Juzi jioni baada ya uchaguzi niliondoka Nzega kuja Dar es salaam kujiandaa kwa safari ya kumpeleka baba yangu India kwa matibabu. Alfajir, majira ya saa 10 na nusu, nikapata taarifa kutoka jimboni kuwa kuna vijana wawili wamepigwa risasi za moto kwenye zoezi la kuhesabu kura Kituo cha Imeli na wako mahtuti hospitalini. Mmoja kafariki jana mchana. Mwingine bado amelazwa hospitalini. Miezi kadhaa iliyopita nilikoswa kuuawa na polisi kwenye moja ya mikutano yangu jimboni. Mimi siyo mtaalamu wa usalama, lakini najiuliza, hivi hakuna namna nyingine ya kutuliza ghasia zaidi ya hii ya kulenga wananchi wasio na silaha kwa risasi za moto? Leo wananchi wenzangu wameandamana jimboni wakilaani siyo tu Jeshi la polisi bali pia na chama changu na serikali yake. Naungana na wananchi wenzangu kupinga na kukemea vikali kitendo hiki. Naungana nao katika majonzi haya makubwa na ninaahidi kuiwajibisha serikali mpaka
tutakapopatiwa taarifa ya hatua za kinidhamu na za kisheria alizochukuliwa askari aliyefanya kitendo hiki kiovu na kisichokubalika kwenye jamii! Tunahitaji majibu haya haraka iwezekanavyo kabla hatujatangaza hatua nyingine za nguvu ya umma tutakazochukua. Wakati serikali ikijipanga, ni mategemeo yangu kuwa, viongozi wa Serikali wanaohusika na ulinzi na usalama wa Raia na mali zao watajipima, wataona aibu na kuiona thamani ya damu na pumzi ya kijana mdogo Bartholomew Edward iliyokatiliwa bila sababu za msingi kwa kuwajibika kisiasa. Natuma salamu zangu za pole na rambi rambi kwa wazazi, familia yote, ndugu, jamaa na marafiki, na zaidi Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Pentekoste Nzega.
No comments:
Post a Comment