Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imepanga
kuajiri walimu zaidi ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari ili
kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini. Alitoa kauli hiyo juzi
wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Kiwere, mara baada ya
kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu kwenye Shule
ya Sekondari ya Kiwere, tarafa ya Kalenga, wilayani Iringa.
Alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule kulingana na mahitaji
yaliyowasilishwa na kwamba watakapopata mgao wao hawana budi kuziangalia
kwanza shule zenye miundombinu iliyokamilika kama ilivyo kwa shule
hiyo.
“Mkoa mzima wa Iringa unahitaji kuwa na maabara 318 na zilizo
tayari mpaka sasa ni 108. Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza
kujengwa na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao
kutakuwa na maabara 249 zilizokamilika,” alisema.
“RC inabidi uwasukume watu wako ili hizi 69 ambazo bado hazijaanza
kujengwa zikamilike kabla ya Juni mwaka huu kama ambavyo Mheshimiwa Rais
Jakaya Kikwete alikuwa ameelekeza. Alisema hataongeza tena muda wa
ujenzi,” aliongeza. Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo serikali
imeamua kuipa umuhimu wa kipekee na kuiweka katika moja ya maeneo sita
muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa ya Haraka (BRN).
Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe wasikivu ili waweze kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Elimu wa Wilaya
ya Iringa, Leonard Msigwa, alisema ujenzi wa nyumba hizo nne ambazo zina
pande mbili umegharimu sh. milioni 323.2.
Bw. Msigwa alisema ujenzi wa nyumba ulifanywa na shirika la DESWOS
la Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja
na wananchi.
Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Afisa Elimu huyo
alisema hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya Kemia na
Baiolojia lakini bado viko kwenye hatua ya kupaka rangi.
“Ujenzi wa maabara hadi sasa umekwishagharimu sh. milioni 52.8/- na
katika kipindi cha Februari 2015, tumefanikiwa kutengeneza baadhi ya
samani za maabara yaani meza 24 na stuli 96 zenye thamani ya sh.
8,940,000/-,” alisema.
No comments:
Post a Comment