Pages

Thursday, November 27, 2014

Makamu Rais Zimbabwe atimuliwa ZANU-PF


Vyombo vya habari vya Serikali nchini Zimbabwe vinaripoti kuwa Makamu wa Rais,Joyce Mujuru, ameondolewa kwenye kamati kuu ya chama cha ZANU-PF.
Mujuru anashutumiwa kupanga mauaji dhidi ya Rais wa nchi hiyo,Robert Mugabe.
Hatua hiyo imekuja baada ya Kampeni dhidi ya Mujuru iliyofanywa na Mke wa Rais Mugabe, Grace ambaye kwa kiasi kikubwa anaamini anataka kumrithi Mumewe atakapotoka madarakani.


Viongozi kadhaa wa ZANU-PF wameshindwa kutetea nafasi zao katika Chama hicho.
Bi Mujuru alitarajiwa kumrithi rais Mugabe mwenye umri wa miaka tisini.
Kamati ya uchaguzi katika mkoa wa kaskazini wa Mashonaland ya kati imekataa wasifu wa Makamu wa rais nchi hiyo Joice Mujuru kama baadhi ya stakabadhi zake za kuomba kazi katika uchaguzi uliofanyika siku ya Jumanne.
Bi Mujuru ambae alikuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha ZANU PF, alikuwa pia waziri mchanga zaidi katika baraza la mawaziri la rais Robert Mugabe wakati taifa hilo lilipojinyakulia uhuru wake mwaka wa 1980.
Alipanda ngazi na kuwa kiongozi wa pili mwenye ushawishi zaidi chamani kutokana na wasifu wake wakati wa vita vya uhuru dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza.
Katika kipindi cha miezi michache iliyopita - amekuwa akishambuliwa katika mikutano ya kampeni kutoka kwa mke wa rais Robert Mugabe, Grace, ambaye anamhutumu kwa kutowajibika, ufisadi na amemtaka ajiuzulu.
Kumekuwa na fununu kuwa Bi. Mugabe amekuwa na nia na ari ya kutaka kumrithi mumewe.
Mmoja wa wapinzani wakuu wa Mujuru, ni Waziri wa Sheria Emmerson Mnangagwa, na inaaminika kuwa ni mmoja wa wagombea wakuu ambao wanaongoza katika harakati za kumrithi rais Mugabe ambaye anatimu miaka 91 miezi mitatu ijayo.

Haijabainika ikiwa Mujuru atahudhuria kongamano la uchaguzi wa chama cha ZANU PF wiki ijayo, ambapo uongozi mpya wa chama hicho utateuliwa

No comments:

Post a Comment