EXCLUSIVE! Kile kisa cha mtalaka wa mwimba taarab mahiri
Bongo, Aisha Ramadhani Nkongo ‘Isha Mashauzi’, Jumanne Hassan ‘Tevez’ kuteswa
na kudhalilishwa nchini Afrika Kusini kisa kikidaiwa ni kudhulumu mzigo wa
wafanyabiashara wenzake kimeingia awamu nyingine!
Majeraha ya mgongoni aliyopata, Jumanne Hassan ‘Tevez’
wakati wa kuteswa.
Kwa mara ya kwanza Gazeti Pendwa la Amani Tanzania limeweza
kuzungumza na Tevez kwa dakika arobaini na tano kutokea nchini humo ambako anauguza
majeraha.
KWANZA SIKU YA TUKIO
Kabla Tevez hajasimulia kilichompata na hali yake kwa sasa,
ni muhimu kukumbuka kuwa, tukio hilo
ambalo lilikuwa habari ya Jiji la Dar es
Salaam, lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo picha zake zilizagaa zikimuonesha
akiwa amefungwa kamba huku mwili wake ukiwa umetapakaa damu na majeraha kadhaa.
AMANI LAMSAKA
Kwa vile habari za tukio hilo ziliandikwa na baadhi ya
vyombo vya habari bila kupata balansi (uwiano) na Tevez mwenyewe, Amani
liliingia kazini kumsaka mhanga huyo usiku na mchana.
MSIKIE SASA
Akizungumza kwa hisia kali na gazeti hili juzi, Februari 3,
mwaka huu kutoka Mji wa Durban, Afrika Kusini, Tevez alisema:
“Kusema ukweli tukio lililonikuta watu huko nyumbani (Bongo)
wanalitafsiri tofauti sana. Nimesikia kwamba wanasema eti nilidhulumu mzigo wa
mtu, ndiyo maana niliteswa! Si kweli.”
‘Tevez’ akiwa salama nyumbani kwake.
UKWELI NI UPI?
“Ishu iko hivi, mwenyeji wangu hapa Durban, anaitwa Ibra,
ndiye ambaye alinipokea siku nilipotua hapa.
“Huyu bwana inaonekana
ni tamaa. Aliniundia njama, aliita wenzake na kuniteka kisha kunitesa
sana wakidhani nina pesa nyingi.
“Niliteswa sana kwa kweli. Kama mlivyoona picha.
Nilidhalilishwa sana, lakini katika yote ukweli sijadhulumu mzigo wa mtu.”
ULICHOPOTEZA KATIKA UTESWAJI
“Katika mateso yangu,
walifanikiwa kunipora Dola za Marekani elfu 14 (kama shilingi milioni 22) na
Randi za Afrika Kusini elfu 3 (shilingi 480,000) zikiwemo simu zangu mbili aina
ya Samsung na Nokia ambazo nilikuwa nazitumia sana kuwasiliana na watu wangu
muhimu.”
HAIKUWA KAZI RAHISI
Tevez akazungumzia jinsi jamaa walivyomkamata: “Jamaa siku
wananiteka usiku kiukweli nilipambana nao sana hadi wanafikia hatua ya kunizidi
nguvu na kunifunga kamba. Nilikuwa nimewachapa kwelikweli ila kwa vile walikuwa
wengi na walikuwa wakitumia silaha nilijikuta nikiishiwa nguvu baada ya
kunipiga na kitu kizito kichwani nikapoteza fahamu, nilipojitambua ndiyo
nikakuta wamenifunga kamba.”
KINACHOKUUMA NINI?
“Tukio linaloniuma zaidi ni yule jamaa ambaye anaonekana
katika picha amekaa jirani na mimi, hana shati. Alinichoma pasi mgongoni,
namchukia sana lakini nimemwachia Mungu.”
‘Tevez’ akiwa na mwanaye.
KUHUSU KUKATWA NYETI, KUFANYIWA KITU MBAYA
Tevez: “Nasikia watu huko Tanzania wanazusha eti nimekatwa
nyeti, si kweli kabisa. Mimi nimepigwa na kuchomwa pasi wala hakuna kitu kama
hicho zaidi ya kunichoma na pasi.
“Nimesikia wengine wanasema nimetobolewa macho, huo ni
uzushi wa watu tu! Mimi niko safi na hali yangu ya kiafya inaendelea vizuri.”
SABA WAMEKAMATWA
Tevez tena: “Nashukuru sana serikali ya huku wameweza
kunisaidia kwani mpaka sasa ninapoongea na wewe Musa Mateja hawa jamaa
wamekamatwa saba.
“Jana (Jumatatu) walifikishwa mahakamani na kusomewa
mashitaka ya kunishambulia na kupora fedha. Wanatarajiwa kurejea tena
mahakamani baada ya siku 7, ingawa nimeambiwa kesho (jana Jumatano) wataletwa
Polisi Central ya huku kwa ajili ya mimi kuwatambua zaidi.”
BONGO LINI TEVEZ?
“Bongo natarajia kurudi Alhamisi (leo) au Ijumaa (kesho)
kama mambo yangu yatakuwa kwenye mstari ila pia sasa hivi natarajia kuwasiliana
na balozi wetu ili nijue kama ana taarifa zangu na namna ambavyo ataweza
kunisaidia kama kiongozi wangu.”
HALI YAKO KWA SASA
“Kusema ukweli naendelea vizuri ni majeraha tu ambayo hata
hivyo yanakauka. Ila hili la pasi mgongoni ndiyo linasumbua kwa mbali, lakini naamini litakaa
sawasawa.”
No comments:
Post a Comment