Wafanyabiashara watatu na wanachuo watano wamepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida wakikabiliwa na mashitaka ya
kumdhalilisha kupindukia askari polisi wa kike na kumsababishia maumivu makali
mwilini.
Mwanasheria wa Serikali, Petrida Mutta alidai mbele ya
Hakimu Joyce Minde, kwamba kwa pamoja, washitakiwa hao walimfanyia unyama
askari huyo kwa kumvua nguo zote na kumwacha mtupu kisha kumshambulia na
kumsababishia maumivu makali mwilini.
Waliopandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Joyce Minde,
ni Jasmin Iddi (40), Abdallah Hamduni (26), Ramadhani Bakari (32) wote
wafanyabiashara wa mjini hapa pamoja na dereva, Saidi Saidi (50) .
Wengine ni Aurelia Adolf Mushi (20), Grace Daniel Paul (21),
Happiness Kiluvya (23), Jackline John (20) na Constansia Masaki (21) wanaodaiwa
ni wanachuo katika moja ya vyuo vya elimu ya juu mjini Singida.
Mwanasheria wa serikali, alidai wakati wote wa kitendo hicho
cha udhalilishaji, polisi huyo, alikuwa akichukuliwa picha za video huku akiwa
mtupu na kuzisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Tukio hilo inadaiwa
lilifanyika Februari 14, mwaka huu saa 11.30 jioni ambako kwa mujibu wa
Mwendesha Mashitaka, inadaiwa polisi huyo wa kike alikutwa akiwa na mume wa
mshitakiwa, Jasmin wakiwa kando ya Ziwa Singidani wakivinjari siku hiyo ya
Wapendanao.
Hata hivyo, mume ambaye jina halikupatikana, inadaiwa
alitoroka. Mutta alidai mbele ya mahakama hiyo kuwa kitendo walichofanya
washitakiwa ni kinyume na Kanuni ya Adhabu 138 A kifungu cha 16 cha Mwenendo wa
Makosa ya Jinai kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Wote walikana
mashitaka
CHANZO- masamablog.com
No comments:
Post a Comment