Pages

Wednesday, November 5, 2014

MSHTUKO!!!SITTI MTEMVU ATOWEKA



Stori: Chande Abdallah na Deogratius Mongela
WAKATI suala la kudaiwa kudanganya umri likiwa bado ‘bichii’, taarifa zinadai kuwa mshindi wa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu ametoweka na hajulikani alipo, Risasi Mchanganyiko limechimbua stori kamili.
Mshindi wa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu.
Shughuli ya kumsaka mrembo huyo ili kujua undani wa sakata lake ilianzia Temeke ambako ilielezwa kuwa ndiko anakoishi.
Mapaparazi wetu walipofika katika nyumba waliyoelekezwa, walikuta imebadilishwa na kuwa Ofisi ya Vikoba ambapo mmoja wa wahudumu wa ofisi hiyo kwa sharti la kutoanika jina lake gazetini, aliwataka waandishi wetu kwenda Mbezi-Makonde akidai ndiko anakoishi kwa sasa.
“Hapa ilikuwa nyumba ya zamani lakini kwa sasa ni ofisi na Sitti hakai hapa, kama mnamtaka nendeni Mbezi-Makonde huko nasikia ndiko anakoishi,” alisema mtumishi huyo.

 
Mapaparazi wetu hawakuchoka, walifunga safari hadi Mbezi-Makonde ambapo walikuta nyumba yenye maduka yaliyoandikwa Mtemvu Foundation, wakaenda moja kwa moja katika saluni mojawapo iliyokuwa na bango lililosomeka Malisa huku likiwa na picha ya Sitti sambamba na namba za simu.
Sitti Mtemvu wakati wa kutwaa taji la Miss Tanzania 2014.
Dada mmoja aliyeonekana kufanana na Sitti alizidi kutibua hali ya hewa baada ya kusema Sitti amesafiri nje ya nchi pasipo kufafanua nchi gani.“Sitti amesafiri nje ya nchi, ila kama mnamtaka nafikiri nitawapa namba zake akirudi kati ya Jumatatu au Jumatano ya wiki ijayo (wiki hii),” alisema dada huyo pasipo kutaja jina lake.
Mmoja wa majirani wa mrembo huyo alihoji inawezekanaje mrembo huyo akasafiri nje ya nchi wakati suala lake la umri halijapata ufumbuzi?“Mh! Ataondokaje wakati bado ana majanga ya umri?” alihoji jirani huyo.
Aidha, mapaparazi wetu hawakutaka kuishia hapo, Jumapili iliyopita walitia timu Buza Kipera katika Kanisa la The Revelation Church la Nabii Yaspi Bendera ambalo ilielezwa kuwa Sitti anaabudu, ili kujiridhisha kama yupo, lakini pia hakuonekana huku waumini wakidai hawajamuona kwa siku za karibuni.Nabii Yaspi Bendera wa Kanisa la The Revelation Church.
“Hatumuoni siku hizi, ila alikuwa anakuja katika ibada ya peke yake kwa nabii saa kumi lakini siku za karibuni hatumuoni,” alisema muumini mmoja.Katika ibada inayoendeshwa kanisani hapo ambayo mapaparazi wetu walizama ‘kiintelijensia’, Nabii Yaspi alisikika akimkingia kifua Sitti kuwa alistahili ushindi na kumtabiria kufika mbali na hata kuwa Miss World huku akiwaonya wanaomfuatilia mrembo huyo.
“Mara ya kwanza nilimtabiria Sitti kushinda u-miss Tanzania na kweli akashinda, sasa wanatokea watu wakidai mara ana hipsi kubwa, ooh kadanganya umri, huu wote ni upepo tu na utapita.“Kama Sitti hatakengeuka kwenye imani yake atafika mbali zaidi na kushinda hata Miss World. Wale wote watakaoendelea kumfuatilia wataparalaizi,” alisema Nabii Yaspi.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), walisema bado wanalifanyia uchunguzi suala la Ritta kudaiwa kufoji cheti cha kuzaliwa kutokana na baadhi ya nyaraka zake kuonesha amezaliwa mwaka 1989 huku yeye akidai amezaliwa 1991.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara akitafakari jambo.
Wakati RITA na BASATA wakiwa hawajatoa tamko lolote kufuatia uchunguzi waliodai wataufanya, gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara ili azungumzie sakata hilo.
“Waziri ni mtu mkubwa sana kuzungumzia suala kama hilo, watafute wasaidizi wangu pale wizarani watakuambia kinachoendelea. Naweza kutoa tamko halafu nikaonekana mtu wa ajabu, kumbe watu wanaendelea kulifanyia kazi, nenda kamuone Mkurugenzi wa Utamaduni atakusaidia,” alisema Waziri huyo alipozungumza nasi kwa njia ya simu.

No comments:

Post a Comment