Yule mganga aliyejitapa kumtengenezea nyota ya mvuto staa wa
Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ustadh Yahya amehukumiwa kifungo
cha miaka saba (7) jela baada ya kukutwa na hatia katika kisa cha kuchanganya
akihusishwa na wizi wa gari.
Ustadh Yahya akiwa chini ya ulinzi.
TUJIUNGE MAHAKAMA YA WILAYA YA ILALA
Habari za uhakika zilieleza kwamba aliyehitimisha kesi hiyo
ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar, Hassan
Kisailo mapema Jumatatu wiki hii wakati jua la asubuhi likiwaka.
HAKIMU ASHUSHA MIWANI
Huku kijasho chembamba kikimtiririka huku akishusha miwani
kidogo kuona wahudhuriaji wa kesi hiyo, Hakimu Kisailo alitoa hukumu hiyo kwa
maelezo kwamba, mnamo Januari 20, mwaka jana, maeneo ya Kariakoo jijini Dar,
Yahya alidaiwa kuiba gari aina ya Toyota RAV4 lenye namba za usajili T 139 BSJ
likiwa na thamani ya Sh. milioni 12, mali ya Edrick Elieza.
Wakati Hakimu Kisailo akisoma hukumu hiyo, mshtakiwa na
wadhamini wake hawakuwepo mahakamani hapo hivyo alisema mara tu baada ya hukumu
wahusika hao watakamatwa ili wakatumikie adhabu inayowakabili.
MAPITIO MTIRIRIKO WA KESI
Huku akiangalia kulia na kushoto, Hakimu Kisailo alisema
kuwa, baada ya kuupitia mtiririko wa kesi hiyo, alibaini kwamba ni kweli mshtakiwa
huyo alitenda kosa hilo hivyo alimhukumu kwenda jela miaka 7.
MANENO YA HAKIMU
Kama ilivyo desturi ya Magazeti ya Global kutaka kujua vitu
kwa undani, mwanahabari wetu alizungumza hakimu huyo kuhusiana na hukumu hiyo
ambapo alishusha tena miwani kidogo kisha kumwangalia kwa juu na kusema:
“Ni kweli huyo mnayemuita sijui Mganga wa Diamond
nimemhukumu kwenda jela miaka 7, ingawa hakuwepo hapa mahakamani.
“Nasikia alitoroka tangu alipowekewa dhamana lakini kifungo
hicho kitaanza muda wowote atakapokamatwa.”
WADHAMINI NAO WANALO
Hakimu Kisailo alisema kwamba, Ustadh Yahya aliwekewa
dhamana na watu wawili, Moses Msangi na Seme Kisusandi ambao wanatakiwa kulipa
faini ya shilingi milioni moja kila mmoja au kwenda jela miezi sita wakati
sangoma huyo akisakwa.
Hakimu Kisailo alisema licha ya jamaa huyo kuingia mitini,
wadhamini wake nao hawakuwepo mahakamani hapo na kusema kuwa mkono wa sheria ni
mrefu utawafikia popote pale walipo.
MANENO KUNTU
Mmoja wa mashuhuda wa kike aliyekuwa kwenye chumba cha
hakimu huyo alisikika akisema: “Huyo mganga wa Diamond hana lolote, iweje
ashindwe kuzima kesi yake na kufikia hatua ya kuhukumiwa kifungo hicho wakati
huwa anajidai ni mkali kwenye mambo ya kuwatengenezea watu nyota?
“Unaweza kukuta huko mitaani anajifanya kuwaambia wateja
wake ana uwezo wa kuzima ‘makesi’ makubwa-makubwa kumbe hata kesi yake mwenyewe
inamshinda.”
DIAMOND ATUPIWA LAWAMA
Shuhuda huyo alikwenda mbele zaidi na kumtupia lawama
Diamond kwamba alishindwaje kumsaidia mtu aliyempaisha hadi sasa hivi anawiki
kimataifa?
DIAMOND ANASEMAJE
Amani lilimsaka Diamond ili kumfikishia ‘ubuyu’ kuwa mganga
wake amehukumiwa miaka sasa jela lakini simu yake ya kiganjani iliita bila
kupokelewa na hata alipofuatwa nyumbani kwake, Sinza-Mori, Dar, hakuwepo.
TUMEFIKAJE HAPA?
Ustadh huyo alidaiwa kukamatwa na gari hilo alilodai kufika
mikononi mwake kutoka kwa mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Mwanahamis.
Ustadh alikamatwa akikatiza nalo Tabora
mjini ndipo akawekwa nyuma ya nondo za mahabusu kabla ya kusafirishwa jijini
Dar kwa hatua zaidi za kisheria ambazo zimemhukumu kifungo hicho.
No comments:
Post a Comment