Dar es Salaam. Matukio ya wasafiri kukamatwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa na nyara za Serikali na dawa
za kulevya, yanazidi kuchukua sura mpya baada ya raia mmoja wa Ubelgiji
kukamatwa akiwa na fuvu la binadamu.
Raia huyo, Balcjan Christine Weejktgns (49),
alikamatwa Jumatatu saa 2.30 usiku wakati akiwa katika taratibu za
kuingia uwanjani hapo tayari kwa safari ya kuelekea Ubelgiji kupitia
Zurich, Uswisi.
Tukio la kukamatwa kwa Mbelgiji huyo ni mwendelezo
wa matukio ya aina yake uwanjani hapo baada ya
watu wengine wawili kukamatwa kwa nyakati tofauti kwenye uwanja huo wakiwa na kucha za simba na kenge walio hai.
watu wengine wawili kukamatwa kwa nyakati tofauti kwenye uwanja huo wakiwa na kucha za simba na kenge walio hai.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Hamisi
Selemani alisema mtu huyo alikutwa ameficha fuvu hilo la binadamu kwenye
mfuko wa plastiki.
“Alivyopita kwenye mashine za ukaguzi tulimtilia
shaka na tulipompekua tulimkuta amebeba fuvu la kichwa cha binadamu
kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa plastiki ndani ya sanduku alimokuwa
ameweka nguo zake na vitu mbalimbali,” alisema Selemani.
Raia huyo anadaiwa kuwa ni mkazi wa Chuo Kikuu cha
Kilimo (SUA) mkoani Morogoro na inadaiwa kuwa alikuwa nchini kwa ajili
ya kufanya utafiti.
Kamanda Selemani alisema baada ya askari wa kikosi
cha polisi cha JNIA kumhoji kwa undani madhumuni ya kubeba fuvu,
alisema ni mali yake na kuwa alikuja nalo nchini kutoka Ubelgiji.
“Kwa maelezo yake alidai kuwa fuvu hilo
analimiliki muda mrefu tangu alipoingia nchini mwaka 2000 akitokea
Ubelgiji akidai kuwa yeye ni mtafiti,” alisema.
Pamoja na raia huyo wa Ubelgiji kujitetea kuwa ni
mtafiti, Kamanda Selemani alisema sheria za nchi haziruhusu mtu kumiliki
viungo vya binadamu hivyo anayekiuka lazima akamatwe na kuchukuliwa
hatua za kisheria.
“Jeshi la polisi haliwezi kuona taratibu za nchi
zikivunjwa hata kama ni raia wa kutoka nje ya nchi ambaye amekuja
kufanya utafiti nchini. Lazima afuate sheria,” alisema na kuongeza:
“Wito wangu ni kwamba watu wote wanatakiwa kufuata
taratibu za nchi. Huyu raia ameona kitu cha kawaida kuishi na fuvu la
kichwa, lakini hapa ni tofauti na nchini kwao,” alisema.
Alisema polisi inaendelea na upelelezi ili kujua
sababu ya Mbelgiji huyo kusafirisha fuvu hilo na kuahidi kuwa uchunguzi
ukikamilika, atafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment