Pages

Thursday, September 11, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MATOKEO YA HARAMBEE YA TAASISI YA MKAPA ILIYOFANYIKA MWANZA 23 AGOSTI 2014

Kwa niaba ya Msarifu wa Taasisi Mhe. Benjamin William Mkapa, Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na wafanyakazi wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa tunatoa shukrani za dhati kwa kuweza kufanikisha harambee ya kuchangia. Mradi wa Mkapa Fellows, iliyofanyika jijini Mwanza siku ya Jumamosi, tarehe 23 Agosti 2014 katika ukumbi wa Hotel ya JB Belmont.



Harambee iliyohudhuriwa na wageni karibia 230 iliongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania,Mhe Mizengo Pinda ambae alikuwa mgeni rasmi akiambatana na Raisi mstaafu,Mhe. Benjamin W. Mkapa pamoja na Mama Anna Mkapa. Harambee hii iliyofanyika na Taasisi ya Benjamin W. Mkapa ni ya mara ya kwanza kutekelezwa na Taasisi nje ya Mkoa wa Dar Es Salaam. Kwa hatua za awali tuliamua kuanzia katika Kanda ya Ziwa,na kuwashirikisha washikadau waliopo katika mikoa sita (6) ya Kanda ya Ziwa. Harambee ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Tshs 1.38billioni na hivyo kuvuka lengo lililowekwa la kukusanya kiasi cha Tsh 500 millioni katika Kanda hiyo.
Kiasi kilichokusanywa kitatumika kutekeleza mradi wa Mkapa Fellows unaoendeshwa na Taasisi ya Benjamin W. Mkapa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Mradi huu wa Mkapa Fellows unatekelezwa katika mizunguko miwili; ambapo mzunguko wa kwanza ulianza Januari 2013 na utamalizika Desemba 2014 na ulifikia Halmashauri sita (6) nchini za Sumbawanga vijijini, Kalambo, Nkasi, Msalala, Kishapu na Biharamulo. Baadhi ya mafanikio ya mradi huu hadi leo, ni pamoja na tumeshaajiri na kuwapeleka katika wilaya hizo 6 wataalam wa afya 30 kati ya lengo la miaka mitano la watalaam 180, na pia ujenzi wa vyumba vya upasuaji 9 kati ya 30 umeshakamilika, na ununuzi na uwekaji wa vifaa vya kutolea huduma pia kukamilika. Fedha za utekelezaji wa mzunguko huu wa kwanza zilifanikiwa kupatikana kupitia mfadhili wa Serikali ya Ireland na wafanyabiashara zaidi ya 50, wakiwemo pia Kampuni ya African Barrick Gold.
Mzunguko wa pili wa huu mradi utaanza Januari 2015 mpaka Desemba 2017 na utafikia Halmashauri 9 za Shinyanga vijijini, Kahama,Meatu, Bariadi, Itilima, Busega, Maswa,,Chake Pemba na Mkoa wa Kati Unguja.
Kwa muhtasari fedha hizi zilizokusanywa katika Harambee hii ya Kanda ya Ziwa,zitasaidia kuchangia katika bajeti inayohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi kuanziaJanuari 2015. Hali kadhalika mradi wa Fellows ambao una bajeti ya Tshs. 15bilioni kwa miaka 15, ilikuwa bado na pengo la Tshs. 10billion, hivyo kwa kupata mchango wa kutoka Kanda ya Ziwa wa Tshs. 1.3billioni,sasa litapunguza hilo pengo hadi Tshs. 8.7 bilioni. Wakati huo huoTaasisi itaendelea na mikakati mingine mbalimbali ya kutafuta fedha za kutekeleza mradi huu hadi mwaka 2017.
Kwa nafasi ya pekee, Taasisi ya Benjamin W. Mkapa HIV/AIDS (BMAF) inapenda kutoa shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda kwa kukubali mwaliko wa kuwa mgenirasmi katika harambee hiyo. Pia shukrani zinatolewa kwa mawaziri na manaibu mawaziri na viongozi mbalimbali ambao walituunga mkono katika Harambee hii.
Taasisi inatoa shukrani zake kwa Wakuu wa mikoa wa Kanda ya Ziwa kwa kukubali kwao kuongoza mikoa na Halmashauri zilizopo chini yao, katika maandalizi na kushiriki kikamilifu katika harambee hii. Aidha Taasisi ya BMAF inatoa shukrani za dhati kwa wafanyabiashara wote wa Kanda ya Ziwa kwa kuweza kuchangia katika mradi huu. Mafanikio haya ni mfano mzuri wa Public-Private Partnership (ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma/serikali), ambapo inaweza kuleta mabadiliko katika kuimarisha huduma za afya nchini. Moyo na uaminifu waliotuonyesha ni mkubwa na tuna Imani tutaendelea kushirikiana katika kuleta maendeleo ya sekta ya afya, hususan katika maeneo ya vijijini.
Shukrani za pekee ziwaendee wadhamini wetu waliofadhili hafla ya chakula cha jioni cha harambee, ambao ni Anglo-Gold Ashanti, NSSF, Bank M, PPF,NHIF, Nyanza Bottling Co, Montage Limited, JB Belmont, Afya Radio,Mwananchi Communication, Jembe ni Jembe, Isamilo Hotel, Clouds FM naSahara Media Group.

Imetolewa na:
Dkt Ellen Mkondya-Senkoro
Afisa Mtendaji Mkuu
Taasisi ya Benjamin William Mkapa
S. L. P 76274, Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment