Mrisho Ngassa
Na Richard Bakana, Dar es salaam
MSHAMBULIAJI wa klabu ya Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania,
Taifa Stars, Mrisho Ngassa, amejutia uamuzi wake wa kukataa kujiunga na El
Merreikh ya Sudan akisema kuwa yalikuwa ni mapenzi yake makubwa kuichezea
Yanga.
Akiongea na Shaffihdauda.com baada ya mchezo wa jana
alipoibuka shujaa kwa kuifungia Yanga bao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, Ngassa
alisema kuwa baada ya kugundua alifanya makosa makubwa kuwagomea Simba na Azam
FC ambao ndio walitaka kumpeleka El Merreikh, alipofunga mabao hayo alilazimika
kuwaomba msamaha mashabiki kwa uamuzi ambao sasa anaujutia.
“Nilifanya makosa kutokwenda El Merreikh ndio maana hata leo
nilipofunga magoli ilibidi niombe msamaha kwa sababu Simba na Azam walitaka
kunipeleka El Merreikh, Nilifanya kama kuwakosea na kwasababu nilikuwa naipenda
Yanga ilibidi niichezee” Amesema Ngassa kwa hari ya uchungu ajijuta kosa
alilofanya katika maisha yake la kukataa kwenda kucheza mpira wa kulipwa nchini
Sudan.
Katika msimu wa 2013/2014 Ngassa alijiunga na Yanga akitokea
Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo akiwa ni mali ya Azam FC, Katika uamisho huo
TFF iliamuru awalipe Simba kiasi cha Tsh. Milioni 30 kama pesa ambayo
walimsajilia kutoka Azam FC pamoja na Tsh. Milioni 15 kama fidia baada ya
kugundulika alikuwa amesajiliwa timu mbili zaidi ya hapo TFF ilikuwa imepanga
kumfungia endapo asingelipa deni hilo.
Kufatia Yanga kuonyesha nia ya dhati ya kutaka huduma ya
kiungo huyo ambaye amewahi kufanya majaribio kunako klabu ya West Ham ya
Uingereza, Uongozi wa Mwenyekiti Manji uliamua kumlipia deni hilo kwa
makubaliano kuwa atakuwa akikatwa kiasi cha Tsh Laki tano katika kila mshahara
wake wa mwezi na ikawa hivyo kweli.
Ngassa ambaye kwa sasa amebakiza mkataba wa miezi mitano
Jangwani, ameuambia mtandao huu kuwa makubaliano hayo yamevunjwa na sasa
anamiezi miwili hapokei mshahara kwa kuwa wanaukata wote.
“Hadi sasa hivi nakatwa, Mshahala wenyewe sipewi,Nacheza tu
kwasababu namaliza muda wangu lakini namshukuru Mungu yeye ndio anajua la
mbele, Walisema watanikata laki tano, wakaja wakaanza kunikata milioni na baada
ya hapo wakaanza kukata yote inamaana hadi hapa mshahara wa miezi miwili
sijapewa kwahiyo siwezi kuidai timu” Amesema Ngassa ambaye ni Mfungaji bora wa
kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka jana.
Akizungumzia namna
alivyoifunga Mtibwa Sugar hapo jana, Ngassa anasema kuwa Kocha Hans Van De
Pluijm alimuambia asitoke katikatika ya mabeki wawili wa wapinzani wao ambao walionekana kuwa wazito
kukimbia.
“Mwalimu aliniambia kwamba wale mabeki wa kati ni wazito
ndio nikazitumia nvyema nafasi, sikuweza kutoka pale katikati” Amesema Ngassa.
Kwa upande wake Kocha Hans Van De Pluijm amesema kuwa
udhaifu wa mabeki wa kati wa Mtibwa Sugar aliuona katika kipindi cha kwanza
ndio maana aliamua kumuingiza Ngassa mwenye kasi kubwa.
“Kitu muhimu ni kuwa
alitakiwa kutumia fursa alizozipata
kwasababu nilijua kuwa toka kipindi cha kwanza kuwa mabeki wawili wa
kati hawakuwa haraka, kwahiyo ninafurahia matokeo tuliyopata” Amesema kocha
huyo aliokuwa akiongea na shaffihdauda.com.
No comments:
Post a Comment