Na Dunstan Shekidele, GPL, MOROGORO
WATU kadhaa wamejeruhiwa katika vurugu zilizotokea jioni hii huko Dumila
mkoani Morogoro kati ya wakulima na wafugaji ambapo polisi wameingilia
kati na kutumia mabaomu ya machozi kutuliza ghasia hizo.
Chanzo cha vurugu hizo kinadaiwa kuwa ni kukatwa mkono kwa mkulima mmoja
aishiye Kijiji cha Mketeni wilayani Kiloasa wakati akibishana na
mfugaji ambaye ni kabila la Kimasai kuhusu eneo la kulishia mifugo.
Kufuatia kitendo hicho cha kukatwa mkono, mkulima huyo aliwafuata
wenzake na kuwapa taarifa ambapo walikusanyika na kuanzisha vurugu dhidi
ya wafugaji wa eneo hilo.
Baada ya kuona kuwa bado haitoshi na baadhi ya wafugaji kukimbia,
wakulima walimalizia hasira zao katika Barabara ya Morogoro - Dodoma
ambapo waliamua kuifunga kwa takribani masaa mawili huku wakichoma
matairi.
Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliingilia kati na kutumia
mabomu ya machozi kuwatawanya wakulima ambao pia walikuwa tayari
wamevamia baadhi ya nyumba za kulala wageni zinazomilikiwa na wafugaji
eneo hilo na kufanya uharibifu.
Majeruhi katika vurugu hizo wamepelekwa hospitali kwa huduma ya kwanza.
No comments:
Post a Comment