Jana tarehe 13/01/2015 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake wa Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete
ilifanya kikao chake cha kawaida cha siku moja Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Pamoja na mambo mengine baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na
Kamati Kuu ni pamoja na:-
1. SAKATA LA AKAUNTI YA ESCROW.
Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na sakata hili.
Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua yafuatayo:-,
i). Pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali,
Kamati Kuu imeitaka serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza
maazimio ya bunge juu ya swala hilo.
ii). Kamati Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana wajenge
utamaduni wa kuwajibika kwa dhamana zao, na wasipowajibika waliowapa dhamana
wachukue hatua za kuwawajibisha.
iii). Aidha Kamati Kuu imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili
kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili
kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya maamuzi vya Chama. Kikao cha
Kamati Ndogo ya Maadili kitafanyika tarehe 19/01/2015 kwa ajili ya utekelezaji
wa agizo hilo.
2. WALIOPEWA ADHABU KWA KUKIUKA MAADILI YA CHAMA.
Itakumbukwa kuna makada sita wa CCM walipewa adhabu kwa
kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM
kugombea urais, watamaliza muda wa adhabu zao mwezi wa pili mwaka 2015.
Baada ya muda wa adhabu zao kuisha, itafanyika tathimini
kuona kama walizingatia mashariti ya adhabu zao. Na kama kuna ambao watakutwa
hawakuzingatia mashariti ya adhabu zao wataongezewa adhabu.
3. SOKO LA MAHINDI.
Kamati Kuu imepokea taarifa ya mwenendo wa soko la mahindi
nchini. Baada ya tathimini na uchambuzi, pamoja na kazi iliyofanywa na
serikali, Kamati Kuu imeiagiza serikali kuangalia upya mfumo unaotumiwa na Hifadhi
ya Taifa ya Chakula ( NFRA)katika ununuzi wa mahindi, ili unufaishe zaidi
wakulima badala ya utaratibu wa sasa ambao kwa kiasi kikubwa unanufaisha zaidi
mawakala badala ya wakulima moja kwa moja.
4. RATIBA YA VIKAO VYA CHAMA.
Kamati Kuu imepitisha ratiba ya shughuli mbalimbali za Chama
kwa mwaka 2015.Aidha ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM ndani ya
dola utapangwa na vikao vijavyo vya Chama.
Nape Moses Nnauye
CCM Secretary for Ideology & Publicity.
No comments:
Post a Comment