KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mkazi wa mjini Namanyere
wilayani hapa mkoa wa Rukwa, Gilbert Paul (37) aliyejiandalia maziko yake miaka
14 iliyopita, bado yu hai.
Kwa sasa mtu huyo ameanza maandalizi ya kuchimba na kujenga
kaburi la gharama, ikiwa ni pamoja na kununua jeneza.
Paul, baba ya mtoto mmoja na mchoraji maarufu mjini
Namanyere aliyehitimu Kidato cha Nne 2001 katika Shule ya Sekondari Nkasi,
anasema anafanya hivyo kwa kuwa ana amani maisha ya duniani yana ukomo wake na
ni ya kupita tu.
Aliyasema hayo juzi, akithibitisha kujichongea
msalaba
mkubwa na kuutundika kwenye paa la kibanda chake anamofanyia kazi zake katika
Mtaa wa Sasala.
Msalaba huo mweupe mkubwa, umeandikwa tarehe aliyozaliwa ya
Desemba 24, 1977, lakini katika tarehe ya kufa, ameweka alama ya kiulizo.
Msalaba huo unaonekana waziwazi, kiasi cha wageni wanaopita eneo hilo, kudhani
ni nyumba ya ibada.
Paul alisisitiza kuwa msalaba huo uliofikisha miaka 14 sasa,
ndio utakaosimikwa katika kaburi lake, ambalo anatarajia kulichimba na
kulijengea, akikadiria litamgharimu Sh milioni moja, sawa na gharama ya jeneza
alilotarajia kulinunua.
“Nilipotafuta mafundi wanitengenezee msalaba huu, wote
waligoma wakidai ni uchuro na hawajawahi kusikia wala kuona mtu akijifanyia
maandalizi yake ya maziko akiwa bado anaishi . “Mama alilia sana walipomtaarifu,
akidai katika ukoo wa baba yangu na wa kwake hakuna aliyewahi kufanya hivyo
…Baba alifariki nikiwa na miaka saba, mwanzoni watu walidhani nina tatizo la
akili na wengine waliamini nimeathirika kwa Ukimwi hivyo nimekata tamaa ya
kuishi, lakini sivyo…“ anasema.
Alieleza kuwa katika maisha yake yote, hakuwahi kuwa na
rafiki wa kike mjini humo kutokana na kujitengenezea msalaba huo, unaomfanya
wamuogope sana, hadi kuona kuna ulazima wa yeye kwenda kijiji cha mbali na hapo
.
“Nilichumbia na kuoa chapuchapu nikihofia mke wangu
mtarajiwa akibaini nimejitengenezea msalaba hatanikubali,“ alieleza.
Mke wa Paul, Paskaria Salvatory (25) akizungumzia tukio
hilo, anasema kama angefahamu, kamwe asingekubali kuolewa naye.
“Si kawaida mtu kujitayarishia maziko yake mwenyewe akiwa
hai. Nilibaini mwezi mmoja baada ya kuolewa, kwa kweli nilishituka sana, pia
wanawake wenzangu walikuwa wakinibeza na kuniita kwa majina ya kuudhi, lakini
sasa nimezoea na nimezaa naye mtoto mmoja mwenye umri wa miaka miwili. Mume
wangu ana akili timamu, ni mwenye huruma na anayejali familia“, alibainisha.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment