Ujambazi wa kutumia pikipiki unaendelea kulitikisa
Jiji la Dar es Salaam, baada ya majambazi wanne waliokuwa na silaha
kuvamia duka kubwa (supermarket) katika Barabara ya Mwaikibaki (zamani
Old Bagamoyo) majira ya saa 10 jioni juzi na kupora pesa.
Mashuhuda wa tukio hilo waliiambia NIPASHE kuwa, majambazi hao
walikuwa kwenye pikipiki mbili wakiwa na silaha, walifika katika duka
hilo linalojulikana kama Lecturer na mara baada ya kuteremka walipiga
risasi hewani.
Mmoja wa mashuhuda hao ambaye anafanyakazi kwenye saluni ya
kutengeneza nywele karibu na duka hilo, aliyejitambulisha kwa jina moja
la Salma, alisema alikuwa amesimama ghorofani kwenye saluni hiyo na
kushuhudia majambazi hao wakimchukua mmoja wa walinzi wa duka hilo na
kumtanguliza kuingia ndani ya duka hilo.
Alisema majambazi watatu, wawili wakiwa na silaha waliingia ndani huku mmoja wao akibaki nje kuangalia hali ya usalama.
Alisema duka hilo liko karibu na maduka mengine likiwamo duka la
dawa, duka la nguo, duka la wakala wa pesa kwa njia ya simu, lakini
majambazi hayo yalionekana kulilenga duka hilo.
“Inaonekana walikuwa wana lengo la kuvamia duka hilo, kwa sababu
maduka mengine yote hawakuyagusa,” alisema shuhuda huyo. Alisema
majambazi hayo yalikuwa yamevaa kofia ngumu (helmet) na wakati wakiingia
ndani ya duka hilo hawakuzivua.
“Ni vijana wenye umri kati ya miaka 20 na 25, walikuwa wamevaa
kawaida tu, jeans na T-shirt, huwezi kudhani ni majambazi mpaka
tulipoona wakitoa bunduki na kupiga risasi hewani ndiyo tukajua kuwa
duka lile limevamiwa,” alisema.
Alisema waliingia kwenye duka hilo bila wasiwasi, walichukua muda
kama wa dakika 15 kukamilisha lengo lao na walipotoka walikuwa wamebeba
begi lililoonekana kuwa lilikuwa na pesa na mfuko wa Rambo mweusi
ulioonekana kujaa fedha za sarafu.
Salma alisimulia kuwa baada ya kuchukua fedha hizo, walipanda
pikipiki zao na kuondoka huku mmoja wa majambazi aliyekuwa kwenye
pikipiki ya nyuma akipiga risasi nyingine hewani. Hata hivyo, hakuna
tukio la kifo wala mtu kujeruhiwa.
Polisi walifika eneo la tukio nusu saa baada ya majambazi hao kutokomea kusikojulikana.
NIPASHE ilipowasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camilius Wambura, kutaka kujua kiasi kilichoporwa, alisema yuko kwenye
kikao.
No comments:
Post a Comment