JACLINE MASANJA A.K.A JACK WA NJIAPANDA ENZI ZA UHAI WAKE.
Ilikua ni miaka kumi iliyopita (10) mwaka 2004, nikiwa ndio
kwanza nimeanza kufanya kazi chini ya kaka yangu Dr Sebastian Ndege na chini ya
uangalizi wa karibu sana wa boss Ruge Mutahaba na Boss Joseph Kussaga
nilipokutana na wewe mdogo wangu Jackline Masanja kupitia Njiapanda ulipokuwa
unatafuta msaada ukiwa mgonjwa sana.
Ulikua shujaa sana kukubali kusema kuwa uko tayari Dr Ndege
atangaze hali yako mbele ya uma wa WaTanzania na kwa ruhusa yako tukafanya
kipindi na wewe huku ukiwa mgonjwa na ukasema kuwa umeathirika na kwa kipindi
kile kinga yako ilikua chini sana (CD4 zilikua 4).
Wewe ulikua ni watu wa mwanzo kabisa kuja mbele ya umma
kuongea kuhusu hali halisi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na maradhi ya
UKIMWI. Tulikuita shujaa na Muhimbili ulipokua unatibiwa kipindi kile wahudumu
wote walikuita Jackie wa Njiapanda (ndio chanzo cha kumuita jina hilo miaka
yote hii). Kutokana na juhudi nyingi zilizofanyika ulipona kabisa na ukarudi
kwenye hali yako ya kawaida ya kawaida na ukaendelea na maisha yako.
Kutokana na yote yaliyotokea mimi na Dr Ndege tukaona ni
vyema kama tutakuomba ukae na sisi kama Njiapanda na uendelee kutusaidia kwa
kuwa Njiapanda ilikua imekua sana na waliokua wanahitaji msaada walikuwa
wanaongezeka kila kukicha. Hukusita kukubali na kuanzia miaka hiyo ukawa
unatusaidia kushughulika na wote wanaohitaji msaada wa Njiapanda. Ni wengi uliwachukua
na kukaa nao kwako ingawa hali yako ya kiuchumi haikua nzuri sana kusema eti
wewe ni tajiri.
Miaka ilienda na ukaendelea kupambana na maisha huku
ukiendelea vyema. Nakumbuka vizuri sana sakata la dawa ya Babu wa Loliondo
lilipoanza mimi na wewe tulikua hasi na chanya. Mimi nilikua napinga sana kwa
kuwa nilikua na sababu za kisayansi na wewe siku zote ulikua unakasirika kwa
kuwa ulikua ukiamini kuwa dawa inaponya. Ukaniomba nikuruhusu uende na kweli
tukakubaliana tukafanya mchakato na ukaenda. Tukakubaliana kuwa mimi
nachohitaji ni kimoja tu nacho ni kukutumia wewe kama somo kwa hiyo tukarekodi
kila kitu kabla hujaenda kwa babu na tukafanya kipindi maalum.
Ukasema kinga yako ni ngapi na kila kitu wala hukuogopa.
Ukaenda Loliondo ukanyweshwa kikombe na ukarudi. Tukafanya kipindi ukasema
unaendelea vizuri. Tukaendelea na vipimo na maisha yakaenda. Miezi miwili
baadae nakumbuka nilikua nimekaa kliniki nikakuona kwa chini unatembea huku
unajikongoja, nikakufuata pamoja na manesi wa pale clinic tukakuchukua
tukaendelea na uchunguzi tukagundua kuwa kinga yako imeshuka sana kwa kuwa
baada ya kwenda kwa babu hukuendelea na dawa (kinga ilikua 14).
Tukaanza kufanya jitihada za kuhakikisha afya yako inarudi
kuwa nzuri na kweli ukawa Ok na tukafanya kipindi tena kuhusu kilichotokea.
Kama kawaida ukawa shujaa na kusema kila kitu. Kupitia kwako waTanzania
wakajifunza mengi kuhusu kikombe cha babu na maambukizi ya virusi vya UKIMWI
kwa ujumla. Kupitia wewe Jackline Masanja watu wakafanya maamuzi huku wanajua,
ambayo kisayansi ni jambo la maana sana. Jackie mdogo wangu, mimi na Dr
Sebastian Ndege kamwe tusingeweza kuifikisha Njiapanda ilipofika bila ya
ushujaa wako, bila ya utayari wako wala bila ya uwazi wako.
Sio tu kwa kupitia story yako watu wamejifunza mengi kuhusu
maambukizi ya virusi vya UKIMWI bali pia mchango wako wa kusaidia Njiapanda na
watu wa njiapanda tumeweza kufanya mengi sana. Nakumbuka habari ya wamasai
uliileta wewe, habari ya yule msichana aliyelazimishwa kufanya mapenzi na mbwa
ilitoka kwako, watoto wa mitaani wanaolazimishwa kufanya mapenzi kinyume cha
maumbile pale kariakoo uliifuatilia wewe mpaka ukalala kariakoo usiku kucha
kuifuatilia. Ni nyingi sana Jackie.
