Veronica Romwald na Mwajuma Mazao, Dar es Salaam
HATIMAYE mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Emmanuel
Mbasha, ameibuka na kuweka wazi suala la mgogoro wa mtoto na mkewe Flora
Mbasha.
Hatua hiyo imekuja miezi saba tangu wawili hao walipoingia
katika mgogoro wa ndoa yao hali iliyosababisha Mbasha kufikishwa mahakamani kwa
kosa la ubakaji.
Hivi karibuni, picha za mtoto mchanga zilisambazwa
katika
mitandao ya kijamii na kudaiwa kuwa ni wa Flora aliyezaa na Mchungaji Kiongozi
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana
baada ya kuahirishwa kwa kesi ya ubakaji inayomkabili katika Mahakama ya Ilala,
Mbasha alisema hayupo tayari kuzungumzia kuzaliwa kwa mtoto huyo, ila anayeweza
kueleza ukweli kuhusu baba wa mtoto ni Flora mwenyewe.
Alipoulizwa kwanini anashindwa kueleza suala hilo la mtoto
hali ya kuwa Flora bado ni mke wake kwa mujibu wa sheria, alisisitiza kuwa
hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa.
“Siwezi kuongea chochote, ukweli wote anaujua Flora nendeni
mkamfuate atawaeleza, na sijaongea na gazeti lolote kuhusu mtoto huyo… kwa sasa
sipo tayari kusema lolote,” alisema Mbasha.
Februari 10, mwaka huu gazeti hili lilimtafuta Flora kwa
njia ya simu ili kuzungumzia suala hilo ambapo alisema: “Siko tayari kuzungumza
lolote kuhusu Mbasha kwa sasa. Yeye ana jeuri ya pesa ndiyo maana anafanya haya
yote, lakini mimi ninasimama na Mungu wangu na ninajua Mungu atanipigania.”
Alipoulizwa kuhusu hali ya mtoto wake mchanga, alisema:
“Mtoto hajambo, lakini mtoto anayesambazwa kwenye mitandao siyo wangu, na hizo
picha nyingine nafikiri ni za kutengeneza tu.”
Kutokana na kuzagaa taarifa za picha za mtoto huyo ambaye
anadaiwa kuwa amezaa na Flora, Mchungaji Gwajima, alisema taarifa hizo ni za
uzushi na huenda zinasambazwa na Mbasha.
Mchungaji Gwajima alikwenda mbali na kusema pamoja na uzushi
huo unaosambazwa dhidi yake kwa kuhusishwa katika uhusiano na Flora, anamwachia
Mungu kila kitu.
“Si unajua hiyo issue (suala, jambo) ya Mbasha ni ya muda
mrefu tu. Wakati mwingine mimi huwa sijibu ujinga.
“Awali niliwaza kuwashtaki (alipoanza kuhusishwa kwamba ana
uhusiano na Flora) wanaoeneza uzushi huo, lakini nikaona ‘It doesn’t hold
water’ (haina mashiko), najua shutuma hizo zinatoka wapi,” alisema Mchungaji
Gwajima.
Alipoulizwa kuhusu mtu anayemshuku kueneza uvumi huo
alisema: “Probably’ (nadhani) atakuwa Emmanuel Mbasha mwenyewe. Tangu mwanzo
alipotuhumiwa kumbaka shemeji yake na kutoroka akihofia kukamatwa na polisi,
mkewe alikuja kanisani kwetu na mimi nilimwagiza mwenyekiti wa kusaidia jamii
amsaidie.
“Sasa Mbasha alipotoka huko alikokimbilia na kusikia kuwa
mkewe yuko hapa kanisani, ndipo alipoanza kueneza uzushi,” alisema.
Gwajima alisisitiza kuwa Flora hakufikia kwake kwa jambo
lolote bali aliendelea kuishi katika nyumba aliyopanga.
Alipoulizwa kwanini hamshtaki Mbasha ili kulinda heshima
yake, alisema ameshawaita ndugu zake akiwamo baba yake mzazi, lakini nao
wakaonekana kutommudu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya kituo cha
televisheni ya East Africa (EATV), Agosti 27, mwaka jana Flora alihojiwa na
kituo hicho kupitia kipindi cha Kikaangoni Live, kinachoendeshwa kwa njia ya
mtandao wa kijamii wa Facebook na kusema ujauzito aliokuwa nao ni wa mumewe
Mbasha na si Mchungaji Gwajima.
Alisema hawezi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mchungaji
Gwajima kwa kuwa ni mjomba wake, na kwamba watu wamekuwa wakizusha kwa lengo la
kumchafua na kumshushia hadhi.
No comments:
Post a Comment