Watu watatu wameuawa na wengine sita kujeruhiwa
katika mapigano yaliyozuka kati ya wakulima na wafugaji katika Bonde la
Kilimo cha Mpunga la Matembele, lililoko kati ya vijiji vya Mabwegere na
Mbigili, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Waliofariki; wawili wanatoka upande wa wakulima, ambao ni wakazi wa
Kijiji cha Mbigili na mmoja ni mfugaji kutoka jamii ya Kimasai
anayeishi katika Kijiji cha Mabwegere.
Kati ya waliojeruhiwa; wawili hali zao zinadaiwa kuwa ni mbaya na
hivyo, kulazimika kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro kwa
matibabu zaidi.
Mapigano hayo yalizuka juzi zikiwa zimepita wiki mbili baada ya
nyumba 46 zilizokuwa zikimilikiwa na baadhi ya wafugaji wa Kijiji cha
Mabwegere na wakulima kuchomwa moto na kundi linalodaiwa ni la wakulima,
huku wafugaji wa jamii ya Kimasai wakikimbia kuokoa maisha yao.
Akizungumza na waandishi wa habari baada kuwatembelea majeruhi
waliopo katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Joseph, iliyopo katika
mji mdogo wa Dumila, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo,
alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo pamoja na majeruhi.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Joseph Peter (26) na Rajab Nasoro
(55) wote wakulima kutoka Kijiji cha Mbigili na mfugaji wa jamii ya
Kimasai, Kaduhu Kashu, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mabwegele. Wote
walifariki baada kuchomwa vitu vyenye ncha kali katika mapigano hayo.
Waliojeruhiwa ni Binzi Dotto (42) Shigele John, Juma Someke,
Mohamed Athuman, Mbwana Athuman na mfugaji, ambaye jina lake
halijatambulika baada ya kukimbizwa na ndugu zake katika hospitali
isiyofahamika.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi, majira ya kati ya saa 9 na saa
10 jioni, baada ya wakulima wanaokadiriwa kufikia 15 kutoka katika
Kijiji cha Mbigili, kwenda katika Bonde la Matembele wakiwa na matrekta
kwa ajili ya kuanza kutayarisha mashamba ya kilimo cha mpunga. Tarimo
alisema siku mbili kabla ya tukio hilo, aliitisha kikao cha maridhiano
baina ya pande mbili hizo kwa ajili ya kupata suluhisho la mgogoro wa
bonde hilo, lakini upande wa viongozi wa kijiji cha wafugaji cha
Mabwegere haukufika katika mkutano huo.
Aliitupia lawama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kwa kushindwa kupeleka wasuluhishi wa mgogoro huo wa ardhi katika bonde
hilo kama walivyoahidi.
Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Milenia Shayo,
alithibitisha kupokea miili ya watu wawili na mmoja kufariki wakati
akiendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo, alisema kupitia
Afisa Habari wake, Nabwike Mwakatika, kuwa atatoa taarifa baada ya
kutoka kwenye eneo la tukio.
No comments:
Post a Comment