Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, December 22, 2014

NDIO BASI TENA KWA WACHEZAJI HAWA WA SIMBA NA YANGA


Dar es Salaam. Klabu za Simba na Yanga zimefanya mabadiliko kwenye vikosi vyao na moja kwa moja watakuwa wameathiri nafasi za baadhi ya wachezaji wa vikosi hivyo.

Timu zote hizo kongwe zimefanya mabadiliko zaidi katika kujiimarisha lakini pamoja na mapendekezo mapya yaliyowekwa, imewaweka pabaya baadhi ya wachezaji na hivyo kufanya wakati wao kuwa mgumu.

Yanga imewasajili Mliberia Kpah Sherman, Mrundi Amissi Tambwe na Danny Mrwanda kwenye safu ya ushambuliaji na kipa Athumani Majogo, wakati Simba imewasajili Dan na Simon Sserunkuma, Juku Musheed (wote raia wa Uganda) na Hassan Kessy. Wafuatao watakalia kuti kavu Simba kipindi hiki;

William Lucian ‘Gallas’

Usajili wa Hassan Kessy aliyetokea Mtibwa Sugar utampa wakati mgumu beki huyu na kwamba anaweza kuwa chaguo la pili kama si la tatu. Licha ya kuwa na uzoefu na umri wake bado ukiwa mdogo, Lucian atakuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi mbele ya Kessy, ambaye amekuwa akiwindwa na Simba kwa kipindi kirefu bila mafanikio hapo awali.

Nassor Masoud ‘Chollo’

Beki huyu mkongwe wa Simba ameonekana kurudisha makali yake hivi karibuni, lakini inasadikiwa uwepo Kessy utamrudisha tena benchi.


Chollo hajawa na kipindi kizuri kwa takribani mwaka sasa kutokana na matatizo ya majeraha. Chollo uenda akawa mbadala wa Kessy kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.

Hassan Isihaka:

Hakika amekuwa akifanya kazi kubwa na hata kuaminika kuanza kwenye michezo yote ya kirafiki na ya ligi kwa msimu huu. Isihaka amekuwa akicheza sambamba na Joseph Owino lakini hali ilivyo sasa baada ya usajili wa beki Juku Musheed, huenda akapoteza nafasi.

Shaban Kisiga ‘Marlone’

Licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuichezesha timu na kufunga mipira ya faulo. Kiungo huyo mshambuliaji anaweza kupoteza nafasi kwa washambuliaji Dani Sserunkuma na Elius Maguli ambao ni chaguo la kwanza la Kocha wa Simba Patrick Phiri aliyetokea kwenye klabu ya Gor Mahia ya Kenya.


Said Ndemla
Kiungo huyu amekuwa akijitahidi na mara kadhaa amekuwa akipata nafasi lakini ujio wa Simon Sserunkuma aliyetokea Express ya Uganda unaweza kuzima ndoto zake za kungaa kwani anaweza kuishia benchi kwa kusubiri mchezaji huyo apate nafasi.

Kwa Upande wa Yanga, Mambo yamebadilika na kwamba Kocha mpya wa klabu hiyo, Mholanzi Hans Van Pluijm na msaidizi wake, Boniface Mkwasa wanaweza kubadilisha mambo mengi huku wakiwapa wakati mgumu baadhi ya wachezaji;

Juma Kaseja:

Kipa huyu mkongwe hajaweza kuwa na wakati mzuri kwa kipindi kirefu tangu asajiliwe Yanga akiwa kama mchezaji huru. Kaseja ameshindwa kutamba mbele ya Deo Munishi ‘Dida’, ambaye ameshikilia nafasi yake.
Kaseja pia yuko kwenye hatari ya kupotea zaidi kwani ameshindwa hata kujiunga na timu kipindi hiki ligi iliposimama kwa madai kuwa anaidai Yanga lakini pia Yanga hawaheshimu mkataba wake.

Danny Mrwanda:
Pengine usajili wake Yanga umeikomoa Simba lakini Mrwanda ana wakati mgumu wa kupata nafasi mbele ya mshambuliaji Amissi Tambwe na Kpah Sherman. Mrwanda ni mchezaji mzoefu na mwenye uwezo wa juu, lakini atakuwa na wakati mgumu kwenye utafutaji wa namba kikosi cha kwanza Yanga.

Jerryson Tegete:
Tegete bila shaka amechemka, licha ya kuibuka mara kwa mara na kisha kutoweka tena, yupo kwenye nafasi ngumu hasa kutokana na ujio wa Tambwe, Mrwanda na Sherman.

Andrey Coutinho:
Baada ya Maximo kutupiwa virago, kiungo Andrey Coutinho huenda akajikuta kwenye wakati mgumu kutokana na falsafa za Hans Van Pluijim, ambaye tayari alikuwa ametengeneza wachezaji wake kabla ya kuachana na Yanga Mei mwaka huu.

Hussein Javu:

Mshambuliaji huyu anaweza kukumbana na changamoto kama anazozipata mwenzake Tegete. Atahitajika aweke juhudi za hali ya juu kwa kuwa ndiyo kwanza ametokea majeruhi pia hajaweza kupata muda mwingi wa kucheza.

No comments:

Post a Comment