Kaisi Bin Abdullah akiwa amejiziba sura. |
HATIMAYE kuvamiwa kwa vituo vya polisi na kuporwa silaha
huku askari wake wakiuawa kikatili kumejulikana kunafanywa na nani kufuatia
gazeti hili kunasa mkanda wa video wa mtu mmoja anayejiita Kaisi Bin Abdullah
akijitapa kufanya hivyo kwa lengo la kukusanya silaha ili kulipa kisasi siku si
nyingi!
Ijumaa liliunasa mkanda huo kutoka kwa mtu mmoja aliyekataa
kujitambulisha kwa jina wala kusema anakotokea hapa nchini huku akisema: “Una
maneno ya hatari sana, naogopa kujianika, nitauawa.”
“Siwezi kutaja jina wala mahali ninapoishi, sitaki kupigwa
picha, kama hamtaki niwapatie taarifa hii acheni niondoke,” alisema mtu huyo
huku akinyanyuka kitini jambo lililowafanya wakuu wa dawati kukubaliana na
matakwa yake na kuendelea na mahojiano.
Baadaye ilipatikana fursa ya kuuangalia mkanda huo; Bin
Abdullah ametumia dakika 11: 03 kuzungumzia mambo mbalimbali lakini kubwa
kuliko yote ni kuliponda Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuwakamata wenzao katika
imani na harakati (zinazohifadhiwa kwa sasa) na kuwashikilia kwenye mahabusu
mbalimbali nchini.
ALIANZA KWA KUSEMA
Bin Abullah ambaye kwenye mkanda huo amevaa nguo nyeusi kama
ninja na miwani ya giza, alizungumza kwa kirefu, akitoa wito lakini mbele
akasema:
“Tumeshaungana ili kupambana. Mkoa wa Mtwara zaidi ya
wenzetu kumi na saba walikamatwa kwa makosa ya dhuluma, makosa ya kupanga,
makosa ya ugaidi. Ishirini na moja wamekamatwa Zanzibar wako katika Gereza la
Segerea (Dar). Wenzetu wengine kumi na nane wamekamatwa Mwanza wako katika
Gereza la Kisongo, Arusha. Ndugu zangu, wenzetu wengine kumi na saba wameuawa
Mtwara kwa amri ya ...(anamtaja waziri).”
ADAI WAMECHOKA NA SUBIRA
“Subira yetu imefika mwisho na tulichokuwa tunasubiri Mungu
ameshatupa. Tunatoa ahadi kilichopo hivi sasa tunatoboa jahazi wote tuzame.”
WENZAO WAACHIWE HURU
“Tunatoa rai, wenzetu waliopo Gereza la Kisongo waachiwe
huru. Hapa hatumtishi mtu yeyote yule.”
KUHUSU VITUO VYA POLISI
“Pili, agizo la Ernest Mangu IGP, umetangaza uliwenguni
kwamba umewakamata wote waliovamia vituo vya polisi na umezikamata silaha zote.
Ukweli ni kwamba unatetea tumbo lako. Hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa na
wala silaha hazijakamatwa.
“Mungu ametukubali. Katika Kituo cha Polisi Ushirombo
(Kilimanjaro) tumeweza kuvamia kituo, tukaweza kutoa roho za polisi na tukaweza
kuchukua silaha, tunazo.“Tumevamia Kituo cha Polisi Ikwiriri (Pwani), tumeweza
kuchukua silaha za kutosha, tumeweza kuchukua mabomu ya kutosha. Tunazo silaha
tunasubiri muda zianze kufanya kazi.
“Ernest Mangu nakupa changamogto, hivi sasa tuna
uwezo...(maneno yanahifadhiwa kwa usalama) wakati wowote ambao tunataka.”
HAKUNA UPINZANI?
“Tumeweza kuchukua silaha bila kuwa na silaha yoyote. Ndugu
zetu wa Tanga wameweza kuchukua silaha wakiwa hawana silaha yoyote. Ikwiriri
tumechukua silaha tukiwa hatuna silaha yoyote, mpaka sasa tumeshachukua roho
tano za polisi.”
VITISHO VYA JUMLA
“Ndugu zangu, ...mlikuwa mkinisubiri nitoe tamko, natoa
kauli rasmi...” alihitimisha Abdullah, huku vitisho vya jumla kwenye tamko lake
vikiwahusu polisi, viongozi wa ngazi za juu serikalini pamoja na mikusanyiko ya
ibada.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu.
TAMKO NGUNGURI LA IGP
Baada ya video hiyo, Ijumaa lilimuibukia Mkuu wa Jeshi la
Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu na kuzungumza naye kuhusu mtu huyo na
kumkabidhi video ambapo alisema:
“Nawashukuru sana kwa kuleta video hii, huu ndiyo
ushirikiano unaotakiwa, nawaomba wananchi video za aina hii wazikatae kwa
sababu ni kosa kuwa nazo na watu kadhaa wameshakamatwa kwa kuwa nazo.
“Sisi kama jeshi la polisi tunajua kuwa kuna watu wanadhani
kufanya uhalifu kama huo kutawasaidia kutimiza matakwa yao, lakini ukweli ni
kwamba polisi wapo imara na nina uhakika watuhumiwa watakamatwa kwa
kushirikiana na raia wema.”
SHEHE MKUU AMKANA
Baada ya kuzungumza na IGP, Ijumaa lilimtafuta Shehe Mkuu
Tanzania, Mufti Shaban Simba na kumsimulia kuhusu kuibuka kwa Bin Abullah na
kutaka kujua pengine anamfahamu.
“Kwanza hizo taarifa hizo ndiyo nazisikia kutoka kwako. Hilo
jina ulilonitajia (Bin Abdullah) sijawahi kulisikia labda muangalie kwa wenzetu
upande wa pili.”
KUMBUKUMBU ZA NYUMA
Katika gazeti ndugu na hili, Uwazi, Toleo la Januari 28
mpaka Februari 2, mwaka huu ukurasa wake wa mbele kulikuwa na habari yenye
kichwa; KUUAWA KWA POLISI IKWIRIRI; MAZITO YAIBUKA!
Katika habari hiyo, Uwazi lilichimba kwa kina kuhusu
kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi Ikwiriri na kuuawa kwa askari wake wawili, Edger
Jerald Mlinga (43) na Judith Timothy (32).
Watu hao waliodhaniwa ni majambazi walifanikiwa kupora
bunduki 7, risasi 60 na mabomu kadhaa yaliyokuwa ndani ya kituo na kukimbia
bila kukamatwa.
Baadhi ya watu waliozungumza na Uwazi kwenye eneo la tukio
walisema wana wasiwasi watu hao si majambazi bali ni kundi la kigaidi ambalo
lina mkakati wa kukusanya silaha kwa ajili ya matumizi batili siku za baadaye,
jambo ambalo limeanza kujionesha kupitia video iliyonaswa na Gazeti na Ijumaa.
KUTOKA DAWATI LA IJUMAA
Tunawaomba wananchi kwa ujumla kutokuwapa nafasi watu wa
aina ya Abdullah wanaoeneza chuki kwa lengo la kuwagawa watu na kuleta
machafuko, badala yake kila anayeashiria shari ni vema taarifa zake
zikafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili amani ya taifa iendelee kudumu.
Aidha, tunalitaka jeshi la polisi pamoja na vyombo vya
usalama kulichukulia kwa uzito tamko la mtu huyo anayedai kuwa ni kiongozi wa
ugaidi, kumsaka na kumtia hatiani pamoja na wafuasi wake wote.CHANZO GAZETI LA IJUMAA
No comments:
Post a Comment