Mtoto Mariam Shabani akiwa katika mateso baada ya kupatwa na
gonjwa la ajabu.
MTOTO Mariam Shabani
(5) aishiye Bunju A Zone Kizota nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambaye alizaliwa akiwa mzima, amekumbwa na
ugonjwa wa ajabu unaowashangaza wazazi wake.Mzazi wa mtoto huyo, Idd Shaban
aliwaambia waandishi wetu kuwa
mwanaye akiwa mchanga alisadikika kuwa na
matatizo ya ubongo lakini ukuaji wake ulikuwa mzuri kama wanavyokuwa watoto
wengine.
HALI ILIPOANZA KUBADILIKA
Akifafanua zaidi Shaban alisema: “Alipofika umri wa miaka
miwili hali ilibadilika akawa mtu wa kulala tu na mpaka sasa hawezi kufanya
chochote.
“Baada ya kupata hayo matatizo tuliamua kumpeleka Hospitali
ya CCBRT iliyopo Msasani Dar kwa ajili ya matibabu zaidi lakini ilishindikana
na madaktari walisema tuwe tunampeleka katika tawi la Hospitali ya CCBRT
lililopo Tegeta kwa ajili ya mazoezi kwa ahadi kuwa hali yake itakuwa sawa.
ASHINDWA KUTEMBEA, KUONGEA
“Tuliendelea na mazoezi katika Hospitali ya Tegeta lakini hali ilizidi kuwa mbaya
kabisa kwani Mariam akawa ajiwezi kwa chochote si kutembea wala kuongea, akawa
ni mtu wa kulala muda wote, mbaya zaidi mpaka sasa hawajui kama anasikia au la
sababu hata tukimsemesha haonyeshi ushirikiano.
“Kwa kweli mwanangu anapata wakati mgumu sana kwani hata
akiumwa hatuwezi kujua mpaka alie au awe na joto kali, kuna siku alianguka
kutoka kitandani na kuvunjika mguu kiukweli tulipata tabu kumtibu kutokana na
hali ya maisha kuwa ngumu, tulijitahidi akapona mguu kwa pesa za kududunduliza.
Akiwa amelala.
ALIKUWA ANAONGEA NA
KUCHEKA
“Naumia sana kuona
mwanangu yupo katika hali mbaya wakati alizaliwa akiwa mzima asiye na kasoro,
alikuwa anaongea, anacheka pia aliwahi kutambaa na kutembea katika ukuaji wake
utotoni.
“Nakiri kuwa tuliambiwa ana mtindio wa ubongo, huenda hiyo
hali ilichelewa kujitokeza mpaka baada ya miaka miwili ndipo hali hii
ikajitokeza.
NATAMANI AWE AKIENDA SHULE
“Sijui hatima ya mwanangu, natamani kuona binti yangu
anakwenda shule kama watoto wengine hata kama siyo shule za kawaida basi za
watoto wenye mtindio wa ubongo japo uwezo kifedha sina.
“Mimi ni mjenzi na nina kipato kidogo sana, nawaomba
wasamaria wema, Watanzania wenzangu wanisaidie fedha za matibabu na kibaiskeli
cha kumbebea kwa sababu tumemtengenezea kiti cha mbao ambacho kinamuumiza,”
alisema Shaban.
Yeyote aliyeguswa na
habari ya kusikitisha ya mtoto Mariam awasiliane na mzazi wake kwa simu namba
0718 848 895.
No comments:
Post a Comment