Wiki mbili zilizopita katika mechi za ligi kuu kulitokea
matukio mawili ambayo yalileta mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka
nchini.
Mchezaji wa Azam FC Aggrey Morris alipiga kiwiko Emmanuel Okwi katika mechi iliyowakutanisha Simba vs Mtibwa – kitendo ambacho kilipelekea Okwi kuzimia uwanjani na kupelekwa hospitali – kitendo kingine kilikuwa
kikimhusisha mchezaji wa Mbeya City Juma Nyosso ambaye alionekana akimshika makalio mchezaji wa Simba Elias Maguri.
Baada ya mjadala mkubwa kwenye magazeti na mitandaoni hatimaye leo hii Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imewafungia kati ya mechi tatu na nane wachezaji Juma Nyoso wa Mbeya City
na Aggrey Morris wa Azam kutokana na makosa ya kinidhamu waliyoyafanya
wakiwa uwanjani.
Nyoso ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumfanyia vitendo vya udhalilishaji
mshambuliaji Elias Maguri wa Simba amefungiwa mechi nane za Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL). Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 57 na Ibara ya
11 (f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
Akiwa mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 5 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam, Nyoso alikiri kufanya na kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi
mchezaji Maguri kwa kitendo hicho.
Akisoma uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa
alisema kitendo kilichofanywa na Nyoso ni kosa kubwa, kudhalilisha utu wa
mtu, na ni mfano mbaya kwa watoto na jamii nzima ya mpira wa miguu.
Naye Morris amefungiwa mechi tatu za VPL baada ya kutiwa hatiani kwa
kumpiga mshambuliaji Emmanuel Okwi wakati timu hizo zilipopambana kwenye
mechi ya ligi iliyochezwa Januari 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Kabla ya kusoma uamuzi, Wakili Msemwa alisema mlalamikiwa Morris alikiri
kugongana na Okwi, kwa maelezo kuwa aliingia kwenye ‘reli’ ndiyo ukatokea
mgongano huo.
Kamati baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Simba, ripoti za Brain CT
scan kutoka Besta Diagnostic Centre na nyingine kutoka Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (MOI), taarifa za madaktari zilionyesha Okwi aligongwa kichwani
akiwa anacheza mpira na kuzimia kwa dakika tano, pia mkanda wa video
uliowasilishwa na TFF imeona kulikuwa na kugongana kati ya wachezaji hao.
Hivyo, Kamati ikamtia hatiani Morris kwa kutumia Ibara ya 48(1)(d) ya
Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012 kwa kumfungia mechi hizo tatu na
kumpa onyo kali.
No comments:
Post a Comment