcha anasema angeanza mechi ya Msumbiji asingefunga, na alifunga kwasababu alianzia benchi.

MCHA AMEIFUNGIA MABAO MANGAPI TAIFA STARS?

Nyota huyu anasema ni mara ya kwanza kuifungia Stars katika mechi ya mashindano. Lakini amefunga mabao manne mpaka sasa.
Bao moja alifunga katika mechi ya kirafiki baina ya Taifa stars na Namibia iliyomalizika kwa sare ya 1-1 mjini Windhoek. Mcha alifunga bao hilo baada ya kupiga mpira wa kona ulizama moja kwa moja nyavuni.
Bao lingine alifunga katika mechi ya kirafiki dhidi ya Botswana mjini Gaborone ambapo Stars ililala mabao 4-2. Hii ilikuwa mechi ya mwisho ya Stars kujipima ubavu kabla ya mechi ya jana.
Kwahiyo, mpaka sasa Mcha ameifungia Stars mabao manne baada ya kufunga mawili dhidi ya Msumbiji.
Kwa upande wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Mcha anasema mpaka sasa ameifungia mabao 9.
13

BAO LAKE LA KUSAWAZISHA DHIDI YA MSUMBIJI ANALIELEZEAJE?

Mcha anasema kuwa goli alilosawazisha jana linafanana sana na lile alilofunga dhidi ya Botswana. Anafafanua kuwa kule Botswana alirushwa mpira na Oscar Joshua ambapo John Bocco akauparaza kwa kichwa na ukamkuta sehemu nzuri aliyounganisha moja kwa moja mpaka nyavuni kwa mguu wa kushoto.
Katika mechi dhidi ya Msumbiji, Mcha anasema Erasto Nyoni alirusha mpira ambao John Bocco aliruka juu na beki wa Msumbiji lakini hakugusa mpira na yeye akaunganisha moja kwa moja kama alivyofanya Botswana.

MAJINA KAMILI YA MCHEZAJI HUYU NI YAPI?
Nyota huyu anasema yeye anaitwa Khamis Mcha Khamis.
KWANINI ANAITWA VIALLI?
Mcha anasema utotoni alikuwa anacheza timu ya Kwahani ya Zanzibar. Kuna mchezaji mmoja wa timu ya wakubwa alikuwa anaitwa Shomary na ndiye alimpa jina la Vialli.
Mchana anasema wakati akiwa mtoto alikuwa anapenda kunyoa kipara. Sasa Shomary kila akimuona uwanjani, alikuwa anasema vipi bwana wewe! Unapenda kunyoa kipara kama Gianluca Vialli.
Gianluca Vialli ni mchezaji wa zamani wa Italia aliyekuwa anaichezea klabu ya Juventus.
Kutokana na kitendo cha Shomary kumuita Mcha Vialli, kilisababisha jina hilo liwe maarufu na kutumiwa na wengi. Na hapo ndipo Khamis Mcha `Vialli` likaanza kutumika zaidi.
Lakini unaweza kujiuliza, kwanini Mcha hanyoi kipara tena? Mfungaji huyu wa mabao mawili ya Stars anasema baba yake mzazi, Khamis Mcha alimkataza kunyoa kipara.
Mzee Mcha alimwambia mwanae kuwa kunyoa kipara ni `staili` ya vijana wahuni, kwahiyo akamtaka mtoto wake kuachana na unyoaji wa aina hiyo.
Mcha anasema siku zote yeye ni msikivu, alimsikiliza baba yake na kuamua kuacha kunyoa kipara kwasababu baba hataki na hapendi.

KWANI BABA YAKE, MZEE MCHA KHAMIS ALIKUWA MCHEZAJI?
Mcha anasema baba yake ni mtu wa mpira. Enzi zake alicheza timu ya Kmkm na baadaye Miembeni, zote za visiwani Zanzibar.

JE, KHAMIS MCHA ALIANZIA SOKA WAPI?

Mzanzibar huyu anasema alianzia soka katika timu ya Kwahani, akajiunga na Mbuyuni, baadaye Tembo, (zote za Zanzibar).
Baada ya kutoka Tembo alijiunga na Miembeni ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Zanzibar Ocean View.


Alipotoka katika timu hiyo akajiunga na Azam fc ambapo amecheza misimu mitatu na msimu ujao unakuwa wa nne.

No comments:

Post a Comment