Kila Mtanzania anangoja kusikia mbivu na mbichi ndani ya
Ripoti ya Escrow kwa mujibu wa uchunguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kisha kuwekwa pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Wanataka kujua hali halisi ya rasilimali zao, eti
linaibuliwa Zuio la Mahakama, kwamba bunge lisisome wala kujadili Escrow.
Chombo gani kisichojua wananchi wanataka nini kwa sasa? Sasa
kwa nini kitende kinyume na maslahi ya Watanzania? Chenyewe kinatoa huduma zake
kwa muongozo na thamani ipi ikiwa kinapishana na matakwa na wananchi?
Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria, kuelekeza na kutoa
haki. Haiwezi kutafsiri sheria bila kutungwa na bunge. Yaani wabunge
wanaochaguliwa na wananchi, hutunga sheria kwa maslahi ya wapigakura. Kwa
mantiki hiyo, mahakama hutafsiri sheria zilizotungwa na wawakilishi wa wananchi
kwa maslahi ya wananchi.
Mhimili nambari moja, yaani serikali, kazi yake ni kusimamia
na kutekeleza hizo sheria kama zilivyotungwa na wawakilishi wa wananchi
(bunge), vilevile kama zilivyotafsiriwa na mahakama. Mpaka hapo utaona kuwa
wananchi ndiyo mabosi wa mihimili yote.
Ufafanuzi huo, utoshe kuonesha kuwa mahakama kwa kuzingatia
kiu ya wananchi, vilevile kwa kutii matakwa ya wenye nchi, na kwa kuepusha hali
ya hatari ambayo inaweza kujitokeza pale wananchi watakapopandwa na hasira
kuona dola inakwenda kinyume nao, mahakama haina budi kujiweka kando na kuacha
bunge litende kazi yake.
Skendo ya Escrow ni nzito; wahuni wavaa suti wamekwapua
zaidi ya shilingi bilioni 300 za Watanzania. Wamiliki wa hizo fedha wanataka
kusikia wawakilishi wao (wabunge), wanachukua hatua gani kuwanyoosha hao wezi
na wasaliti wakubwa wa rasilimali zao.
Mahakama ni ya wanasheria. Basi niwakumbushe msemo wao
kwamba “haki siyo tu itendeke, bali ionekane ikitendeka.” Kwa kuheshimu huo
msemo wao, niwaambie kuwa wananchi wa Tanzania hawataona haki inatendeka kama
Ripoti ya Escrow haitasomwa na kujadiliwa bungeni.
JE, MAHAKAMA INATAKA KUVUNJA KATIBA YA NCHI ?
Hakuna chombo wala mtu yeyote anayeruhusiwa kuvunja Katiba.
Sheria au uamuzi wowote unaokwenda kinyume na Katiba ni batili. Katiba ya
Tanzania ya mwaka 1977 ambayo bado ipo hai, Ibara ya 100 katika vifungu vyake
viwili vinavyoelezea Madaraka na Haki za Bunge, vinazuia mahakama kuingilia
bunge.
Inatamka;
(1) Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu
katika bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika
Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali pengine nje ya bunge. (hapa
Katiba imeifunga mahakama dhidi ya uhuru wa bunge)
(2) Bila kuathiri Katiba au masharti ya sheria nyingine
yoyote inayohusika. Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai
mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya bunge au
aliloleta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.
Vifungu hivyo viwili vipo pia kwenye Sheria namba 15, ibara
ya 14, iliyotungwa mwaka 1984, kuhusu Uhuru wa Majadiliano na Uratibu wa
Shughuli bungeni.
Bunge pia linabebwa na Katiba katika Ibara ya 101, inasema:
“Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuwezesha mahakama
na sheria kuhifadhi na kutilia nguvu uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu
wa shughuli katika bunge ambao kwa mujibu wa Ibara ya 100 umedhaminiwa na
katiba.”
Mpaka hapo ni wazi Katiba inaigaragaza mahakama. Amri ya
Zuio la Mahakama (Court Injunction Order), haina ubavu mbele ya bunge. Hao
majaji ambao wamekaa kikao na watuhumiwa wa Escrow na kuamua kuwabeba kwa
mtindo wa Amri ya Zuio, wamefeli kikatiba.
Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, kwa ufasaha
kabisa, inapigilia msumari kuwa mahakama haitaingilia bunge. Kwa maana hiyo,
Amri ya Zuio kwa bunge ni kuendelea kushusha hadhi chombo hicho.
