Pages

Monday, February 23, 2015

Ujambazi wa kutumia pikipiki walitikisa jiji la Dar


Ujambazi wa kutumia pikipiki unaendelea kulitikisa Jiji la Dar es Salaam, baada ya majambazi wanne waliokuwa na silaha kuvamia duka kubwa (supermarket) katika Barabara ya Mwaikibaki (zamani Old Bagamoyo) majira ya saa 10  jioni juzi na kupora pesa.
Mashuhuda wa tukio hilo waliiambia NIPASHE kuwa, majambazi hao  walikuwa kwenye pikipiki mbili wakiwa na silaha, walifika katika duka hilo linalojulikana kama Lecturer na mara baada ya kuteremka walipiga risasi hewani.

 
Mmoja wa mashuhuda hao ambaye anafanyakazi kwenye saluni ya kutengeneza nywele karibu na duka hilo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Salma, alisema alikuwa amesimama ghorofani kwenye saluni hiyo na kushuhudia majambazi hao wakimchukua mmoja wa walinzi wa duka hilo na kumtanguliza kuingia ndani ya duka hilo.
Alisema majambazi watatu, wawili wakiwa na silaha waliingia ndani huku mmoja wao akibaki nje kuangalia hali ya usalama.
Alisema duka hilo liko karibu na maduka mengine likiwamo duka la dawa, duka la nguo, duka la wakala wa pesa kwa njia ya simu, lakini majambazi hayo yalionekana kulilenga duka hilo.
“Inaonekana walikuwa wana lengo la kuvamia duka hilo, kwa sababu maduka mengine yote hawakuyagusa,” alisema shuhuda huyo. Alisema majambazi hayo yalikuwa yamevaa kofia ngumu (helmet) na wakati wakiingia ndani ya duka hilo hawakuzivua.
“Ni vijana wenye umri kati ya miaka 20 na 25, walikuwa wamevaa kawaida tu, jeans na T-shirt, huwezi kudhani ni majambazi mpaka tulipoona wakitoa bunduki na kupiga risasi hewani ndiyo tukajua kuwa duka lile limevamiwa,” alisema.
Alisema waliingia kwenye duka hilo bila wasiwasi, walichukua muda kama wa dakika 15 kukamilisha lengo lao na walipotoka walikuwa wamebeba begi lililoonekana kuwa lilikuwa na pesa na mfuko wa Rambo mweusi ulioonekana kujaa fedha za sarafu.
Salma alisimulia kuwa baada ya kuchukua fedha hizo, walipanda pikipiki zao na kuondoka huku mmoja wa majambazi aliyekuwa kwenye pikipiki ya nyuma akipiga risasi nyingine hewani.  Hata hivyo, hakuna tukio la kifo wala mtu kujeruhiwa.
Polisi walifika eneo la tukio nusu saa baada ya majambazi hao kutokomea kusikojulikana.
NIPASHE ilipowasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, kutaka kujua kiasi kilichoporwa, alisema yuko kwenye kikao.

No comments:

Post a Comment