Pages

Monday, February 23, 2015

Serikali kuajiri walimu zaidi ya 35,000


Waziri Mkuu Mizengo
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imepanga kuajiri walimu zaidi ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini. Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Kiwere, mara baada ya kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu kwenye Shule ya Sekondari ya Kiwere, tarafa ya Kalenga, wilayani Iringa.



Alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na mahitaji yaliyowasilishwa na kwamba watakapopata mgao wao hawana budi kuziangalia kwanza shule zenye miundombinu iliyokamilika kama ilivyo kwa shule hiyo.
“Mkoa mzima wa Iringa unahitaji kuwa na maabara 318 na zilizo tayari mpaka sasa ni 108. Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza kujengwa na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao kutakuwa na maabara 249 zilizokamilika,” alisema.
“RC inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo bado hazijaanza kujengwa zikamilike kabla ya Juni mwaka huu kama ambavyo Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameelekeza. Alisema hataongeza tena muda wa ujenzi,” aliongeza. Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo serikali imeamua kuipa umuhimu wa kipekee na kuiweka katika moja ya maeneo sita muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN).
Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe wasikivu ili waweze kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Elimu wa Wilaya ya Iringa, Leonard Msigwa, alisema ujenzi wa nyumba hizo nne ambazo zina pande mbili umegharimu sh. milioni 323.2.
Bw. Msigwa alisema ujenzi wa nyumba ulifanywa na shirika la DESWOS la Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na wananchi. 
Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Afisa Elimu huyo alisema hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya Kemia na Baiolojia lakini bado viko kwenye hatua ya kupaka rangi. 
“Ujenzi wa maabara hadi sasa umekwishagharimu sh. milioni 52.8/- na katika kipindi cha Februari 2015, tumefanikiwa kutengeneza baadhi ya samani za maabara yaani meza 24 na stuli 96 zenye thamani ya sh. 8,940,000/-,” alisema.

No comments:

Post a Comment