Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai, Mkoani
Kilimanjaro, imepanga kuanza kusikiliza utetezi wa Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (pichani), Februari
27, Ijumaa, baada ya kiongozi huyo kushindwa kufika mahakamani hapo
jana kujitetea kama ilivyokuwa imepangwa.
Mbowe anakabiliwa na kesi ya kumshambulia mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Nasir Yamin, Jimbo la Hai.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alitakiwa kujitetea mahakamani hapo
jana, lakini alishindwa kufanya hivyo, kutokana na kuhudhuria uzinduzi
wa uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa
njia ya mfumo wa mashine za kielekroniki (BVR).
Akitoa sababu za Mbowe kutofika mahakamani hapo jana mbele ya
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Denis Mpelembwa, wakili Issa
Rajab, alisema mteja wake huyo hakuweza kufika mahakamani kwa ajili ya
kujitetea kwa sababu kwa nafasi yake amealikwa kuhudhuria uzinduzi huo.
“Kwa hiyo mheshimiwa hakimu tunaomba tarehe nyingine ambayo mteja
wetu atatakiwa kufikia kwa ajili ya kujitetea,” alisema wakili huyo.
Aidha, Wakili Rajab alidai kuwa shahidi muhimu wa Mbowe, Clement
Kwayu, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, naye
hakuweza kufika mahakamani hapo kutokana na dharura ambayo hata hivyo
hakuieleza mahakama hapo. Baada ya ombi hilo la upande wa utetezi,
Hakimu Mpelembwa, alimtaka mdhamini wa Mbowe, Awazi Uronu kuhakikisha
mshtakiwa anafika mahakamani hapo tarehe iliyopangwa bila kukosa, kwa
kuwa kesi hiyo imechukua muda mrefu kumalizika huku kila upande ukitaka
haki itendeke.
Katika kesi hiyo, Mbowe anadaiwa kumshambulia kwa kipigo mwangalizi
huyo, Nassir Yamin, katika kijiji cha Nshara, kata ya Machame Kusini,
wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment