Uzinduzi wa makala mapya ya kipindi maarufu cha Big Brother
nchini Afrika Kusini umeahirishwa baada ya moto mkubwa kuteketeza studio za
kipindi hicho mjini Johannesburg.
Kipindi hicho kilistahili kuanza Jumapili hii lakini
waandaaji wa wa kipindi chenyewe wameamua kuahirisha uzinduzi huku wakitafuta
sehemu nyingine ya kupeperushia kipindi hicho.
Hakuna aliyejeruhiwa kwenye mkasa huo wa moto na
kilichousababisha bado hakijajulikana kwani uchunguzi untarajiwa kufanywa.
Washiriki katika kipindi hicho kutoka nchi 14 Afrika
watakuwa wanashiriki katika makala ya 9 ya kipindi hicho.
Kipindi chenyewe kinatarajiwa kupeperushwa kwa siku 99 kabla
ya mshindi kutangazwa.
Mshindi wa mwaka huu anatarajiwa kupokea kitita cha dola
300,000 kima sawa na kile kilichotolewa kwa mshindi mwaka 2013.
Waandalizi wa kipindi hicho Endemol na M-Net walisema kuwa
juhudi za kupata sehemu mbadala ya kuendeshea kipindi hicho itakuwa kazi ngumu
kutokana na ukosefu wa teknolojia inayohitajika kuendeshea kipindi hicho kwani
haipatikani kwa urahisi.
''Kila juhudi italenga kupata ufumbuzi haraka iwezekanavyo
kuhakikisha kuwa kipindi hicho ambacho hutazamwa na watu wengi zaidi Afrika
kitaendelea.''waliongeza kusema waandalizi.
Waandalizi pia walisema kuwa washiriki kutoka Ghana walipata
tatizo la viza na hivyo wakaamua kuchua raia wa Ghana wanaoishi nchini Afrika
Kusini kwenyewe.
Pia washiriki wapya walitarajiwa kutoka Rwanda na Sierra
Leone kwa mara ya kwanza lakini kutokana na changamoto za hapa na pale
hawataweza kushiriki.
Kipindi cha Big Brother ni kipindi maarufu sana Afrika
kutokana na kupendwa sana kwake, na kilianza kupeperushwa mwaka 2003. Washiriki
kutoka Tanzania, Angola, Nigeria, Namibia, Zimbabwe na Afrika Kusini wamewahi
kushinda katika makala ya awali.
Mnamo mwaka 2010, kipindi hicho kiligonga vyombo vya habari
baada ya mshiriki mmoja kutimuliwa kutoka katika nyumba hiyo baada ya kumpiga
makonde mshindani mwanamke.
No comments:
Post a Comment