Pages

Friday, February 20, 2015

TMAA yagundua njia 400 utoroshaji madini


Dar es Salaam. Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA) umetangaza dau nono kwa yeyote atakayewezesha kukamatwa kwa mfanyabiashara yeyote anayesafirisha madini kwa njia za magendo kupitia njia za panya zaidi ya 400 zilizopo nchini.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta alipokuwa akitoa taarifa ya mwaka uliopita ya mapambano dhidi ya magendo ya madini mbele ya waandishi wa habari.

“Kwa kipindi cha kuanzia Januari mpaka Desemba mwaka jana, wakala umeweza kukamata watoroshaji



 wa madini ya aina mbalimbali katika matukio 27 tofauti. Tunawaomba Watanzania wazalendo kushirikiana nasi ili kuwabaini watu wote wanaojishughulisha na magendo haya na tayari wizara imethibitisha zawadi ya asilimia tano ya thamani ya madini yatakayokamatwa itatolewa,” alisema Mteta.

Wakala umeanza utekelezaji wa mkakati huo ulioratibiwa tangu mwaka 2012 wakati huo Serikali ilisema itatoa asilimia 30 ya thamani ya mzigo baada ya kugundua kuwapo kwa watu wanaolipwa asilimia 10 kusaidia kufanikisha magendo hayo na hivyo kuchangia kuikosesha mapato.

Alisema hilo lilikuwa ni pendekezo linaloendelea kutekelezwa na kwamba, kiasi hicho ni haki ya mtoa taarifa ambaye hatotajwa mahali popote katika mchakato mzima wa hatua za kisheria.

“Utoroshaji wa madini umekithiri, zinahitajika nguvu za pamoja ili kuhakikisha Taifa linanufaika na rasilimali zake. Atakayekamatwa mali yake itataifishwa na kama ni kampuni basi itanyang’anywa leseni yake na kutoruhusiwa tena kufanya shughuli zake hapa nchini,” alisema Mteta.

Kwa madini yanayoingizwa ili yasafirishwe nje bila kuwa na vibali, alisema nayo yakikamatwa yatataifishwa hivyo kuwataka wote wanaofanya hivyo kutumia ofisi za ukaguzi zilizoko mipakani kuhalalisha madini waliyonayo.

Meneja wa Uthaminishaji, George Kaseza alisema njia za panya ni nyingi na wakala huo peke yake hauwezi kufanikiwa kudhibiti, hivyo aliwataka wananchi kushiriki kuziba njia hizo kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au ofisi ya wakala iliyo karibu.

“Nwaka jana tulikamata madini yenye thamani ya zaidi ya Sh850 milioni katika viwanja vyetu vya ndege pekee,” alisema.

Alisema wakala umejitahidi kuimarisha ulinzi na ukaguzi katika viwanja vya ndege kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kama Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.

“Juhudi hizo zimewezesha kukamatwa kwa madini yenye thamani ya Sh8.4 milioni.

“Hiyo ilikuwa ni baada ya kupata taarifa kutoka kwa mwananchi aliyetilia shaka mienendo ya mtuhumiwa. Kesi ipo mahakamani mpaka sasa,” alisema.

No comments:

Post a Comment