Kikwete na Ukawa
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAZUNGUMZO ya kusaka
mwafaka kati ya Rais, Jakaya Kikwete na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) yamemalizika huku kila upande ukitoa masharti ya kumaliza mgogoro
uliopo kuhusu kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Mkutano huo uliofanyika Ikulu ndogo mjini
Dodoma jana,
uliratibiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), huku ukiwa umehusisha
viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho kililiambia
MTANZANIA kuwa, katika kikao hicho viongozi wa Ukawa walikwenda na pendekezo la
kumtaka Rais Jakaya Kikwete asitishe mkutano wa Bunge la Katiba ili kuruhusu
mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo
walitoa mapendekezo hayo kwa Rais Kikwete
ikiwemo kuitaka Serikali kupeleka marekebisho madogo yafanyike katika
Katiba ya sasa kuruhusu mgombea binafsi na uundwaji wa Tume huru ya Uchaguzi.
Mbali na hilo pia wamemuomba Rais Kikwete katika marekebisho
hayo ya Katiba ya mwaka 1977 kuwepo kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court) na
matokeo ya urais yaruhusiwe kupingwa mahakamani.
Hata hivyo taarifa hizo zilidai kuwa, mjadala huo mkali
ulihitimishwa na Rais Kikwete kuwataka wajumbe hao wa TCD kuhakikisha wanakaa
pamoja na kuangalia namna bora ya kuliahirisha Bunge hilo kwani sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 haielezi namna ya Bunge hilo kuahirishwa.
Chanzo hicho kilisema kutokana mapendekezo hayo ya kila
upande wajumbe wanaounda TCD walitakiwa kwenda kujadiliana kwa kina namna bora
ya kuliendea jambo hilo kama ilivyopendekezwa na Rais Kikwete.
Katika kikao hicho TCD walilazimika kuunda kamati ndogo
itakayoongozwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia huku wajumbe wake
wakiwa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana,
Mwenyekiti wa Chama cha Wanannchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa.
Kamati hiyo itafanya kazi ya kuchambua mapendekezo
mbalimbali ambapo itakutana tena Septemba 6-7 mwaka huu kabla ya Septemba 8
kukutana na Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa hizo kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza baada ya
kikao hicho cha pamoja Rais Kikwete, atawasiliana na mamlaka husika kuangalia
namna bora ya kusitisha vikao vya Bunge hilo ili kuruhusu mazingira ya
kufanyika kwa Bunge la Jamhuri.
Hatua hiyo italifanya Bunge la Jamhuri kufanya marebisho
hayo kwa ajili ya muundo wa Tume ya Uchaguzi na namna bora ya kufanyika kwa
uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na baadaye
uchaguzi mkuu mwakani.
Awali akitoa taarifa za kikao hicho na Rais Kikwete,
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema kwamba baada ya mjadala mzito
walikubaliana kukutana tena na Rais Kikwete Septemba 8 mwaka huu.
“Ndugu waandishi wa habari, leo (jana) wenyeviti na makatibu
wa vyama vya siasa vinavyounda TCD tulikutana na rais kujadili ajenda mbili.
Ajenda ya kwanza ilihusu mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba na ajenda ya pili
ilihusu mambo ya kuimarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Rais amekubali kuangalia mambo tuliyomweleza na akatuomba
na sisi wajumbe wa TCD tukayatafakari huku na yeye akiendelea kuyatafakari ili
tukutane Septemba 8 mwaka huu.
“Kwa kuwa jambo hili ni muhimu, tumeunda kamati ndogo
itakayoangalia mambo yaliyozungumzwa na kuyatolea ufafanuzi kisha kamati hiyo
itawasilisha ripoti yake Septemba 8 tutakapokutana,” alisema Cheyo.
Kabla ya Rais Kikwete kukutana na wajumbe wa TCD, wajumbe
hao walianza kukutana wenyewe katika Hoteli ya Dodoma na kujadiliana mambo ya
kuzungumza pindi watakapokutana na Rais Kikwete.
Baada ya kutoka hapo, walielekea Ikulu ndogo iliyoko
Kilimani mjini hapa. Hata hivyo, kabla Rais Kikwete hajakutana na TCD,
inasemekana alikuwa na mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na
Uratibu, Steven Wasira pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Taarifa za ndani zilinaeleza kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM
Tanzania Bara, Phillip Mangula, nusura achafue hali ya hewa baada ya kuwataka
Ukawa warudi bungeni wakati mazungumzo hayo yakiendelea.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kauli hiyo ilionekana kuwakera
baadhi ya wajumbe wa Ukawa wakiwamo
Profesa Lipumba na Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya ambao walilazimika
kumpinga wazi wazi.
Wakati wa mijadala ya vikao hivyo, CCM waliwakilishwa na
Kinana na Mangula. Chadema waliwakilishwa na Dk. Slaa pamoja na Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu. Kwa upande wa NCCR-Mageuzi, alikuwapo Mbatia na
Katibu mkuu wake, Mosena Nyambabe wakati CUF waliwakilishwa na Profesa Lipumba
pamoja na Sakaya.
Chama cha UDP kiliwakilishwa na mwenyekiti wake, John Cheyo
akiwa na mdogo wake Isack Cheyo. TLP alikuwapo Mwenyekiti wa chama hicho,
Augustine Mrema na Fahmi Dovutwa aliviwakilisha vyama visivyokuwa na wabunge
bungeni.
Mtanzania
No comments:
Post a Comment