Pages

Monday, February 23, 2015

Maji ya mimba yakiingia kwenye mfumo wa damu humuua mama


Vifo vinavyotokana na uzazi kwa akinamama wakati wa kujifungua ni jambo lenye historia ndefu. Kitabu cha kale zaidi cha historia ya binadamu kinasimulia kisa cha kifo cha Raheli mke wa Yakobo kilichotokana na uzazi alipokuwa anajifungua mtoto wake wa kiume, Benjamini, zaidi ya miaka 6,000 iliyopita (Mwanzo 35:16).
Zaidi ya wanawake 600,000 duniani kote, hufariki dunia kila mwaka kutokana na matatizo ya mimba na kujifungua. Bara la Afrika pekee linachangia katika mzigo wa vifo vya wajawazito duniani kwa asilimia 



50, ingawa linachangia kwa asilimia 20 pekee katika idadi ya vizazi duniani. Hii ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa hospitali ya Massana na Chuo cha Uuguzi, Profesa R.S. Lema katika mada yake aliyoiwasilisha katika mkutano wa wanasayansi uliondaliwa na APHFTA jijini Dar es Salaam mwaka 2013.
Chanzo kimoja cha habari kinaeleza kuwa takwimu za hivi karibuni nchini zinaonyesha kwamba, Tanzania inapoteza kinamama 7,900 kutokana na sababu zitokanazo na ujauzito. Idadi hiyo ni sawa na vifo 22 kwa siku.
Pamoja na sababu nyingi mbalimbali, vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua vinaweza kutokea baada ya maji ya mimba yajulikanayo kama ‘amnioni,’ kuingia kwa bahati mbaya katika mfumo wa damu ya mama anayejifungua.
Tatizo hili lijulikanalo kama Amniotic Fluid Embolism. Kwa mara ya kwanza katika historia ya tiba, lilihusishwa na kusababisha hatari kwa wajawazito mwaka 1926, wakati Ricardo Meyer alipolifafanua.
Athari zake kwa uhai wa wajawazito lilifafanuliwa vizuri zaidi mnamo mwaka 1941 na Dk Paul E. Steiner pamoja na C.C. Lushbaugh.
Tatizo hili ingawa hutokea mara chache sana, ni kubwa na linaloweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya au kupoteza maisha ya mama anayejifungua kwa haraka.
Baadhi ya wataalamu na wachunguzi wa masuala ya afya ya uzazi, wanakadiria kuwa tatizo hili linashika namba ya tano katika vyanzo vya vifo vya wanawake wakati wa kujifungua duniani kote.
Watafiti N.J. McDonnell, V. Percival na M.J. Paech wanaamini kuwa tatizo hili ndilo linaloongoza kwa vifo vya kinamama wakati wa kujifungua. Hii ni kwa mujibu wa utafiti wao uliochapishwa katika jarida la afya lijulikanalo kama International Journal of Obstetric Anaesthesia toleo la mwaka 2013. Katika utafiti wao, A. Conde-Agudelo na R. Romero uliochapishwa katika jarida la magonjwa ya kinamama (American Journal of Obstetrics and Gynecology) toleo la 201(5) la mwaka 2009, walibaini kuwa tatizo hili humpata mwanamke mmoja kati ya kila wanawake 15,200 huko Amerika ya Kaskazini na mwanamke mmoja kwa kila wanawake 53,800 wanaojifungua huko Ulaya.
Tatifi kadhaa zinaonyesha kuwa tatizo hili ni miongoni mwa vyanzo vinavyoongoza kusababisha vifo vya wanawake wakati wa kujifungua nchini Marekani na kwamba husababisha takribani asilimia 10 ya vifo vyote vya kinamama wakati wa kujifungua katika nchi zilizoendelea.
Dk Michael D. Benson wa Kitivo cha Magonjwa ya Wanawake cha Chuo Kikuu cha Northwestern, nchini Marekani anasema, katika makala yake iliyochapishwa katika Jarida la Clinical and Developmental Immunology toleo la mwaka 2012, kuwa wachunguzi wengine wanaamini kuwa tatizo hili ni kubwa kiasi cha kusababisha kifo kimoja kwa kila wanawake 600 wanaojifungua.
Maji ya mimba yanapoingia katika mfumo wa damu, husafirishwa na mishipa ya damu hadi kwenye moyo na katika mapafu na kusababisha mzio hatarishi ambao humfanya mzazi kushindwa kupumua na moyo hushindwa kufanya kazi.

No comments:

Post a Comment