NINI UHURU WA MAHAKAMA? NINI UHURU WA BUNGE ?
Bunge haliruhusiwi kuingilia uhuru wa mahakama. Kadhalika
mahakama inakatazwa kuingilia uhuru wa majadiliano na uendeshwaji wa shughuli
ndani ya bunge. Kila mhimili umekatazwa, sasa nani anastahili nini?
Kwa kifupi ni kwamba bunge halitathubutu kujadili kesi
iliyopo mahakamani, kwa msingi kwamba shauri lilifunguliwa mahakamani kabla ya
kufika bungeni. Katika mazingira hayo, ikitokea bunge limejadili kesi hiyo,
litakuwa limeingilia uhuru wa mahakama.
Kama shauri limeanzia bungeni kabla ya kufika mahakamani,
mahakama haitakuwa na budi kuacha mchakato wa kibunge kuendelea, huku yenyewe
ikijikita kwenye utekelezaji wa kutafsiri sheria katika kesi husika pasipo
kutekwa na uelekeo au uamuzi wa bunge.
Sakata la Escrow lilianzia bungeni, Kamati ya PAC ikaandaa
hadidu za rejea na kumkabidhi CAG achunguze. Upande wa pili, Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda naye aliiagiza Takukuru. Maagizo yote yalitoka katika mfumo wa
bunge. Kwa hiyo, mahakama haina ubavu wa kuzuia bunge lisiendelee na kazi yake.
Kwa nini bunge na kinga? Tafsiri ni kuwa wabunge wapo kwa
ajili ya wananchi, kwa hiyo lazima walindwe wanapokuwa wanafanya kazi yao ya
uwakilishi wa wananchi katika kutunga sheria na kuisimamia serikali.
Mwaka 1883, Bunge la Canada liliambiwa na kuitikia kwa
pamoja kuwa “Kinga za bunge ni kinga za wananchi na haki za bunge ni haki za
wananchi.” Kwa maana hiyo, mahakama ikizuia Escrow isijadiliwe bungeni, itakuwa
kwa pamoja imevunja kinga na haki za wananchi.
Mwandishi Erskine May, katika kitabu chake ‘Treaties on the
Law, Privileges, Proceedings and Usage of Parliament’ ameandika: “Haki za bunge
ni haki zote za kipekee za bunge na za kila mbunge binafsi kwa jumla, ambazo
bila kuwepo kwake, bunge na wabunge hawawezi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”
Suala la kuwashughulikia wezi wa Escrow ni moja ya majukumu
ya wabunge. Sasa kwa tafsiri ya Erskine, hapo kinga ya bunge na wabunge itakuwa
wapi ikiwa watakubali zuio la mahakama kujadili ripoti hiyo. Labda isemwe leo
kuwa bunge halina kinga na Katiba ya nchi iwe imevunjwa.
SPIKA AKIKUBALI ESCROW ISIJADILIWE TATIZO NI YEYE
Spika wa Bunge ni mtu mkubwa sana katika nchi. Ukiondoa Rais
na Makamu wa Rais, Katiba inamtambulisha kama yeye ndiye bosi namba tatu, halafu
wa nne nne ni Jaji Mkuu. Mama Anne Makinda ni mkuu wa nchi baada ya Rais na
Makamu wa Rais. Katiba inasema hivyo.
Kwa kutambua nafasi yake kwamba yeye ni mkubwa kuliko Jaji
Mkuu (kikatiba), vilevile mhimili anaouongoza ni namba mbili baada ya serikali,
mahakama ni wa tatu. Hana sababu yoyote ya kuburuzwa au kuyumbushwa ukizingatia
anazo kinga zote.
Uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusitisha
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadili Ripoti ya CAG kwa hati ya
dharura, eti mpaka hoja ya msingi ipatiwe ufumbuzi ni mtego hatari kwa wananchi
dhidi ya bunge, mahakama na serikali yao.
Kwa nini walalamikaji waende kufungua kesi baada ya kubaini
‘uharamia’ wao umegundulika? Walikuwa wapi wakati PAC inamuagiza CAG kwenda
kufanya ukaguzi? Baada ya kuona upepo wa kaskazi na kusi umekuwa kimbunga ndiyo
wakimbilie mahakamani?
Hoja yao kwa nini CAG alifanya ukaguzi wakati mahakama
ilishatoa hukumu? Hoja dhaifu sana, yaani walitegemea fedha zote zaidi ya
shilingi bilioni 300 zibebwe na ukaguzi usifanyike. Hapohapo ipo hoja kuwa
mahakama haijawahi kutamka popote kuwa IPTL ilishinda kesi.
Spika wa Bunge anaweza kuamua mambo mawili, ama kukubali
kudharauliwa kwa kuwa mtiifu wa mahakama (kinyume na Katiba ya nchi) halafu
baadaye abebe msalaba wa dhambi za wezi sambamba na kuonja machungu ya hasira
za wananchi, au asimamie heshima na thamani yake kwa kuendelea na Ripoti ya
Escrow ili ajiandike historia iliyotukuka, kasha vizazi vijavyo vimkumbuke.
Kwa kifupi ni kwamba kama Ripoti ya Escrow haitajadiliwa
bungeni, maana yake Makinda atakuwa hajiamini na haelewi nguvu ya mhimili
anaouongoza. Zaidi ya hapo atakuwa amevunja Katiba ya Nchi. Upande wa pili,
itaonekana kuna madudu anaficha na zuio la mahakama ni mbeleko tu.
Majaji watatu waliotoa Amri ya Zuio kwa bunge leo, wamekiuka
Sheria namba 15, Ibara ya 14, ya mwaka 1984 inayohusu Uhuru wa Majadiliano na
Uratibu wa Shughuli ndani ya bunge. Wamekosa heshima kwa Sheria ya Kinga,
Madaraka na Haki za Bunge, vilevile wamevunja Katiba Ibara ya 100.
Makinda pia kwa kukubali kusitisha mjadala wa Escrow,
atakuwa ameshindwa hata kutumia fursa ambayo amepewa na Katiba katika Ibara ya
101, kwamba bunge linaweza kutunga sheria ya kujilinda, kujihifadhi dhidi ya
mahakama. Sheria hiyo inatungwa chini ya dhamana ya Ibara ya 100.
AMRI YA ZUIO ILIGONGA MWAMBA KWA DAVIDO;
Oktoba 18, mwaka huu, mwanamuziki kutoka Nigeria, David
Adedeji Adeleke ‘Davido’ alipanda jukwaani, akatumbuiza na kuondoka kurudi
nchini kwao bila kupata usumbufu wowote.
Davido alipanda jukwaa la Fiesta wakati kulikuwa na Amri ya
Zuio kutoka Mahakama ya Kisutu, ikiikataza Kampuni ya Prime Time Promotion
kumtumia Davido kwenye shoo ya Fiesta kutokana na mgogoro wa kimkataba baina
yake na Kampuni ya Times Promotions and Entertainment, vilevile alinyimwa
kibali na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Hata hivyo, Davido alipanda jukwaani na hakuna uamuzi wowote
wa dharura ambao ulichukuliwa kutoa fundisho kwa wakaidi wa Amri ya Zuio. Ile
adhabu ya kudharau mahakama (Contempt) haikufanya kitu.
Ni aibu kubwa kwa taifa letu ambalo linaongozwa na misingi
ya sheria na dola. Ni nchi isiyokuwa na dola peke yake ndiyo alichokifanya
Davido hapa nchini kinaweza kutokea na kuvumiliwa kana kwamba hakikutokea kitu.
Mahakama haikuona aibu hii!
Kama kwa Davido ilitokea hivyo, nitashangaa sana kama bunge
litanywea na kuamua kusitisha hoja nzito yenye maslahi mapana kwa taifa. Bunge
linaweza kuendelea na kazi yake. Halafu wahusika waendelee kutapatapa
mahakamani. Swali; kama kweli ni watu wazuri na walitenda kilicho halali na
haki, wasiwasi wa kukimbilia mahakamani wa nini wakati Ripoti ya Escrow
haijasomwa?
Jibu ni kwamba wanajua walichokifanya na wanaelewa kilichomo
ndani ya Ripoti ya Escrow na wanatambua nini ambacho kinaenda kusomwa na Mwenyekiti
wa PAC, Zitto Kabwe, kwa maana hiyo ni waelewa wa kile kinachokaribia kuwapata.
Ripoti isomwe, hata wakizuia itavuja na wananchi watachukua uamuzi. Tuache
kulinda ufisadi kwa amani yetu na maendeleo ya uchumi wetu.
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu waongoze wabunge wetu kusimama kidete Ripoti ya Escrow
isomwe.
By Luqman Maloto
No comments:
Post a Comment