Marehemu Robert John Mpwata (34) enzi za uhai wake.
Na Makongoro Oging’, Issa Mnally/Uwazi
MTU mmoja anayeaminika kuwa ni Mtanzania, Robert John Mpwata
(34) anadaiwa kuuawa kwa kuwekewa sumu na mwili wake kukutwa chumbani kwake
katika Mji wa Shorten nchini Ujerumani siku chache zilizopita.
Habari kutoka kwa baadhi ya marafiki zake waliopo huko,
zinasema Robert aliyekuwa mwanamichezo aliyecheza sarakasi, karate na judo,
aliwasiliana nao kwa njia ya simu mara kwa mara na walipata taarifa za kifo
chake siku saba ya kufariki dunia.
Inadaiwa kabla ya kifo cha mwanamichezo huyo, alikuwa
akiwasiliana vizuri na wenzake, lakini umauti wa ghafla uliomkuta na mazingira
yake, unawapa hofu kuwa huenda alifariki baada ya kuwekewa sumu.
Inadaiwa kuwa Februari 8, mwaka huu ilikuwa ni siku
waliyotakiwa kufanya onyesho, kitu ambacho kiiwafanya wawe na mawasiliano ya
mara kwa mara.
Mwandishi wa habari hii aliwasiliana na ubalozi wa Tanzania
nchini Ujerumani, ambako mfanyakazi mmoja aliyekataa kutajwa jina lake kwa vile
siyo msemaji, alikiri kusikia taarifa hizo, lakini akasema inakuwa vigumu kwao
kutoa msaada kwa vile taarifa isiyo rasmi inasema marehemu alikutwa na
vielelezo vinavyomtambulisha kuwa ni mtu wa Somalia.
Robert John Mpwata akiwa na mke wake.
Naye Mwenyekiti wa umoja wa Watanzania nchini humo, Mfundo
Peter Mfundo alikiri kutokea kwa kifo hicho, kwani awali marehemu aliwaaga
Watanzania wenzake kuwa ataondoka kwenda nyumbani kwa mke wake.
“Mimi nilipata taarifa kutoka kwa rafiki yake wa
karibu
baada ya wiki mbili tangu akutwe amefariki, hakuna anayejua kilichomuua maana
serikali bado haijatoa majibu. “Mpaka sasa bado tunasubiri kutatokea nini na
hata kama ikitokea tupewe maiti kuisafirisha ni kazi kwani ni zaidi ya shilingi
milioni 12, nimewasiliana na baba yake anasema hana nauli ya kumleta huko.
“Robert alikuja hapa katika shughuli za sanaa na alimuoa
Mjerumani aliyezaa naye mtoto Daniel ambaye ana umri wa miezi minne,” alisema
kiongozi huyo.Kwa mujibu wa Peter, mke wa marehemu aliwaambia kwamba angependa
amzike mumewe nchini humo ili iwe rahisi kwa mtoto wake kuhani kaburi lake.
Ndugu zake marehemu Robert John Mpwata wakiwa Bongo, (mwenye
shati jekundu ni baba yake).
John Mpwata (65), baba mzazi wa marehemu akiwa nyumbani
kwake Manzese Kilimahewa jijini Dar, alisema taarifa za kifo hicho
zimemuumiza.“Mwanangu aliondoka mwaka 2007 kutafuta maisha huko Ujerumani na
kwa mara ya mwisho niliongea naye Desemba 22, mwaka jana, aliniambia atakuja nyumbani
na mkewe Mzungu hivi karibuni baada ya mwanaye Daniel kuanza kutembea.
“Lakini cha kushangaza hivi karibuni nimepata taarifa ya
kifo chake, sina jinsi maana nimeambiwa uwezekano wa mwili kuletwa ni mdogo na
ningependa kwenda kumzika lakini sina milioni 2.5 za nauli, ninawaomba
Watanzania wanisaidie nikamzike mwanangu,”
No comments:
Post a Comment