Rasimu ya Katiba Mpya
Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Alli
Omari Juma amefuta matumaini ya Watanzania kuhusu kupatikana kwa Katiba mpya,
badala yake akabainisha kuwa wajumbe wako Dodoma kwa ajili ya kula posho tu.
“Nawakumbusha watu kufuta matumaini ya kupata Katiba Mpya,
kinachojadiliwa hapa ni mambo ya
kulazimishana kila upande, sisi wengine
tunaona bora ya Ukawa waliotoka nje kuliko mambo ya humu ndani,” alisema Juma
na kuongeza:
“..Hata wale Wapemba waliokwenda Umoja wa Mataifa kudai haki
ya kujitenga , naona walikuwa halali kwani hapa bungeni hakuna mwakilishi hata
mmoja kutoka huko wakati tunaambiwa kuwa itakuwa Katiba ya wote, ni
kudanganyana.”
Mjumbe huyo alisema kuwa Rasimu ya Warioba imetupwa na
wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi kiasi cha kuwafanya wengine waone kuwa
kinachotengenezwa ni marekebisho ya Katiba ya 1977.
Alisema kuwa suala la akidi pia litakuwa ni moja ya vikwazo
vitakavyosababisha kutopatikana kwa Katiba, akitolea mfano kutoka kwenye kamati
yake Namba 4.
Alisema ndani ya kamati hiyo mambo mengi yanachakachuliwa
kwani wajumbe wanaotakiwa kutoka Zanzibar ni 14 lakini waliopo ni 12 tu, ambao
baadhi hawakubaliani na mawazo ya CCM lakini wanaambiwa mambo ni mazuri.
“Ukawa walitoka kwa uhalali kabisa nami nawaunga mkono, sisi
tuliobaki humu ndani tulikuja kwa makusudi ya kuangalia kinachoendelea na sasa
tunaona mambo ni ovyo,” alisema.
Kwa upande mwingine alimlaumu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu
Samuel Sitta kwamba amekuwa ni kinara wa kuvuruga kanuni kila wakati na kutaka
mambo yake mwenyewe.
Jumba ambaye ni mtaalamu wa sheria, aliwatupia lawama pia
viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba nao wanapaswa kulaumiwa kwa
kushindwa kuwaweka Wazanzibar pamoja ili wajue wanataka nini.
Kwa mujibu wa Juma, kila maeneo wanayojadili wanafanya kazi
hiyo kwa kuboresha maslahi ya CCM kwani wanawasaidia kuwaandikia Ilani yao.
Alimtaka rais Jakaya Kikwete kukubaliana na maoni ya watu
mbalimbali kwamba bunge la Katiba lisitishwe mara moja kuliko kuendelea
kujadili misimamo mikali ya CCM.
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment