Pages

Wednesday, November 26, 2014

Mahakama ilimshindwa Davido, inawezaje kuzuia Escrow Bungeni?

Kila Mtanzania anangoja kusikia mbivu na mbichi ndani ya Ripoti ya Escrow kwa mujibu wa uchunguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kisha kuwekwa pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
 Watanzania wapo njia panda, hawajui mchele ni upi, chuya zipi. Upo ukweli unaosambazwa lakini uongo umekuwa mwingi sana. Hao walio njiapanda ndiyo wenye nchi yao. Wao ndiyo mabosi wa serikali, mahakama na bunge.
 Mihimili yote hiyo lazima ifanye kazi kwa maslahi ya wananchi. Serikali, bunge au mahakama, inapofanya kazi kinyume na kile ambacho wananchi wanataka hiyo ni batili. Leo Watanzania wanataka Ripoti ya Escrow, ndiyo maslahi yao yalipo.


Wanataka kujua hali halisi ya rasilimali zao, eti linaibuliwa Zuio la Mahakama, kwamba bunge lisisome wala kujadili Escrow.
Chombo gani kisichojua wananchi wanataka nini kwa sasa? Sasa kwa nini kitende kinyume na maslahi ya Watanzania? Chenyewe kinatoa huduma zake kwa muongozo na thamani ipi ikiwa kinapishana na matakwa na wananchi?

Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria, kuelekeza na kutoa haki. Haiwezi kutafsiri sheria bila kutungwa na bunge. Yaani wabunge wanaochaguliwa na wananchi, hutunga sheria kwa maslahi ya wapigakura. Kwa mantiki hiyo, mahakama hutafsiri sheria zilizotungwa na wawakilishi wa wananchi kwa maslahi ya wananchi.

Mhimili nambari moja, yaani serikali, kazi yake ni kusimamia na kutekeleza hizo sheria kama zilivyotungwa na wawakilishi wa wananchi (bunge), vilevile kama zilivyotafsiriwa na mahakama. Mpaka hapo utaona kuwa wananchi ndiyo mabosi wa mihimili yote.

Ufafanuzi huo, utoshe kuonesha kuwa mahakama kwa kuzingatia kiu ya wananchi, vilevile kwa kutii matakwa ya wenye nchi, na kwa kuepusha hali ya hatari ambayo inaweza kujitokeza pale wananchi watakapopandwa na hasira kuona dola inakwenda kinyume nao, mahakama haina budi kujiweka kando na kuacha bunge litende kazi yake.

Skendo ya Escrow ni nzito; wahuni wavaa suti wamekwapua zaidi ya shilingi bilioni 300 za Watanzania. Wamiliki wa hizo fedha wanataka kusikia wawakilishi wao (wabunge), wanachukua hatua gani kuwanyoosha hao wezi na wasaliti wakubwa wa rasilimali zao.

Mahakama ni ya wanasheria. Basi niwakumbushe msemo wao kwamba “haki siyo tu itendeke, bali ionekane ikitendeka.” Kwa kuheshimu huo msemo wao, niwaambie kuwa wananchi wa Tanzania hawataona haki inatendeka kama Ripoti ya Escrow haitasomwa na kujadiliwa bungeni.


JE, MAHAKAMA INATAKA KUVUNJA KATIBA YA NCHI ?

Hakuna chombo wala mtu yeyote anayeruhusiwa kuvunja Katiba. Sheria au uamuzi wowote unaokwenda kinyume na Katiba ni batili. Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ambayo bado ipo hai, Ibara ya 100 katika vifungu vyake viwili vinavyoelezea Madaraka na Haki za Bunge, vinazuia mahakama kuingilia bunge.

Inatamka;

(1) Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali pengine nje ya bunge. (hapa Katiba imeifunga mahakama dhidi ya uhuru wa bunge)

(2) Bila kuathiri Katiba au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika. Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya bunge au aliloleta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.

Vifungu hivyo viwili vipo pia kwenye Sheria namba 15, ibara ya 14, iliyotungwa mwaka 1984, kuhusu Uhuru wa Majadiliano na Uratibu wa Shughuli bungeni.

Bunge pia linabebwa na Katiba katika Ibara ya 101, inasema: “Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuwezesha mahakama na sheria kuhifadhi na kutilia nguvu uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu wa shughuli katika bunge ambao kwa mujibu wa Ibara ya 100 umedhaminiwa na katiba.”

Mpaka hapo ni wazi Katiba inaigaragaza mahakama. Amri ya Zuio la Mahakama (Court Injunction Order), haina ubavu mbele ya bunge. Hao majaji ambao wamekaa kikao na watuhumiwa wa Escrow na kuamua kuwabeba kwa mtindo wa Amri ya Zuio, wamefeli kikatiba.

Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, kwa ufasaha kabisa, inapigilia msumari kuwa mahakama haitaingilia bunge. Kwa maana hiyo, Amri ya Zuio kwa bunge ni kuendelea kushusha hadhi chombo hicho.


NINI UHURU WA MAHAKAMA? NINI UHURU WA BUNGE ?

Bunge haliruhusiwi kuingilia uhuru wa mahakama. Kadhalika mahakama inakatazwa kuingilia uhuru wa majadiliano na uendeshwaji wa shughuli ndani ya bunge. Kila mhimili umekatazwa, sasa nani anastahili nini?

Kwa kifupi ni kwamba bunge halitathubutu kujadili kesi iliyopo mahakamani, kwa msingi kwamba shauri lilifunguliwa mahakamani kabla ya kufika bungeni. Katika mazingira hayo, ikitokea bunge limejadili kesi hiyo, litakuwa limeingilia uhuru wa mahakama.

Kama shauri limeanzia bungeni kabla ya kufika mahakamani, mahakama haitakuwa na budi kuacha mchakato wa kibunge kuendelea, huku yenyewe ikijikita kwenye utekelezaji wa kutafsiri sheria katika kesi husika pasipo kutekwa na uelekeo au uamuzi wa bunge.

Sakata la Escrow lilianzia bungeni, Kamati ya PAC ikaandaa hadidu za rejea na kumkabidhi CAG achunguze. Upande wa pili, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda naye aliiagiza Takukuru. Maagizo yote yalitoka katika mfumo wa bunge. Kwa hiyo, mahakama haina ubavu wa kuzuia bunge lisiendelee na kazi yake.

Kwa nini bunge na kinga? Tafsiri ni kuwa wabunge wapo kwa ajili ya wananchi, kwa hiyo lazima walindwe wanapokuwa wanafanya kazi yao ya uwakilishi wa wananchi katika kutunga sheria na kuisimamia serikali.

Mwaka 1883, Bunge la Canada liliambiwa na kuitikia kwa pamoja kuwa “Kinga za bunge ni kinga za wananchi na haki za bunge ni haki za wananchi.” Kwa maana hiyo, mahakama ikizuia Escrow isijadiliwe bungeni, itakuwa kwa pamoja imevunja kinga na haki za wananchi.

Mwandishi Erskine May, katika kitabu chake ‘Treaties on the Law, Privileges, Proceedings and Usage of Parliament’ ameandika: “Haki za bunge ni haki zote za kipekee za bunge na za kila mbunge binafsi kwa jumla, ambazo bila kuwepo kwake, bunge na wabunge hawawezi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”

Suala la kuwashughulikia wezi wa Escrow ni moja ya majukumu ya wabunge. Sasa kwa tafsiri ya Erskine, hapo kinga ya bunge na wabunge itakuwa wapi ikiwa watakubali zuio la mahakama kujadili ripoti hiyo. Labda isemwe leo kuwa bunge halina kinga na Katiba ya nchi iwe imevunjwa.


SPIKA AKIKUBALI ESCROW ISIJADILIWE TATIZO NI YEYE

Spika wa Bunge ni mtu mkubwa sana katika nchi. Ukiondoa Rais na Makamu wa Rais, Katiba inamtambulisha kama yeye ndiye bosi namba tatu, halafu wa nne nne ni Jaji Mkuu. Mama Anne Makinda ni mkuu wa nchi baada ya Rais na Makamu wa Rais. Katiba inasema hivyo.

Kwa kutambua nafasi yake kwamba yeye ni mkubwa kuliko Jaji Mkuu (kikatiba), vilevile mhimili anaouongoza ni namba mbili baada ya serikali, mahakama ni wa tatu. Hana sababu yoyote ya kuburuzwa au kuyumbushwa ukizingatia anazo kinga zote.

Uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusitisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadili Ripoti ya CAG kwa hati ya dharura, eti mpaka hoja ya msingi ipatiwe ufumbuzi ni mtego hatari kwa wananchi dhidi ya bunge, mahakama na serikali yao.

Kwa nini walalamikaji waende kufungua kesi baada ya kubaini ‘uharamia’ wao umegundulika? Walikuwa wapi wakati PAC inamuagiza CAG kwenda kufanya ukaguzi? Baada ya kuona upepo wa kaskazi na kusi umekuwa kimbunga ndiyo wakimbilie mahakamani?

Hoja yao kwa nini CAG alifanya ukaguzi wakati mahakama ilishatoa hukumu? Hoja dhaifu sana, yaani walitegemea fedha zote zaidi ya shilingi bilioni 300 zibebwe na ukaguzi usifanyike. Hapohapo ipo hoja kuwa mahakama haijawahi kutamka popote kuwa IPTL ilishinda kesi.

Spika wa Bunge anaweza kuamua mambo mawili, ama kukubali kudharauliwa kwa kuwa mtiifu wa mahakama (kinyume na Katiba ya nchi) halafu baadaye abebe msalaba wa dhambi za wezi sambamba na kuonja machungu ya hasira za wananchi, au asimamie heshima na thamani yake kwa kuendelea na Ripoti ya Escrow ili ajiandike historia iliyotukuka, kasha vizazi vijavyo vimkumbuke.

Kwa kifupi ni kwamba kama Ripoti ya Escrow haitajadiliwa bungeni, maana yake Makinda atakuwa hajiamini na haelewi nguvu ya mhimili anaouongoza. Zaidi ya hapo atakuwa amevunja Katiba ya Nchi. Upande wa pili, itaonekana kuna madudu anaficha na zuio la mahakama ni mbeleko tu.

Majaji watatu waliotoa Amri ya Zuio kwa bunge leo, wamekiuka Sheria namba 15, Ibara ya 14, ya mwaka 1984 inayohusu Uhuru wa Majadiliano na Uratibu wa Shughuli ndani ya bunge. Wamekosa heshima kwa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, vilevile wamevunja Katiba Ibara ya 100.

Makinda pia kwa kukubali kusitisha mjadala wa Escrow, atakuwa ameshindwa hata kutumia fursa ambayo amepewa na Katiba katika Ibara ya 101, kwamba bunge linaweza kutunga sheria ya kujilinda, kujihifadhi dhidi ya mahakama. Sheria hiyo inatungwa chini ya dhamana ya Ibara ya 100.


AMRI YA ZUIO ILIGONGA MWAMBA KWA DAVIDO;

Oktoba 18, mwaka huu, mwanamuziki kutoka Nigeria, David Adedeji Adeleke ‘Davido’ alipanda jukwaani, akatumbuiza na kuondoka kurudi nchini kwao bila kupata usumbufu wowote.

Davido alipanda jukwaa la Fiesta wakati kulikuwa na Amri ya Zuio kutoka Mahakama ya Kisutu, ikiikataza Kampuni ya Prime Time Promotion kumtumia Davido kwenye shoo ya Fiesta kutokana na mgogoro wa kimkataba baina yake na Kampuni ya Times Promotions and Entertainment, vilevile alinyimwa kibali na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Hata hivyo, Davido alipanda jukwaani na hakuna uamuzi wowote wa dharura ambao ulichukuliwa kutoa fundisho kwa wakaidi wa Amri ya Zuio. Ile adhabu ya kudharau mahakama (Contempt) haikufanya kitu.

Ni aibu kubwa kwa taifa letu ambalo linaongozwa na misingi ya sheria na dola. Ni nchi isiyokuwa na dola peke yake ndiyo alichokifanya Davido hapa nchini kinaweza kutokea na kuvumiliwa kana kwamba hakikutokea kitu. Mahakama haikuona aibu hii!

Kama kwa Davido ilitokea hivyo, nitashangaa sana kama bunge litanywea na kuamua kusitisha hoja nzito yenye maslahi mapana kwa taifa. Bunge linaweza kuendelea na kazi yake. Halafu wahusika waendelee kutapatapa mahakamani. Swali; kama kweli ni watu wazuri na walitenda kilicho halali na haki, wasiwasi wa kukimbilia mahakamani wa nini wakati Ripoti ya Escrow haijasomwa?

Jibu ni kwamba wanajua walichokifanya na wanaelewa kilichomo ndani ya Ripoti ya Escrow na wanatambua nini ambacho kinaenda kusomwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, kwa maana hiyo ni waelewa wa kile kinachokaribia kuwapata. Ripoti isomwe, hata wakizuia itavuja na wananchi watachukua uamuzi. Tuache kulinda ufisadi kwa amani yetu na maendeleo ya uchumi wetu.

Mungu ibariki Tanzania.

Mungu waongoze wabunge wetu kusimama kidete Ripoti ya Escrow isomwe.


By Luqman Maloto

No comments:

Post a Comment