Jengo la makao makuu ya Idara ya ushushushu ya
Uingereza,jijini London
|
Kuna ukweli mmoja usiofichika wala kupingika kwamba watu
wengi sana wanapenda kazi ya ushushushu, yaani Uafisa Usalama wa Taifa. Hiyo
sio kwa Tanzania pekee bali sehemu nyingi duniani. Ukiingia mtandaoni utakutana
na watu wengi wanaozungumzia taaluma ya intelijensia au/na wahusika katika hali
ya kutamani kuifahamu taaluma hiyo nyeti au kuwa mhusika.
Leo nitaanza mlolongo (series) wa makala kuhusu
taaluma hiyo
adimu. Hata hivyo ni vema nikatahadharisha mapema kwamba nitakachoandika ni
kile tu kinachoruhusiwa kuandikwa hadharani.Kimsingi,taaluma ya ushushushu
inatawaliwa na usiri,na mengi ya yanayohusiana na taaluma hayo yanabaki kuwa
siri. Hata hivyo,kuna maelezo ambayo yapo wazi japo inahitaji uelewa wa aina
flani kuchora mstari kati ya kipi ni siri na kipi ni ruksa kuwa hadharani.
Kwa tafsiri rahisi, ushushushu ni taaluma inayohusu
ukusanyaji wa taarifa za kiusalama kwa njia za siri (clandestine methods). Japo
kwa kiswahili ushushushu ni intelijensia, kiundani kuna tofauti kati ya
ushushushu unaofanyika ndani ya nchi na unaofanyika nje ya nchi.
Kwa hapa Uingereza, Idara ya ushushushu inayoshughulika na
masuala ya ndani inajulikana kama MI5 na inayohusiska na ushushus nje ya nchi
ni MI6.Kwa huko nyumbani, tofauti hizo zipo ndani ya muundo wa taasisi husika,
kwa maana kwamba kuna taasisi moja tu lakini ndani yake kuna mgawanyo wa
kimajukumu ya ndani na ya nje.
Kadhalika, japo mashushushu wamekuwa wakifahamika pia kama
spies, ukweli ni kwamba spy ni shushushu anayefanya kazi nje ya nchi yake, kitu
kinachojulikana kiusalama kama ujasusi au espionage kwa Kiingireza.Japo mataifa
mbalimbali yana miundo tofauti ya Idara zao za Usalama wa Taifa,lengo na kazi
kuu ni ukusanyaji wa taarifa hizo.Kwa minajili ya makala hizi, nitazungumzia
zaidi mazingira ya huko nyumbani Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa
Taifa ya mwaka 1996, Idara yetu ya Usalama wa Taifa ni idara ya serikali iliyo
chini ya Ofisi ya Rais,ambayo ina jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa za
usalama na kuziwasilisha 'mahala kunakohusika' katika namna ambayo Mkurugenzi
Mkuu wa Idara hiyo ataona inafaa.
Kimsingi, mkuu'halisi' wa Idara hiyo ni Rais mwenyewe,ambaye
kwa lugha ya kiusalama anafahamika kama 'sponsor.' Wakuu wa Idara za usalama
popote pale duniani hufahamika kama spymaster.
Maeneo makuu ya kazi za Idara ya Usalama wa Taifa ni
kukusanya na kuchambua habari za kiusalama zinazohusiana na ujasusi
(espionage),uzandiki (subversion),uhujumu (sabotage) na ugaidi (terrorism).
Lakini jukumu la Idara hiyo si kukusanya taarifa hizo na kuzichambua tu bali
pia kuzuwia matukio hayo yanayofahamika kama matishio ya usalama wa taifa.
Ni kwa vile utendaji wa kazi wa Idara yoyote ile ya Usalama
wa Taifa unaegemea katika usiri mkubwa ndio maana kwa 'mtaani' kuna hisia
tofauti kuhusu umuhimu wa taasisi hiyo. Ukweli ni kwamba laiti umma ungefahamu
nini kinafanywa (au kinapaswa kufanywa) na Idara hiyo basi kwa hakika
ingethaminiwa zaidi ya kuogopwa tu.
Ni muhimu hapa nisisitize kuwa ninazungumzia 'hali mwafaka'
yaani kwa Kiingereza ideal situation. Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko
mengi miongoni mwa wananchi wakiishutumu Idara yetu ya Usalama wa Taifa kuwa
imeleemea mno kwenye siasa hasa kuibeba CCM, imezembea mno kiasi cha kuruhusu
ufisadi kushamiri, na imekuwa ikilaumiwa pia kutokana na matukio mbalimbali
yanayotishia usalama wa Taifa kama vile ugaidi.
Wanaotoa lawama hizo wapo sahihi kwa kiasi flani, kwani
kushamiri kwa maovu katika jamii sambamba na mwendelezo wa matukio yanayotishia
usalama wa taifa ni viashiria kuwa Idara ya Usalama ya nchi husika ina
mapungufu kiutendaji.
Hata hivyo,ni muhimu kutambua kanuni moja muhimu ya ufanisi
au kushindwa kimajukumu kwa Idara ya Usalama wa Taifa popote pale.Ni kwamba
wakati Idara husika inapaswa kuwa macho katika kila sekunde kuzuwia matendo ya
kidhalimu, wanaopanga kufanya matendo hayo wanahitaji mara moja tu kufanikisha
azma yao.
Mfano halisi ni kwenye matukio ya ugaidi. Wakati gaidi
anahitaji fursa moja tu kufanikisha tukio la kigaidi, Idara ya Usalama
inahitaji kila fursa- kila sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi,
mwaka-kuhakikisha gaidi hafanikiwi.
Kadhalika, wakati inaweza kuwa rahisi kuilaumu Idara ya
Usalama wa Taifa inaposhindwa kuzuwia tukio flani, kwa mfano shambulio la
kigaidi nchini Kenya, kiuhalisi suala zima la ukusanyaji wa taarifa za
kiusalama ni gumu mno.
Hebu pata picha: unaletewa tetesi kuwa kuna mtu anataka
kulipua bomu kanisa au msikiti. Mara nyingi tetesi hizo huwa hazibainishi
jinsia ya mtu huyo,wajihi wake, ni mwenyeji au mgeni na vitu vingine muhimu vya
kuweza kumtambua japo kwa ugumu.
Kutokana na ugumu wa zoezi la kukusanya taarifa za
kiusalama,ndio maana wahusika-mashushushu/maafisa wa Idara ya Usalama wa
Taifa-wanapaswa kuwa watu wenye akili isiyo ya kawaida, au angalau wenye uwezo
mkubwa wa kutumia akili.Neno lenyewe intelijensia linahusiana na matumizi ya
akili.Lakini si akili tu, bali pia maafisa usalama wa taifa hupaswa kujifunza
na kuendeleza hisia ya sita (6th sense).
Mwanadamu wa kawaida ana hisia 5: HARUFU kwa kutumia pua;
LADHA kwa kutumiamdomo/ulimi, KUGUSWA (touch) kwa kutumia ngozi, KUONA kwa
kutumia macho, KUSIKIA kwa kutumia masikio. Lakini kwa mashushushu wanapaswa
kuwa na hisia ya ziada ya kutambua kitu zaidi ya kutumia hisia hizo 5 kuu. Si
kazi rahisi hata kidogo.
Basi kwa leo niishie hapa.Nitaendelea na mfululizo wa makala
hizi angalau kila wiki.
Source: chahali blog
No comments:
Post a Comment