Ripoti ya daktari wa magonjwa ya akili iliyowasilishwa
katika kesi dhidi ya Mwanariadha mashuhuri Afrika kusini, Oscar Pistorius,
inaashiria kuwa anaugua msongo wa kimawazo na yumo katika hatari ya kujitoa
uhai.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa na wakili wake, inasema
anamuomboleza mpenzi wake Reeva Steenkamp.
Siku ya Jumatatu, mahakama ilielezwa kwamba Pistorius hana
matatizo ya akili wakati alipompiga Bi. Steenkamp risasi .
Anakana kutekeleza mauaji hayo, akieleza kuwa ilikuwa bahati
mbaya alipohofia kwamba aliingiliwa nyumbani mwake na mtu asiyemjua.
Awali meneja wa Pistorius alihojiwa.
Ufanisi wa Pistorius
Siku ya Jumanne, Peet van Zyl alisema Pistorius amekuwa mtu
anayejulikana kimataifa katika mashindano ya olimpiki kwa walemavu ya mwaka
2012, na alitarajiwa kufanikiwa zaidi.
Mwanariadha huyo aliyekatwa miguu yake miwili, alishindana
katika mashindano hayo ya walemavu na ya olimpiki huko London.
Van Zyl amesema huenda Pistorius angejiongezea kipato chake
mara tano au sita zaidi.
Aliongeza kwamba ni mfanyabiashara na ana nafasi nyingi
kutokana na kusifika kwake.
Meneja wa Pistorius anasema anaomboleza kifo cha mpenzi wake
Mwandishi wa BBC anasema Pistorius akiwa kizimbani Pretoria,
ni hakika kwamba aliyatafakari yaliokuwa yakisemwa na Van Zyl kuhusu uwezekano
wake kufanikiwa zaidi ambao kwa sasa umebadilika.
Mwendesha mashtaka Gerrie Nel amesema hakujuwa kwamba Van
Zyl angeitwa mahakamani kutoa ushahidi na ameomba mahakama isitishe vikao hadi
Jumatano ili ajitayarishe kumhoji, ombi ambalo jaji aliliridhia.
Bwana van Zyl ni miongoni mwa mashahidi wa upande wa utetezi
kuwasilishwa.
Mwandishi wetu anafahamu kwamba huenda upande wa mashtaka
baadaye ukamuita daktari huyo, aliyemchunguza Pistorius katika mwezi uliopita,
aje atoe ushahidi
Madaktari watatu wa mgonjwa ya akili waliiwasilisha ripoti
moja iliyosema mwanariadha huyo yupo sawa kiakili kushtakiwa.
Pistorius, mwenye umri wa miaka 27, anasema alifyetua risasi
kadhaa akiwa katika hali ya kuogopa kukilenga choo alipokuwepo Bi Steenkamp.
Anashtakiwa kwa kutekeleza mauaji ya kupangwa, na upande wa
mashtaka unasema wapenzi hao waligombana kabla ya Pistorius kumpiga risasi na
kumuua Bi Steenkamp.
No comments:
Post a Comment