Jackie, kwangu mimi na kwa Dr Sebastian Ndege wewe ni mdogo
wetu yule yule wa miaka 10 iliyopita. Ulikua unatuita kaka na sisi tukauita
mdogo wetu. Nakumbuka hata mambo yalipokua magumu nikgombana na ma boss wangu
kina Ruge nilikua nakuomba ukaniombee msamaha maana boss Ruge alikua anakupenda
sana kama mdogo wake, nilijua kuwa ukisema tu boss atanisamehe
hahahaaaaa…asante sana mdogo wangu kwa kuokoa jahazi mara kwa mara lol.
Leo hii nimeamua kuandika huu waraka mrefu kwako wewe Jackie
kwa kupitia ndugu zangu wa Facebook na platforms nyingine kwa sababu, siku ya
jumamosi 22 November 2014 nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu na mfanyakazi
mwenzangu Geah Habibu kukuhusu wewe mdogo wangu, kwamba mwili wako umekutwa
ukiwa umekwishafariki.
Sio tu kuwa kifo chako kilikua cha kawaida bali inaonekana
umeuawa. Kwa bahati mbaya sana kwa sasa siko nchini kwa hiyo sikuamini na
sikuweza kufanya chochote mpaka pale nilipoona picha yako. Kusema ukweli bado
sikuamini so nikaongea na Douglas na Amani (watengenezaji wa Njiapanda)
wafuatilie hii habari. Mwisho wa siku ni kweli ikaonekana kuwa umeuawa tena
kikatili.
Nikawasiliana na kaka yangu Dr Sebastian Ndege naye
hakuamini. Jumapili ilipofika nikasema nisiseme chochote maana naona bado si
kweli (nisamehe mdogo wangu) nikajikaza nikafanya Njiapanda bila kusema
chochote. Jana jumatatu ndio Geah akanihakikishia kuwa ni kweli umefariki na
baba yako amekutambua na msiba kweli uko.
Nimelia sana, sijui kwa nini umefanyiwa ukatili huu, siwezi
kusema chochote kwa kuwa sijui, lakini kitu kimoja nachoamini na kinachoniuma
moyoni mwangu ni kuwa mimi, wewe na Seba tumepambana sana Zaidi ya miaka kumi
kuhakikisha unakua ok na afya njema, najiuliza swali yote hiyo ilikua kwa nini?
JE NI KWELI KUWA JUHUDI ZOTE HIZO ZILIKUA KUKUTAYARISHA UJE UUWAWE KINYAMA
NAMNA HII??
Mwenyezi Mungu pekee ndie anayejua kilichotokea na ndiye
anayejua hukumu ya kila mmoja wetu. Jackie mdogo wangu umeenda, umeacha wadogo
zako na familia yako. Mungu akulaze mahali pema peponi mdogo wangu, naamini
sasa utapumzika maana umehangaika sana na haya maisha.
Familia yako naamini Mungu atabariki itakaa salama na yote
yatakua heri. Dr Ally Kaduma na clinic nzima ya IDC wanakulilia, Clinic ya
watoto na ya watu wazima ya DarDar wanakulilia watamiss unga wako ule wa uji wa
watoto uliokua unaleta.
Clouds Media yooote inakulilia, boss Ruge anakulilia,
familia yote ya Njiapanda inakulilia, kina mama Derick na kina brother Gelvas
na kaka yako mkubwa kabisa Danny Kiondo wanakulilia.
Mimi, Dr Ndege, Mishy Singano, Jackie Chengula (tunamwita
JACKIE mkubwa kwa kuwa wewe ulikua unajiita Jackie mdogo), Simon Simalenga,
Amani Siri, Douglas Pius, Arnold Kayanda (hadi harusi yake ulisimamia), Geah
Habib, Regina Mwalekwa, Ruge Mutahaba, Team Njiapanda ya tangu 2003 mpaka ya
leo wote tunakulilia mdogo wetu.
Kwetu sisi wote wewe bado ni Jackie wa Njiapanda yule wa
tangu 2004. Mdogo wetu mwenye upendo na uliyekua tayari kutumia hadithi ya
maisha yako kama fundisho kwa wengine. Wewe ni shujaa na kamwe hilo halitokaa
libadilike. Sheria itachukua mkondo wake kwa wote waliosababisha kifo chako na
Mungu atamhukumu kila mtu kwa jinsi alivyotenda.
Ninalia sana, ninahuzunika sana ninatamani ningeweza kufanya
lolote lakini nimeshindwa ndio maana nikashindwa kukuokoa na hili, Mungu
atanisamehe maisha yameniweka mbali na wewe mdogo wangu mpaka mauti yamekukuta.
Kibaya Zaidi ni kuwa hata kukuzika sitaweza kwa kuwa niko mbali na nyumbani.
Lakini ninaamini huko ulipo utafurahi kufahamu kuwa ninafanya yote haya
ninayofanya ili niweze kuwasaidia waTanzania wenzetu vizuri Zaidi nao wawe na
afya njema kama nilivyojitahidi kufanya yako iwe.
Ulale pema peponi mdogo wangu, Jackline Masanja..
Mungu ibariki familia yako,
Mungu ibariki Clouds Media Group
Mungu ibariki Njiapanda
No comments:
Post a Comment